Dar es Salaam. Serikali imetangaza Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 inayohuisha na kufuta sera kadhaa zilizosimamia sekta hiyo, huku elimu ya msingi ikitakiwa kuwa ya bure na kuishia kidato cha nne, lakini wadau wa elimu nchini wana shaka kama utekelezaji wake utafanyika kwa ufanisi.
Sera hiyo inaweka msingi wa kutatua matatizo mengi ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wadau wa elimu kuanzia ufundishaji hadi maslahi ya walimu, ikitoa matamko ambayo Serikali inatakiwa iyatekeleze, mengi katika kipindi kifupi.
Katika sera hiyo, kutakuwa na mabadiliko makubwa kwenye mfumo wa elimu ya awali, msingi na sekondari utakaokuwa wa muundo wa 1+6+4+2+3+, mfumo ambao utamaanisha kuwa elimu ya msingi ambayo itaanzia chekechea hadi kidato cha nne, itakuwa ni lazima na ya bure, badala badala ya unaotumika sasa wa 2+7+4+2+3+, ikimaanisha chekechea ni miaka miwili, msingi saba, sekondari minne, elimu ya juu ya sekondari miaka miwili na elimu ya juu miaka mitatu na zaidi.
Katika mabadiliko hayo, umri wa kuanza shule pia utabadilika, sanjari na muda wa elimu msingi ya lazima kuwa miaka kumi.
Mabadiliko mengine ni kujumuishwa kwa mitalaa ya mafunzo ya ufundi, teknolojia ya habari ili kuwezesha wahitimu kupata au kuwa na soko nchini au nje.
Pia, sera hiyo imeainisha kuwapo kwa mkinzano baina yake na Sera ya Ajira na Utumishi wa Umma ya mwaka 1999 inayotamka kuwa sifa ya kuajiriwa katika utumishi wa umma kwa masharti ya kudumu ni kiwango cha elimu kisichopungua elimu ya sekondari ya kidato cha nne.
Pia, inaainisha sera hiyo kuwa ushirikiano wa Tanzania na nchi nyingine kikanda na kimataifa umeleta msukumo wa kurekebisha Sera ili kuzingatia masuala ya ushirikiano na utangamano.
Masuala hayo ni pamoja na kuoanisha mitalaa; ulinganifu wa viwango vya elimu na mafunzo; upimaji na utoaji tuzo;
Kutokomeza kutojua kusoma na kuandika pamoja na ulinganifu wa sifa za kujiunga na vyuo vya elimu na mafunzo; na kuleta ulinganifu wa mifumo ya elimu na sifa za wahitimu kikanda.
Kwa kuwa Tanzania siyo kisiwa, sera hiyo inajikita katika kuimarisha utangamano katika elimu na mafunzo ili kumjengea Mtanzania ujuzi, umahiri na uwezo wa kukabiliana na mahitaji yanayojitokeza katika ulimwengu wa kazi na maisha kwa ujumla.
Inasema sera hiyo mpya kuwa tangu kuanza kutekelezwa kwa Sera ya Elimu na Mafunzo (1995), Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo (1996) na Sera ya Taifa ya Elimu ya Juu (1999) kumekuwa na mabadiliko mbalimbali ya kisiasa, kijamii, kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia ambayo yameleta changamoto na kuzifanya Sera hizo zipitwe na wakati.
Inaeleza sera hiyo kuwa mabadiliko ya kiuchumi duniani yamesababisha msukumo kwa nchi zinazoendelea na zilizoendelea ama kubadilisha au kuimarisha sera, programu na mikakati yake ili ziweze kuhimili ushindani wa kiuchumi na kuleta maendeleo endelevu ya kijamii, kisayansi na kiteknolojia.
Akizungumza wakati wa uzinduzi uliofanyika jana kwenye Shule ya Sekondari ya Majani ya Chai, Kiwalani jana, Rais Jakaya Kikwete alisema sera hiyo inajibu hoja mbalimbali na changamoto zinazoikabili sekta ya elimu nchini.
Rais Kikwete alisema elimu bora kwa kila Mtanzania itaamwezesha kukabiliana na changamoto anazokutana nazo.
“Miaka 14 ya utekelezaji wa sera ya sasa kuna mambo yametekelezwa na mabadiliko mengi yamefanyika... sasa tunaanza kufikiria kuwagawia kila mtoto kompyuta mpakato yake kwani tunataka elimu yetu ikidhi mabadiliko hayo,” alisema Rais.
“Tunataka ifikapo 2025 Tanzania iwe na uchumi wa kati na pato la kila Mtanzania lifikie Dola 3,000 (za Marekani). Naamini tutafanikiwa,” alisema.
Aliongeza kusema: “Sera hii itumike kututoa hapa na kutupeleka mbele zaidi, uchumi wa kati na kwa kila mtoto anayeanza darasa la kwanza afike hadi sekondari. Kila shule ya msingi ianze safari ya kuwa na kidato cha kwanza, pili, tatu hadi nne, miaka 10 ya sera hii Taifa liwe limepiga hatua.
Kuhusu Mpango wa Elimu wa Kukuza Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) uliozinduliwa wiki iliyopita na Waziri Mkuu Mizengo Pinda mjini Dodoma, Rais Kikwete alisema: “Mwanafunzi atatakiwa kutumia miaka miwili kujua stadi hizo muhimu.”
“Kuna wanafunzi wanasoma na kufanya mtihani wa darasa la saba wakiwa hawajui KKK, yalikuwa yanatokea hayo kwa kuwa tulikuwa hatujayatilia maanani, lakini sera hii itaondoa hali hiyo.
“Mtoto aliyemaliza miaka miwili, hajui KKK asiende darasa la tatu, atapanda kama atazijua hizo kwani sera inasisitiza kuimarisha muundo wa ufundishaji wa hesabu na masomo ya sayansi,” alisema Rais Kikwete akishangiliwa na walimu wa shule za msingi na sekondari waliokuwapo kwenye hafla hiyo.
Akizungumzia vitabu vya kiada, Rais Kikwete alisema: “Kunatakiwa kuwapo na kitabu kimoja kwa shule zote, sasa kila shule mwalimu ana kitabu chake, tuwe na kitabu kimoja kitakachotumika kutungia mitihani.
“Sasa mnatunga maswali hayamo katika kitabu chochote, watafanyaje vizuri kwa mazingira hayo, hatushindwi kuwa na hili kwani tuna maprofesa ambao wanaweza kabisa kutuandalia vitabu.
“Tusiwalaumu wanafunzi kwa kufeli... mtu anaingia katika mtihani anakutana na swali anasoma hadi anaona wasiwasi kwani hata katika kitabu halimo.”
Akizungumzia changamoto zilizopo, alisema kuwa nyumba za walimu ndilo tatizo ambalo Serikali inaliangalia kwa jicho la pekee katika kuhakikisha kuwa malengo yanayotarajiwa yanafikiwa.
Wakati Serikali ikishughulikia hilo aliwataka walimu kujiepusha na biashara ya elimu pamoja na upendeleo kati ya wanafunzi walionao.
“Mradi unaofuata sasa ni nyumba za walimu vijijini. Walimu ni muhimu katika kuandaa raia wema wa Taifa hili. Wazazi wawe karibu na maendeleo ya watoto wakati Serikali ikiimarisha ukaguzi. Kuanzia sasa, mtoto wa darasa la pili asiyejua kusoma na kuandika asiruhusiwe kuingia darasa la tatu. Elimu ni lazima iwe na thamani,” alisema.
Akigusia suala la ada, Rais Kikwete alisema: “Tutakuwa na ada elekezi, zipo shule za awali ambazo ada zake ni Sh3 milioni wakati chuo kikuu ni Sh1.5 milioni.”
“Hatutazuia kabisa, lakini kama mtu anatoza Sh1 milioni au Sh5 milioni atoe sababu kwa nini anatoza milioni moja au milioni tano ili uendane na hali halisi ya elimu inayotolewa.”
“Sera hii itaimarisha mfumo wa ukaguzi wa shule kwani sasa mwanafunzi anakaguliwa na mwalimu, lakini mwanafunzi bado hatujajua anakaguliwa na nani, lakini sasa sera hii inaelekeza hayo yote.”
Alisema wasomi nchini watumike kuboresha mfumo na maudhui ili elimu yetu ifanane na ile ya nchi zilizoendelea.
Alieleza kuwa wale wanaofanya mitihani ya mitalaa ya kimataifa wanaandaliwa kufanya kazi katika mazingira ya Kiingereza, hivyo nasi tuwe na yetu itakayotutambulisha.
Sera ya sasa inazungumzia msingi kutoka darasa la saba hadi kidato cha nne na Kiswahili kama lugha ya kufundishia katika ngazi zote za elimu huku Kingereza kikitumika kuanzia sekondari na elimu ya juu.
Maoni ya wadau
Waziri Kivuli wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Suzan Lyimo alisema: “Tuliipigia kelele sana sera ya elimu iwepo kwani hii iliyopo imepitwa na wakati... lakini, elimu ya msingi sera inavyosema kuwa itakuwa kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne ni kitu kisichowezekana kutokana na miundombinu iliyopo.”
“Elimu itakuwa bure, lakini michango inafika Sh200,000, Rais (Kikwete) ameshindwa kwa miaka 10 ya uongozi wake kutoa elimu bure hadi anaondoka mwaka huu. Je, ameandaa fedha za kuwasomesha au anaacha mzigo kwa rais ajaye.”
Lyimo, ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu (Chadema) alisema: “Haya ni matatizo ya kuchukua sera zetu (Chadema) bila kutuuliza jinsi zitakavyotekelezeka, sisi ni wazuri sana katika kuandaa mipango na mikakati, lakini utekelezaji wake unakuwa tatizo.
“Hata hii sera yenyewe iliyopo ya mwaka 1995 imeshindwa kutekelezwa hivyo hata hii utekelezaji wake utabaki kama hii iliyozinduliwa.”
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongsco), Mahmoud Mringo alisema: “si kweli kwamba ada zetu ni kubwa, bali zinaendana na ubora wa elimu tunayoitoa, lakini ieleweke kwamba elimu bora ni gharama kubwa.
“Hakuna uwezekano wa kupata elimu bora bila gharama, kama Sh1 milioni au Sh5 milioni ni sahihi kwani watakuwa wamepiga mahesabu yao na naomba ieleweke wazi kwamba hakuna shule inayotoza ada kubwa zaidi ya kuwa tunatoza ada kidogo kuliko ubora wa elimu tunaoutoa,” alisema na kuongeza:
“Hili suala mnaweza kuwa mnaliona juu juu tu, lakini ukweli ni kwamba hakuna upembuzi uliofanyika na kubaini kwamba ada tunazotoza ni kubwa kiasi gani.”
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba alisema kilichozinduliwa ni sawa na matamko, na ili sera yoyote iweze kutekelezeka, inahitaji kutafutiwa ufumbuzi mambo matatu la sivyo hakutakuwa na kipya.
“Kunahitajika kuwapo walimu bora, zana za kufundishia, lakini na walimu wanaolipwa vizuri, kama haya yote yatakuwapo sera itatekelezeka lakini kama yatakosekana utekelezaji hautakuwapo.”
Aliongeza kusema: “Kuna yatakayotekelezwa katika sera hii kama yaliyopangwa kama mambo yaliyohitajika kutoa elimu bora yatakuwapo,” alisema Mukoba
Kaimu mkurugenzi wa taasisi ya HakiElimu, Godfrey Boniventura aliipongeza Serikali kwa kukamilisha sera hiyo ambayo walikuwa wanaisubiri kwa muda mrefu.
“Tunahitaji sera itakayokwenda sambamba na mahitaji ya nchi kama usimamizi, upanuzi, kuondoa matabaka ya elimu hasa viwango vya elimu, lakini angalizo ni je, tutaweza kuitekeleza sera hii kwani sisi ni wazuri sana wa kuandaa mambo na kuyaweka katika maandishi, lakini tatizo linakuja katika utekelezaji wake,” alisema. “Tunasema sekondari hakutakuwa na ada lakini michango ikawa mingi kuliko hata hiyo ada yenyewe, kamati na bodi za shule sasa ni wakati wa kulifuatilia hili kwani ada hazitakuwapo, lakini michango ikaongezeka jambo linaloweza kuwakwaza wazazi.”
Utekelezaji wa sera
Sera hiyo inaeleza kuwa Kingereza kitaendelea kutumika sambamba na Kiswahili katika ngazi ya sekondari na elimu ya juu hadi rasilimali zitakapowezesha Kiswahili kutumika peke yake. Hata hivyo, mchumi wa Kitengo cha Sera cha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Calistus Chonya alisema kwa sasa ni vigumu kueleza ni lini sera hiyo itaanza kutumika kwa sababu itatakiwa kupitia hatua mbalimbali kabla ya kuanza kutumika.
“Kuzinduliwa kwa sera hii haina maana kuwa itaenda kutumika mara moja, ni lazima ipitie michakato mingine kama vile kuandaa mpango mkakati na muswada wa sheria kupitishwa bungeni,” alisema.
Mfumo wa elimu mpya chini ya sera hii utakuwa hauna mtihani wa darasa la saba kama ilivyo sasa, bali kutakuwa na vipimo katika ngazi ya darasa moja kwenda jingine vitakavyowezesha kujua uelewa wa kitaaluma wa wanafunzi kabla ya kufika kidato cha nne.
Mkurugenzi msaidizi wa sera wa wizara hiyo, Atetaulwa Ngatara alisema vipimo hivyo vitamwezesha mwalimu kujua udhaifu wa mwanafunzi na kuandaa utaratibu maalumu wa kuwafundisha ili kutatua upungufu waliona nao bila kurudia darasa.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki akimkaribisha Rais Kikwete, alisema jitihada za uongozi wake katika taifa hili umefanikiwa kuongeza Shule za Sekondari za Serikali kutoka 10 na kufikia 135 katika mkoa huo. Baadhi ya shule hizo ni Jangwani, Azania, Kisutu, Zanaki, Kibasila, Jamhuri na Chang’ombe.
“Katika kila shule tumejenga maabara tatu (maabara za fizikia, kemia na baiolojia) 281, kabla ya ujenzi tulikuwa na maabara 181 hii yote ni matunda ya uongozi wako makini na unaothamini elimu.”
Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia Elimu, Kassim Majaliwa alisema: “Tutahakikisha utekelezaji wa sera hii unafanikiwa kwa mafanikio makubwa.”
Takwimu za udahili
Alitoa takwimu zinazothibitisha kuwa baada ya muda mfupi Tanzania itaizidi Kenya iliyo juu kwa sasa katika udahili wa wanafunzi katika ngazi zote kuanzia msingi mpaka chuo kikuu.
Alisema mwaka 2005 Kenya ilikuwa na wanafunzi 925,340 katika shule za sekondari pamoja na 108,470 vyuo vikuu ikifuatiwa na Uganda wakati Tanzania ilikuwa na wanafunzi wasiofika hata nusu yake. Ilikuwa na wanafunzi 40,719 vyuo vikuu.
Lakini mpaka mwaka jana mabadiliko makubwa yametokea kwani tayari Tanzania imeipiku Uganda kwa udahili. Kenya inadahili wanafunzi milioni mbili wa sekondari na Tanzania ni 1.8 milioni, ikifuatiwa na Uganda wenye 1.3 milioni. Kenya wana wanafunzi 300,000 vyuo vikuu, Tanzania 250,000 na Uganda 140,000.
Alisema idadi hiyo ni kubwa kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita na kukumbusha kuwa wakati Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu inaanzishwa kulikuwa na nafasi 74,000 lakini ni wanafunzi 38,000 tu ndiyo walikuwa wanahitimu kidato cha sita.
Alisema: “Hata kama wangefaulu wote bado isingewezekana kujaza nafasi zilizokuwepo. Lakini hivi sasa tuna uwezo wa kujaza vyuo vyetu vilivyopo. Wakati ule kulikuwa na vyuo vikuu 26 lakini sasa vipo 50.”
Imeandikwa na Ibrahim Yamola, Julius Mathias na Goodluck Eliona wa Mwananchi
No comments:
Post a Comment