Advertisements

Sunday, February 1, 2015

Lissu alipuka bungeni

Sakata la uchotwaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, limeibuka tena bungeni na kuzua malumbano makali baina ya Mwanasheria Mkuu mpya wa Serikali, George Masaju na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) Tundu Lissu (Anayeongea kwenye Video).

Lissu alilipuka bungeni na kumwambia Masaju kuwa ni mshauri wa serikali na si Bunge kuhusu masuala ya kisheria.

Akizungumza wakati akichangia mjadala uliohusu taarifa za Kamati za Bunge, Lissu alisema kuwa mafisadi wakubwa wanaochota fedha za umma wanaishia kujiuzulu bila ya kushtakiwa lakini watu wadogo aliowaita dagaa ndiyo wanaofikishwa mahakamani.


“Watu wanafanya makosa makubwa dhidi ya umma hakuna hatua inayochukuliwa, waheshimiwa wabunge mnaweza mkauliza, lini mtu amewahi kuwajibika, nani kachukuliwa hatua, yupi amefungwa, tunajua wanajiuzulu ili wakafaidi matunda ya wizi wao, sheria zetu zinasema wajiuzulu, wafilisiwe, washitakiwe na wakipatikana na hatia wafungwe, nani ameshitakiwa, kufilisiwa au kufungwa? 

Alisema wanaoshtakiwa ni wadogo hili ndilo tatizo kubwa na mfano mzuri ni hii habari ya Escrow.

Alieleza kuwa licha ya Bunge kumwondoa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuwafukuza mawaziri, waliochukuliwa hatua ya kufikishwa mahakamani ni watu wadogo waliopewa milioni 80, huku wale waliogawana mabilioni ya fedha wakidunda mitaani.

Kuhusu majaji, alisema waliohusika na sakata hilo Bunge liliazimia wawajibishwe, lakini inashangaza kuona kuwa hata Rais Jakaya Kikwete, hajawachukulia hatua kwa madai kuwa lazima majaji hao waanze kuchukuliwa hatua na mahakama, huku akishangaa nani anayemshauri Rais masuala ya kikatiba na sheria.

Kufuatia madai hayo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Masaju alisimama na kutoa taarifa, ambapo alisema kuwa suala hilo lilishatolewa mwongozo bungeni kwamba mambo ya Escrow yapo mahakamani na hayapaswi kujadiliwa, huku pia kanuni za Bunge zikielekeza kuwa suala likishajadiliwa bungeni halipaswi kurudi tena hadi baada ya mwaka mmoja.

“Maazimio ya Bunge lako ni kwamba serikali ilete taarifa ya utekelezaji maazimio kabla ya kumalizika kwa Bunge la Bajeti lakini hata kabla halijaanza, lakini pia kanuni zinakataza kumhusisha mheshimiwa Rais kujenga hoja kwa namna ya kejeli, kwa hiyo mimi naomba kushauri kuwa tunapopata fursa ya kuchangia tujikite kwenye hoja yetu na tutumie lugha ya staha kwa sababu ndivyo kanuni zinavyoelekeza,” alisema Masaju.

Baada ya taarifa hiyo Lissu aliongeza kuwa ameipata taarifa ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye alimwita mrithi wa Werema (Jaji Fredrick Werema, huku akimweleza kuwa ni mshauri wa serikali na si Bunge kuhusu masuala ya kisheria.

Hatua hiyo ilisababisha Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu kusimama na kumtaka Lissu kutotumia lugha za vijembe badala yake ajenge hoja ili wananchi waelewe ujumbe alioukusudia.

“Humu ndani tupo wabunge ambao tunategemea kwanza kanuni tuzichunguze lakini pia vile vile na namna ya kushughulikia hivi vijembe haviwezi kukubalika, jikite kwenye hoja,” alisema Lissu.

Akiendelea na mchango wake, Lissu alisema hoja yake siyo kumkejeli Rais isipokuwa ni kutaka kuona dhana ya utekelezaji ikifanyika ili kuepusha taifa kuingia kwenye hasara kila mwaka.

“Kama mnataka tufute uchafu huu unaoendelea serikalini, Bunge hili tuanze kuwashughulikia mawaziri na wale wote wanaojihusisha na ubadhirifu wa mali za umma, tuwakamate na kuwafilisi na kuwashitaki hawa walioiba mabilioni haya,” alisema Lisu.

Kwa mara nyingine Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Masaju alisimama kuomba mwongozo na kumtaka Lissu kuendelea kuheshimu mihimili mingine kwa kutozungumzia mambo yaliyo mahakamani.

No comments: