ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, February 8, 2015

Madereva wa malori wasubiri msaada wa Waziri Sitta


“Umewahi kuona madereva wa malori wanasherehekea Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi)? Tunataka na sisi tuwe sehemu ya sherehe hizo kwa sababu tunafanya kazi,”

Dar es Salaam. Chama cha Madereva wa Masafa Marefu (Chamamata) kimempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kumteua Samwel Sitta kuwa Waziri wa Uchukuzi, kikiamini kuwa atatatua kero za madereva hao zilizodumu kwa muda mrefu.
Mwenyekiti wa Chamamata, Clement Masanja alisema hayo jana na kuongeza kuwa Waziri Sitta ataendeleza rekodi yake nzuri ya utendaji.
Masanja alisema zipo sheria mbalimbali zinazosimamia ajira, lakini Serikali imeshindwa kusimamia jambo linalosababisha ajali nyingi zinazoweza kuzuilika.
Masanja alibainisha kero kubwa zinazowakabili madereva wa malori nchini kuwa ni masilahi duni, kutokuwa na mikataba ya kazi na mazingira magumu ya kazi.
Masanja alisema madereva wengi wamezikwa nchi za Jamhuri ya Demokrasia ya Watu wa Kongo (DRC), Rwanda na Burundi bila Serikali kuchukua hatua ya kurudisha miili ya marehemu nchini.
“Umewahi kuona madereva wa malori wanasherehekea Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi)? Tunataka na sisi tuwe sehemu ya sherehe hizo kwa sababu tunafanya kazi,” alisema.
Dereva anayefanya safari zake Dar es Salaam – Kinshasa, Said Mwengele alisema analipwa Sh200,000 kwa mwezi.
Alisema madereva wa Tanzania wamekuwa wakilalamikiwa kwa kusababisha ajali kwa sababu ndiyo wenye mazingira magumu ya kazi ukilinganisha na wa Kenya, Zambia na DRC.
MWANANCHI

No comments: