
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (kulia) akipokea Tuzo ya Kimataifa ya mwaka ya Maendeleo ya Udhibiti wa Sekta ndogo ya Mafuta na Gesi inayotolewa na Kampuni ya Kimataifa ya Wildcat International, ya nchini Marekani kupitia machapisho yake maarufu Duniani ya The Oil & Gas Year (TO&GY). Anayemkabidhi Tuzo hiyo ni Mratibu wa Mahusiano kwa Wateja kutoka Jarida la TO&GY, Bi. Laura Carr.
Wizara ya Nishati na Madini imepata Tuzo ya Kimataifa ya mwaka ya Maendeleo ya Udhibiti wa Sekta ndogo ya Mafuta na Gesi.
Tuzo hiyo ya mwaka 2014 inayotolewa na Kampuni ya Kimataifa ya Wildcat International, ya nchini Marekani kupitia machapisho yake maarufu Duniani ya The Oil & Gas Year (TO&GY), imekabidhiwa rasmi jijini Dar es Salaam kwa Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene ambaye alipokea Tuzo hiyo kwa niaba ya Wizara.
Tuzo hiyo, iliyotolewa na Mratibu wa Mahusiano kwa Wateja kutoka Jarida la TO&GY, Bi. Laura Carr inaitambua Wizara kutokana na mafanikio yake katika kushughulikia changamoto za udhibiti wa sekta ndogo ya mafuta na gesi na hivyo kuchochea maendeleo ya sekta hiyo.
Mafanikio hayo ni pamoja na kuwa na sera mpya ya gesi asilia, kuwa na muundo mpya wa makubaliano ya gharama za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi (Production- Sharing Agreement), na kuwa na Rasimu ya Sera Uwezeshaji na Ushirikishaji Wazawa (local content policy).
“Hayo ni baadhi tu ya maendeleo yaliyofanya sekta hii kueleweka na kukubalika zaidi kwa wawekezaji na wadau,” imesema sehemu ya Jarida la TO&GY.
Pamoja na Tuzo ya Wizara ya T0&GY, Shirika la Umeme nchini kupitia Mkurugenzi wake, Mhandisi Felchesmi Mramba ameshinda Tuzo ya Mtu wa Mwaka (Person of the Year, 2014) kutokana na mpango yake ya Dola za Kimarekani Bilioni Sita zitakazowezesha TANESCO kuongeza uzalishaji umeme mara tatu zaidi ya sasa kutokana na vyanzo mbalimbali kama makaa ya mawe, gesi asilia na maji hivyo kuondokana na utegemezi wa uzalishaji umeme kwa kutumia mafuta.
Aidha Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) limeshinda Tuzo ya transition of the year (2014) kutokana na kupiga hatua katika shughuli zake ambapo mbali ya kuwa kuwa mdhibiti wa sekta ndogo ya mafuta na gesi bali pia limekuwa mwekezaji baada ya kushinda tenda na kupata vitalu viwili kwa ajili ya utafiti wa mafuta na gesi nchini.
Usambazaji wa machapisho ya TO&GY hukaguliwa na Taasisi ya Marekani ya BPA Worldwide inayokagua machapisho maalum zaidi ya 2600 katika nchi 30 Duniani yakiwemo majarida maarufu ya Toronto Star, Wall Street Journal na Gulf News.
1 comment:
its so sad tunakenua midomo tu na kucheka cheka na huku wageni wanalamba dume ya haya madini yote yetu.what a shameeeeeeeeeeeeeeeeee.
hakuna mzawa aliye na uchungu na nchi hii wala nini.
Post a Comment