Walioteuliwa ni Dk. Grace Khwaya Puja na Innocent Sebba, ambao uteuzi wao umeanza Machi 20, mwaka huu.
“Rais amefanya uteuzi huu kwa mamlaka aliyopewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 66 (I) (e), ambapo amepewa mamlaka ya kuteua wabunge wasiozidi 10,” ilieleza sehemu ya taarifa ya iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, jijini Dar es Salaam jana. Uteuzi huo umekamilisha idadi ya wabunge, ambao Rais Kikwete amepewa kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo kikatiba.
Wabunge, ambao wameshateuliwa na Rais ni pamoja na Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia); Prof. Sospeter Muhongo na Dk. Asha-Rose Migiro (Waziri wa Katiba na Sheria). Wengine ni Janet Mbene (Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara); Saada Salum Mkuya (Waziri wa Fedha), Zakhia Meghji, Shamsi Vuai Nahodha na James Mbatia (Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi).
KUFANYA KAZI YA UBUNGE KWA MIEZI MINNE TU
Uteuzi wa wabunge hao wapya uliofanywa na Rais Kikwete kipindi hiki, utawafanya wafanye kazi ya ubunge kwa miezi minne tu kabla ya Bunge la 10, lililoanza Novemba, 2010, kuvunjwa Julai, mwaka huu.
Kwa sasa Bunge hilo linaendelea na mkutano wake wa 19, mjini Dodoma kabla ya kuhitimisha wa 20 na wa mwisho, unaotarajiwa kufanyika kwa miezi miwili mfululizo, kuanzia ama mwezi ujao au Mei, mwaka huu.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Elimu na Ushirikiano wa Kimataifa wa Bunge, Jossey Mwakasyuka, alifafanua jana kuwa, jumla ya mikutano ya Bunge moja huwa 20 katika kipindi cha miaka mitano ya uhai wake.
Hivyo, akasema Bunge la sasa, limebakiza mkutano mmoja kukamilisha jumla ya mikutano yake 20.
Alisema mkutano pekee wa Bunge la sasa uliosalia ni wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016, ambao unatarajiwa kuanza mwezi ujao.
Hata hivyo, alisema mkutano huo wa 20 wa Bunge la sasa utafanyika mwezi huo iwapo tu mchakato wa kura ya maoni ya wananchi kuamua ama kuikubali au kuikataa katiba inayopendekezwa itaamuliwa na serikali kutokuwapo. Alisema iwapo serikali itaamua mchakato wa kura hiyo uwe Aprili, mkutano wa 20 wa Bunge la sasa utaanza Mei.
NAO PIA WATALIPWA KIINUA MGONGO
Kuhusu uwezekano wa wabunge hao wapya kulipwa kiinua mgongo, Mwakasyuka alisema watalipwa bila shaka yoyote. Hata hivyo, alisema watalipwa kiinua mgongo kulingana na muda watakaolitumikia Bunge.
“Kisheria, mbunge hulipwa kiinua mgongo kwa muda ambao amefanya kazi (za Bunge),” alisema Mwakasyuka.
Alisema wabunge wote hulipwa sawasawa, ingawa kila mmoja hulipwa kuanzia alipoanza kufanya kazi za Bunge hadi atakapomaliza muda wake na kwamba, hulipwa asilimia ya mshahara wake.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
Si lazima kutumia viungo vyote vilivyopo kabatini ili kutengeneza mchuzi mzuri..wakati mwingine busara , maono na utaifa vi natakiwa vitangulie mbele..
Post a Comment