ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 26, 2015

BVR zaiweka Nec mtegoni. Yaandikiwa barua isitishe uandikishaji kuepusha vurugu.

Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imetakiwa kumshauri Rais Jakaya Kikwete, kusitisha upigaji kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa Aprili 30, mwaka huu, kwa maelezo kuwa kulazimisha suala hilo kutasababisha mpasuko na hatimaye kuzua vurugu na kuvunja amani ya nchi.

Pia imetakiwa kutokubali kuingiliwa katika utendaji wake wa kazi ikiwamo kulazimishwa kuendesha mchakato wa kura ya maoni katika tarehe hiyo.

Matamko hayo yalitolewa kwa nyakati tofauti na Baraza la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Dar es Salaam Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) jana.

Wazee hao wakimtaka Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva (pichani), kumshauri Rais Kikwete, kusitisha upigaji kura hiyo, Jukata limeitaka serikali kuacha kuingilia utendaji kazi wa Nec kuhusu daftari hilo na kuilazimisha kuendesha mchakato huo katika tarehe hiyo.

Pia wamemwandikia Jaji Lubuva barua kumsisitiza kutekeleza ombi lao hilo.

Mwenyekiti wa Baraza hilo, Ester Samanya, alisema wanamshauri hivyo Jaji Lubuva kwa kuwa wanaamini kuwa hadi ifikapo tarehe hiyo, uandikishaji wa wananchi kwenye daftari la kudumu la wapigakura unaoendelea mkoani Njombe kwa kutumia mfumo mpya wa teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR) utakuwa haujakamilika kote nchini.

Alisema hali hiyo inatokana na nyenzo za kufanikisha kazi ya uandikishaji wapigakura katika daftari hilo, ikiwamo muda, vifaa na wataalamu, kutoandaliwa.

Samanya alisema kauli zinazokinzana kati ya Jaji Lubuva na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, juu ya uwezekano wa kura hiyo kupigwa katika tarehe hiyo au la, zinaashiria kuwa serikali inataka mtu wa kufa naye.

Alisema serikali inataka kuonyesha kuwa Jaji Lubuva ndiye aliyeshindwa.

“(Kauli ya Pinda ya kulazimisha) inataka kuonyesha Lubuva ndiye aliyeshindwa,” alisema Samanya.

Hivyo, alimshauri Jaji Lubuva kutokubali kuingia kwenye kashfa ya kujivunjia heshima, badala yake amshauri Rais Kikwete kusitishwa mchakato huo.

“Ili kuiepusha nchi na uvunjifu wa amani, uandikishaji usitishwe. Hilo siyo msiba, lazima liandaliwe. Kulilazimisha, ni sawa na kulazimisha jogoo kutaga. Lubuva asiwe mbuzi wa kafara,” alisema Samanya.

Aliongeza: “Tunachokiona ni fujo inayotaka kutokea, kwani hilo (la kura ya maoni) haliwezi kutekelezeka.”

Kaimu Katibu Mkuu Baraza hilo Taifa, Erasto Gwota, alisema uandikishaji wapigakura kwa kutumia mfumo wa BVR katika nchi nyingi umefeli na kwamba, unafanywa nchini ili kuvuruga uchaguzi mkuu ujao.

“Lubuva amshauri Rais jambo hili lisitishwe. Tukilazimisha hili, wengine watakosa kupiga kura,” alisema Gwota na kushauri kura ya maoni ipigwe baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Katika barua yao yenye kichwa cha habari: “Uandikishaji wa wapigakura kwa kutumia BVR hapa nchini, ambayo ilitarajiwa kupelekwa Nec jana, walimtaka Jaji Lubuva kuangalia upya uandikishaji wa wapigakura kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.

Wanasema hali halisi waliyoiona mkoani Njombe, itawafanya Watanzania wengi kunyimwa haki ya kutopiga kura, ambayo ni haki ya mwananchi kuchagua viongozi wanaowataka.

“Mheshimiwa, tumeona ni jinsi gani vifaa hivyo kuwa ni vichache mno, havitoshelezi na kukidhi haja ya wananchi, ambao ni wengi na wanahitaji kujiandikisha kwa wingi na kwa shauku kubwa sana hasa vijana, ambao hapo awali hawakuwahi kujiandikisha katika daftari la wapigakura lililopita la mwaka 2004 na 2009,” ilieleza sehemu ya barua ya wazee hao iliyosainiwa na Madeni Kapiriro kwa niaba ya wazee hao.

Wanasema pamoja na uchache wa vifaa, wameshuhudia watumishi wa Nec wanashindwa kutumia BVR kwa kazi kama inavyotakiwa.

“Kwa kuwa wewe ni mzee mwenzetu ambaye umepewa dhamana hii ya kusimamia zoezi hili, tunakushauri kwamba heri ukaiambia serikali kwamba mpango huu si sahihi, hivyo tunaomba umwambie Rais usitishwe kabisa ili utafutiwe ufumbuzi mwingine kabla muda kwisha, hasa kwa kuwa serikali imeshindwa kukupa vifaa kwa ajili ya kazi hiyo kama ulivyoomba,” wanasema wazee hao.

Wanaongeza: “Kumbuka kwamba wazee ni hazina ya busara na hekima. Tungependa kuona unatumia busara na hekima. Suala la BVR ni lazima limfikie kila Mtanzania, ambaye ana umri wa kumwezesha kupiga kura (miaka 18 na kuendelea).” Wanasema hiyo itafanya Watanzania wengi kupata fursa ya kutumia demokrasia yao ya kuweka uongozi wanaoutaka kwa ustawi wa maisha yao.

Wanaongeza: “Tunakuomba kama wazee wenzako, umshauri Rais Kikwete kuwa mpaka ifikapo Aprili 30, mwaka huu zoezi la uandikishaji wapigakura nchi nzima litakuwa halijakamilika na hivyo kuendelea kusisitiza kuwa kura ya maoni ikifanyika tarehe 30 Aprili itasababisha uvunjifu wa amani kwa maeneo ambayo hawajajiandikisha na hawajui ni lini zoezi litawafikia."

Alisema: “Ni vyema ukalitangazia taifa mapema ili kuondoa hofu ambayo imetanda miongoni mwa wananchi wetu na ambayo ikiachiwa kama ilivyo itasababisha mpasuko na hatimaye vurugu kwa taifa letu, ambalo ni kisima cha amani na tunasifika kwa hilo."

Aliongeza: “Kumbuka kwamba sisi Watanzania, ambao leo hii ni wazee, tumekuzwa kwa kutumia sheria, hivyo ni wajibu tuendelee kutumia sheria hii ili taifa letu lipate kustawi kwa vizazi vijavyo. Hivyo, tunakuomba ufikishe salamu hizi kwa Rais Kikwete naye ahusike na kusitisha suala zima la kupiga kura ya katiba inayopendekezwa mpaka hapo baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba. Taifa liandaliwe kwa ajili ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu. Tunaomba kuwasilisha ushauri wetu huu mbele yako ili ufanyiwe kazi kikamilifu.”

Jukata
Jukata imeitaka serikali kuacha kuingilia utendaji kazi wa Nec kuhusu daftari hilo pamoja na kuilazimisha kuendesha mchakato wa kura ya maoni katika tarehe hiyo.

Jukata pia imeitaka serikali kutekeleza jukumu la kuwezesha upatikanaji wa fedha na vifaa vya uandikishaji wapigakura katika daftari hilo kwa kutumia mfumo mpya wa BVR.

Kaimu Mwenyekiti wa Jukata, Hebron Mwakagenda, alisema hayo wakati akitoa tamko kuhusu mwelekeo wa kura ya maoni iliyopangwa kufanyika katika tarehe hiyo.

Alisema kura hiyo haitaweza kufanyika kwa vile pamoja na kuandikwa kwa lugha ya Kiingereza, upatikanaji wa sheria ya kura ya maoni umekuwa ni wa kiwango cha chini.

Mwakagenda alisema utafiti mdogo uliofanywa na Jukata, umebaini kuwa Watanzania wengi hawajawahi kuisoma sheri hiyo iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano mwaka 2013.

Alisema pia maoni kutoka wadau kuhusu sheria hiyo, yameonyesha kuwapo na vifungu vyenye utata, ambavyo vimeibua hisia kuwa vinaweza kutumika kuhakikisha katiba inayopendekezwa inapigiwa kura ya ndiyo.

Hata hivyo, Jukata iliitaka serikali kukamilisha makubaliano ya kusitisha mchakato wote wa katiba, yaliyofikiwa Chamwino, mkoani Dodoma kati ya Rais Kikwete na vyama vya siasa, ambavyo ni wanachama wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Hili swala limekuwa likifanyiwa mazoezi kimzaha na wala sio seriousness! Ni bora kuliacha kwa wakati huu na muda ulobakia hautoshi kulazimisha ni kuleta vurugu.