ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 27, 2015

Nape ampongeza Lowassa.

Siku moja baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kusitisha makundi yanayokwenda kumshawishi kugombea urais, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, amempongeza kwa kutii agizo la chama hicho.

Nape amesema hatua hiyo ya Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli ni nzuri kwa kuamua kusitisha makundi kwenda kumshawishi agombee urais, ambayo kwa siku chache mfululizo yalikwenda nyumbani kwake Monduli na mjini Dodoma kwa nia hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana akiwa katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulahman Kinana wilayani Same, Kilimanjaro, Nape alisema anampongeza Lowassa kwa kuwa amekubali kuheshimu kanuni, taratibu na Katiba ya chama ambayo ndiyo inatakiwa kufuatwa na kila mwanachama wa CCM.

Jumanne wiki hii, Nape alimuonya Lowassa kujiepusha na makundi hayo kwa kuwa kufanya hivyo ni kukiuka kanuni na taratibu za chama na kwamba, hali hiyo inamkosesha sifa ya kuteuliwa kugombea urais kupitia CCM.

Nape alisema walimtaka Lowassa, ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM azuie makundi yanayokwenda nyumbani kwake kwa ajili ya kumtaka agombee urais kwani kilichokuwa kinafanyika ni kuanza kampeni kabla ya wakati.

“Kilichokuwa kinafanyika ni kuanza kampeni kabla ya wakati na kwa mujibu wa chama chetu ni makosa, maana anakiuka taratibu na kanuni za chama. Hatuwezi kukaa kimya wakati kanuni zinavunjwa wazi, hivyo nimpongeze Lowassa kwa kutii agizo la chama,” alisema Nape.

Kuhusu shutuma kuwa kauli anazozitoa siyo za chama bali zake binafsi, Nape alisema yeye ndiye msemaji pekee wa chama na hakuna msemaji mwingine, hivyo kauli zinazotolewa ni za chama na siyo zake.

“Kanuni na taratibu ambazo nazisimamia zipo miaka mingi kabla ya mimi kuzaliwa. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM nchi nzima niko peke yangu, hivyo lazima nisimamie misingi ya itikadi pamoja na kanuni na katiba ya chama chetu. Kwa nafasi yangu siwezi kukaa kimya wakati kuna watu wanakosea,” alisema Nape.

Akizungumzia kuhusu wapambe wa makada wanaotaka urais, Nape aliwataka kuwa makini wasije wakawaharibia sifa wagombea wao.

“Ni vizuri wataka urais wakawa makini na ushauri kutoka kwa wapambe wao kwani wanaweza kuwasababishia kukosa sifa ndani ya chama, nawashauri wote wanaotaka kugombea urais kupitia CCM kutowasikiliza wapambe wao kwa kila wanachoambiwa, maana kuna ushauri mwingine unaweza kuwakosesha sifa za kugombea urais,” alisema Nape.

Alisisitiza kwamba, kwenye hilo si kwa wapambe wa Lowassa tu, bali ni kwa wapambe wote waliopo nyuma ya makada wanaotaka kugombea urais mwaka huu.

“Ni muhimu kwa makada wote kuhakikisha wanaheshimu kanuni, taratibu na miiko ya chama ili wawe salama, kinyume cha hapo watajipoteza sifa,” alisisitiza Nape.

Aliwahakikishia makada wa CCM kwamba chama hicho kitatenda haki kwa kila anayeomba nafasi ya uongozi na hakuna atakayenyimwa haki yake.
“Kwa wote ambao watakuwa makini katika kuzingatia kanuni na taratibu za chama, haki zao zitalindwa, lakini wale ambao watakiuka kwa makusudi, hao hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao,” alisema na kuongeza:

“Ndio maana tunaendelea kuwakumbusha makada wote wazingatie kanuni na katiba ya chama chetu. Kinyume cha hapo watakuwa wanajinyima wenyewe haki ya kuomba ridhaa ya kugombea kupitia chama hiki.”

Juzi Lowassa aliwataka wanaotaka kumshawishi wasubiri utaratibu utakaotolewa na chama hicho kuhusiana na suala hilo.

Alitoa kauli hiyo baada ya kutembelewa na vijana 60 waendesha bodaboda kutoka wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya.

KASKAZINI WATOA TAMKO
Zaidi ya vijana 100 wakiwamo wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara, wamekutana mjini Moshi na kutoa tamko linalodai kwamba, iwapo Lowassa atapoteza sifa za kugombea urais, CCM kijiandae kisaikolojia kwa sababu kinaweza kupasuka na kushindwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Vijana hao kutoka Jumuiya za Vyuo Vikuu vya Kanda ya Kaskazini na wengine kutoka sekta binafsi, walitoa angalizo hilo jana mjini Moshi kwa waandishi wa habari, ikiwa ni siku moja tangu Lowassa ajibu kauli ya Nape aliyoitoa Jumanne akidai hawezi kuzuia mafuriko kwa mkono.

Akisoma tamko hilo, Mratibu wa marafiki wa Lowasa wa Kanda ya Kaskazini, Noel Nnko, alisema vijana katika mikoa hiyo hawatasita kuendelea kumshawishi Lowassa kutangaza nia ya kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho kwa kuogopa kauli ya Nape.

Walidai kauli yake ambayo haina baraka za chama inawadhihirishia Watanzania kwamba kuna mgombea wanayemtaka na si anayetakiwa na wananchi.

TUNASUBIRI MTEULE WA CCM
Wakati vijana hao wa kisema hayo, Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu wa CCM Mkoa wa Mbeya, limetoa tamko la kutomuunga mkono mtu yeyote ambaye ametangaza nia ya kugombea urais kwa sasa mpaka pale vikao halali vya chama vitakapomteua mtu anayefaa kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Tamko hilo lilitolewa jana na uongozi wa shirikisho hilo, ikiwa ni siku kadhaa baada ya kuibuka kwa watu waliojitambulisha kuwa ni viongozi wa shirikisho hilo kuzungumza na waandishi wa habari mjini hapa na kutangaza kumuunga mkono na kumshawishi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya, kuchukua fomu ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Mwenyekiti wa shirikisho hilo, Raymond Mweli, alisema kwa sasa shirikisho hilo halimuungi mkono kada yeyote wa CCM aliyetangaza nia wala halimshawishi mtu yeyote kutangaza nia kwa ahadi ya kumuunga mkono, kwa maelezo kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha maadili ya shirikisho hilo na CCM.

Alisema shirikisho linasubiri vikao halali vya chama kumteua mtu ambaye atasimama kugombea urais kwenye uchaguzi huo na kwamba huyo ndiye watakayemuunga mkono na kuhakikisha anashinda kwenye uchaguzi huo.

“Shirikisho kwa sasa halina mgombea wa urais wala nafasi yoyote ya uongozi, kwa maana ya wabunge na madiwani, shirikisho linaamini katika vikao halali vya Chama Cha Mapinduzi, linaamini juu ya maadili ya chama na tunaamini kuwa wakati ukifika CCM kitatuletea mtu anayetosha na si kwamba atatosha ndani ya chama tu, bali hata nje ya chama kwa maana ya kuuzika kwa Watanzania,” alisema Mweli.

Alisema pamoja na msimamo huo wa shirikisho, wanafunzi ambao ni wanachama wa shirikisho hilo mmoja mmoja au kwa makundi yao wanaweza kuwa na misimamo yao au kuwaunga mkono watu wanaowaona wanafaa, lakini kamwe mitazamo hiyo haitakuwa mitazamo ya shirikisho hilo.

Akisoma tamko la shirikisho la wanafunzi hao wa vyuo vya elimu ya juu la CCM mkoa wa Mbeya, Katibu wa shirikisho hilo, Karim Nyanga, alisema watu waliojiita viongozi wa shirikisho hilo na kutangaza kumuunga mkono Prof. Mwandosya, hawajawahi kuwa viongozi wa shirikisho hilo na kwa kufanya hivyo hawalitakii mema shirikisho lao, CCM na taifa kwa ujumla.

Imeandikwa na Augusta Njoji, Same, Emmanuel Lengwa, Mbeya na Godfrey Mushi, Moshi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: