ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 27, 2015

KAULI NZURI NDIYO MSINGI WA MAPENZI!BORA! 2

Wiki iliyopita, tulianza kujadili jinsi kauli nzuri zinavyoweza kujenga au kubomoa penzi lako. Unachopaswa kuzingatia katika maisha yako ya kila siku, ni kuchunga kauli zako uwapo na mwenzi wako.Kauli mbaya, hata kama ni ndogo namna gani, inaweza kusababisha mwenzi wako akakuchukia na kupunguza kabisa mapenzi kwako.

Pia kauli nzuri, mazungumzo ya kufurahisha na ya busara, yana uwezo mkubwa wa kuboresha mapenzi na kumvuta zaidi mwenzi wako.Yafuatayo ni mwendelezo wa mazungumzo ambayo yanaweza kumfanya mwenzi wako azidi kukupenda.

MAZUNGUMZO KUHUSU KAZI
Pata muda wa kuzungumza na mwenzi wako kuhusu kazi. Kama nyote mmeajiriwa, anza kwa kumueleza mambo yanayokukera kazini kwenu, mfano ukali wa bosi wako au umbali kisha utamsikia na yeye akizungumza yake. Kama mmoja wenu hafanyi kazi, jenga mazoea ya kumsimulia jinsi siku yako ilivyokuwa ukiwa kazini au nyumbani. Itamfanya ajihisi ana umuhimu mkubwa kwako.

Msimulie ndoto za maisha yako, labda kwa mfano unapenda kufikia wapi baada ya mwaka mmoja, miwili au mitano ukiwa naye. Hiyo itamjenga na kumuaminisha kwamba kumbe atakuwa na maisha marefu na wewe, jambo litakalozidi kumfanya akupende.

MAZUNGUMZO YA KUMBUKUMBU NZURI
Mkumbushe jinsi ulivyojisikia siku ya kwanza mlipokutana naye. Ni wazi kwamba kila mmoja alikutana na mpenzi wake katika mazingira tofauti kabisa. Hebu jaribu kukumbuka mambo mazuri yaliyotokea siku hiyo na mkumbushe mpenzi wako jinsi ulivyojisikia tangu mara ya kwanza ulipokutana naye.

Bila shaka mada hiyo itamfurahisha sana. Hata kama yapo mambo yasiyofurahisha ambayo yalitokea siku hiyo, usiyazungumzie badala yake mwambie jinsi moyo wako ulivyojawa na upendo wa dhati. Utashangaa jinsi hisia zake zitakavyorudi nyuma na kuwa mpya. Hata kama mmeishi miaka mingi, atakuona kuwa mpya kwake.

MAZUNGUMZO YA VITU ANAVYOVIPENDA
Imezoeleka katika jamii kwamba wanawake ndiyo watazamaji wazuri wa vipindi vya TV au tamthiliya huku wanaume wengi wakipendelea muvi au soka. Jenga utaratibu wa kuwa unafuatilia vitu anavyovipenda mwenzako.

Kwa mfano, kama wewe ni mwanaume na unajua mpenzi wako anafuatilia tamthiliya nzuri inayooneshwa kila wiki, jitahidi kuijua japo kidogo kisha mkiwa wawili, anzisha mazungumzo na mwenzako kuhusu tamthiliya hiyo.
Utashangaa utakavyoukonga moyo wake, kwani atakusimulia kuanzia mwanzo hata vitu ambavyo huvijui. Atajisikia raha kuzungumza na wewe kwa sababu atajua unajali vitu anavyovipenda.

Kama wewe ni mwanamke na unajua mumeo anashabikia timu fulani ya soka, jitahidi japo kuwajua wachezaji wachache wa timu husika na ratiba zake kisha ukiwa na mumeo, anzisha mada hiyo. Atafurahi sana na mtazidi kuuboresha ukaribu wenu.

MAZUNGUMZO KUHUSU MARAFIKI ZAKE
Kuwajua marafiki wa mpenzi wako, huwa ni hatua nyingine ambayo itakusogeza jirani zaidi na mpenzi wako. Simaanishi kwamba uanze kuchunguza udhaifu wa marafiki zake, uwe na mazoea nao au uwe na namba zao za simu! Hapana.

Wajue kwa majina, kazi wanazozifanya na maisha yao japo kwa kifupi ili mpenzi wako anapokupigia stori za rafiki yake fulani, uwe angalau unamjua kidogo na kuchangia naye mazungumzo.

Kuwajua marafiki zake, kunaweza pia kukusaidia kuijua vyema tabia ya umpendaye na kuweza kumdhibiti mapema au kumpa msaada pale anapohitaji ili wasije wakavuruga uhusiano wenu (maana marafiki wengi hawaaminiki).Ni hayo tu! Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Kama kuna mada ungependa tuijadili, nitumie sms kwa namba za hapo juu.

GPL

No comments: