ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 24, 2015

Mtihani mgumu kwa Ukawa .... isome makala hii kwa makini na mwishowe utoe maoni yako

Dar es Salaam. Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju amesema madai ya wadau ya kutaka Tume Huru ya Uchaguzi, mgombea binafsi na haki ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais mahakamani, yatafanyiwa kazi iwapo Katiba Inayopendekezwa itapitishwa kwenye Kura ya Maoni Aprili 30.
Jambo hilo ni mtihani mgumu kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao umetangaza kususia kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa huku ikitaka mambo hayo matatu yafanyiwe kazi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Katika mazungumzo yake na wahariri na viongozi wa magazeti yanayochapishwa na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen jana, Masaju pia alitumia takribani saa mbili kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu suala la kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi.
Akizungumza kwenye ofisi za makao makuu ya Mwananchi Communications Tabata Relini jijini Dar es Salaam jana, Masaju alisema mambo hayo ni muhimu sana katika kipindi hiki na hivyo ni muhimu kwa wananchi kupitisha Katiba Inayopendekezwa ili masuala hayo yaandaliwe utaratibu wa kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.
Katika mkutano wa pamoja na Rais uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, vyama vya upinzani, vikiongozwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vilitoa hoja ya kutaka mchakato wa Katiba Mpya uahirishwe hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba na kwamba katika kipindi hiki Katiba ya sasa ifanyiwe marekebisho ili Tume ya Uchaguzi iwe huru, kuingiza mgombea binafsi na haki ya kupinga mahakamani matokeo ya uchaguzi wa Rais.
“Mambo haya matatu yametambuliwa Katiba Inayopendekezwa na tunaweza kuyawekea mfumo wa kisheria ili yatekelezwe kama Katiba Inayopendekezwa itakuwa imepitishwa. Kama itapitishwa Aprili 30 na Uchaguzi Mkuu ni Oktoba, halafu tukiiweka Katiba hii kabatini (tusiitumie), tutapata shida,” alisema Masaju, ambaye aliisifu Katiba Inayopendekezwa kuwa ina mambo mengi mazuri.
“Ushauri wangu kwa Serikali, kama Katiba imepigiwa kura na watu wakaipitisha, basi tuanze kutekeleza yale yanayowezekana.”
Akizungumzia kipindi cha mpito cha miaka minne ambacho kimewekwa kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa Katiba hiyo alisema si lazima Katiba Inayopendekezwa ianze kutumika baada ya kipindi hicho.
“Huo ni muda tu umewekwa na si lazima ufike. Kuna mambo ya msingi ya kuzingatia. Mfano, Katiba hii imezungumzia masuala ya haki mbalimbali. Haki hizi utekelezaji wake utategemea na bajeti iliyopo. Jambo hili linahitaji muda kidogo. Kuna mambo ambayo hatuwezi kuyafanya kwa sasa, mfano ni hili la haki ya wananchi kupata maji au kuwa na zahanati kwa kuwa linahitaji bajeti kuliandaa,” alisema.
Alisema yale ambayo yanahitaji bajeti kidogo au kutohitaji kabisa, kama suala la kuwapo kwa Tume Huru ya Uchaguzi, yanaweza kuanza kutekelezwa.
“Katiba ikipita kuna mambo tunayoweza kuyafanya hasa yale yanayohusu uchaguzi. Ni mambo ya msingi sana ambayo kama mkiyaacha watu watawashangaa,” alisema.
“Kama watu walitaka mgombea binafsi na leo unakwenda kufanya uchaguzi na Katiba imepitishwa (inatambua mgombea binafsi), halafu huitumii, wengi watakushangaa.”
Hata hivyo, Masaju, ambaye alikuwa mshauri wa rais wa masuala ya katiba na sheria kabla ya kuhamishiwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, alisema kwa maoni yake haoni kama tume iliyopo sasa haiko huru.
Alirejea Ibara ya 74 ya Katiba ambayo alisema inaipa Tume ya Uchaguzi uhuru wa kufanya kazi zake bila ya kuingiliwa na chombo chochote.
“Labda hawa wanataka Katiba iseme composition (watu wanaoiunda). Composition na kutajwa kwenye Katiba hakuna tofauti,” alisema mshauri huyo wa Serikali wa masuala ya sheria na Katiba.
Ukawa ilisusia vikao vya Bunge la Katiba ikidai kuwa lilipoteza mwelekeo kutokana na kuacha kujadili Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na badala yake kujadili mapendekezo ya CCM.
Katika kujaribu kunusuru mchakato huo, Rais Jakaya Kikwete alikutana na vyama vya upinzani chini ya mwamvuli wa Kituo cha Demokrasia (TCD) na ndipo wapinzani walipotoa mapendekezo hayo, moja la mgombea binafsi likiwa limetokana na uamuzi wa Mahakama ya Afrika Mashariki kuhusu kesi iliyofunguliwa na mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila aliyekuwa akitaka haki hiyo itambuliwe.
Hata hivyo, wakati wapinzani wakisubiri mchakato huo kuahirishwa, Bunge la Katiba lilipitisha Katiba Inayopendekezwa na baadaye Rais Kikwete kukabidhiwa. Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Rais Kikwete alitangaza tarehe ya Kura ya Maoni, jambo lililowafanya wapinzani waamue kususia mchakato uliosalia wa kupitisha Katiba Mpya.
Mahakama ya Kadhi
Mwanasheria Mkuu pia alitoa ufafanuzi wa hoja kadhaa ambazo anaona zimekuwa zinawatia hofu wananchi katika suala la kutambua Mahakama ya Kadhi.
“Shetani anaweza kuwa ameingia nchi hii,” alisema Masaju ambaye alitumia muda mwingi kulizungumzia huku akisema si ajenda yake bali amelazimika kufanya hivyo na anashangaa kwa nini viongozi wa Serikali hawajatoa elimu ya kutosha kuhusu Mahakama ya Kadhi.
“Hii kitu mimi naweza kuieleza. Tatizo ni kwamba imechukuliwa na wanasiasa na wagombea urais,” aliongeza.
“Kwanza jambo hili si geni. Mahakama hii nchini ilianzishwa miaka miwili iliyopita. Serikali haianzishi bali inaitambua.”
Akizungumzia hofu hiyo, Masaju alisema suala hilo kwanza linahusishwa na dini ya viongozi waliopo madarakani hivi sasa.
“Wanawahusisha viongozi wakuu wa Serikali kwa sababu ni Waislamu, wapo wanaosema kuwa viongozi hao wanataka kulifanya taifa hili kuwa la Kiislamu,” alisema na kuongeza kuwa hoja hiyo si ya kweli kwa sababu lilishakuwapo tangu enzi za viongozi Wakristo.
Alitaja suala jingine kuwa ni uundwaji wa Mahakama ya Kadhi, ambalo alisema halitaihusu Serikali.
“Wengi walidhani sheria ndiyo itaunda Mahakama ya Kadhi. Hapa linalofanyika ni kutambua tu, mambo mengine watafanya wenyewe Waislamu,” alisema. “Kuna watu walitaka uanzishwaji, mamlaka, sifa za kadhi na maslahi mengine yatajwe kwenye sheria, lakini sisi Serikali tukasema hapana. Haya tuwaachie wenyewe.”
Alisema hofu nyingine ni kuhusu wahusika watakaobanwa na sheria hiyo na kufafanua kuwa hilo litatokana na ridhaa ya watakaotaka Mahakama ya kadhi iwabane.
“Hata Waislamu ambao hawatataka, hawatabanwa na sheria hii. Watakaobanwa ni wale watakaoridhia tu. Ni masuala ya hiari,” alifafanua.
Kuhusu nguvu ya Mahakama ya Kadhi, Masaju alisema hilo lisiwatie hofu watu kwa kuwa masuala ya hiari hayahusishi matumizi ya nguvu na hivyo hakuna mtu atakayelazimishwa kuridhia.
“Watu wanawaza zile sheria kama za kuchinja na nyingine za kutumia nguvu. Masuala yote ya jinai yatabaki mikononi mwa Serikali. Jamhuri ndio inashitaki. Hawa tutawaachia mambo kama ndoa, talaka, wakfu na mirathi lakini kwa watakaoridhia tu,” aliongeza.
“Mambo ya jinai siku zote ni ya serikali na ndiyo maana inayosimama mahakamani ni serikali na mwathirika wa kitendo cha jinai anakuwa shahidi. Kama umepigwa, wewe ndiyo mwathirika wa kile kitendo, lakini mlalamikaji mahakamani ni Serikali, wewe (uliyepigwa) unakuwa shahidi wetu na ukikataa kutoa ushahidi tunakushitaki.”
Hofu nyingine aliyosema inasumbua watu ni fedha za kuendeshea mahakama hiyo baada ya kutambuliwa kisheria.
“Hili halitatuhusu. Waislamu wenyewe ndio watakaoendesha mahakama hizi,” alisema na kuongeza kuwa Waislamu wamekuwa wakiendesha Mahakama ya Kadhi kwa miaka miwili kwa gharama zao.
Muswada wa marekebisho ya sheria ambao ungehusisha kutambuliwa kwa Mahakama ya Kadhi ulitakiwa kuwasilishwa kwenye mkutano uliopita wa Bunge kama ilivyoahidiwa na waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati wa vikao vya Bunge la Katiba, lakini ukaondolewa kwa ajili ya kutoa muda zaidi wa majadiliano.
Kwanini sheria ya Mahakama ya Kadhi
Alisema pamoja na kwamba Serikali haitaingilia uendeshaji wa Mahakama ya Kadhi, inalazimika kuitambua kwa sababu mambo yote ya umma yanaongozwa na kutawaliwa na sheria na isipowekwa sheria watu wanaweza kufanya mambo watakavyo.
“Jambo hili wengi hawajaeleweshwa. Suala hili halipaswi kutufanya tugawanyike. Katika (kujadili) hili, dini zetu tuziweke nyuma na kuweka maslahi ya taifa mbele. Waislamu wasidai makubwa zaidi na wajizuie kutoa matamko, hii ni pamoja na Wakristo,” alisema
Masaju aliwataka Waislamu na Wakristo kuishi kwa upendo kama dini zao zinavyotaka na kusisitiza kuwa Serikali haina dini katika kufanya shughuli zake na kwamba haiongozwi na vitabu vya dini bali itaongozwa na Katiba na Sheria.
Alisema lengo ni kuhakikisha kuwa mambo yanayofanyika katika Mahakama ya Kadhi, kama mume kumpa mkewe nyumba yaweze kutambulika katika mahakama za kawaida.
“Ingekuwa hatari kama Waislamu wangesema lazima Serikali itangaze kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na kuigharamia na kila Mwislamu alazimishwe kwenda katika mahakama hiyo. Suala hili tukilielewa, halina shida maana hata Ibara ya 107 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasisitiza usuluhishi wa migogoro,“ alisema.
Kuhusu kugawanyika kwa Waislamu katika kulitambua Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Masaju alisema hakuna jinsi ya kulikwepa baraza hilo kwa kuwa ni chombo kinachotambuliwa na Serikali kisheria.
“Kwanza kwa mfumo wetu wa sheria, taasisi ile ya Bakwata ndio inayotambulika kabisa kisheria, hivyo endapo wapo wanaoipenda au wasioitaka, hakuna jinsi ya kuikwepa” alisema.
Lakini akasema kuwa katika suala hilo, Waislamu wote waliungana na kuwa na msimamo mmoja.
“Na sisi tunacholenga kama serikali ni kuhakikisha kuwa watu wote katika jamii wanakuwa na amani,” alisema.
Alisema kuwa walikutana na viongozi hao wa Kiislamu Februari 3 na walikiri kuwapo na tofauti, lakini wakasema tofauti walizokuwa nazo wameziondoa na wameungana kutokana na umuhimu wa kuwapo kwa mahakama hiyo.
Mihimili kuingiliana

Akizungumzia tatizo la kuingiliana kwa Bunge, Serikali na Mahakama, Masaju alisema suala hilo ni hatari kwa kuwa linaharibu utaratibu mzima wa utoaji haki.
Masaju, ambaye kwa nafasi yake ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali anakuwa kiungo wa mihimili yote mitatu, alisema Bunge linatunga sheria, Mahakama inatafsiri sheria, na serikali inasimamia utekelezaji wa sheria.
Alisema ibara ya 107 (b) ya Katiba inasema chombo cha juu cha utoaji haki ni mahakama.
“Ndiyo maana tunasema suala likishakuwa mahakamani hatutakiwi tena kujadiliwa nje, na vyombo vya habari vimeruhusiwa kwenda mahakamani kuripoti kile kilichojiri pale siku ile na siyo nje ya pale,” alisema.
Anasema kujadili bungeni mambo yaliyopo mahakamani, kunaharibu kesi. “Kwa mazingira haya hakimu au jaji hawezi kufanya uamuzi ulio huru… sisi mamlaka yetu imewekwa katika Katiba.”
Alisema unapoingilia suala la jinai lililopo mahakamani unakuwa umeingilia uhuru wa mahakama kwa uhuru wake na kwa upande mwingine unakuwa umeingilia serikali maana ndio inayompeleka mtu mahakamani kwa suala la jinai.
“Kwa hiyo ushahidi tutakaokuwa nao sisi utaonekana ni wa uongo… Hakimu au jaji akimuachilia mtu au kumfunga, lazima kutaonekana kumekuwa na shinikizo,” alisema.
Kinga ya wabunge
Akizungumzia kinga ya mbunge, alisema mahakama ina uwezo na mamlaka ya kuhoji uamuzi ya Bunge.
Alisema sheria inasema kila mtu atii Katiba na sheria.
“Huwezi kukaa bungeni ukajiwekea utaratibu wakati ukijua kanuni zinasema usimdhalilishe mbunge mwenzio wala kumtukana,” alisema.
Alisema kuna kanuni inayosema Bunge halitakiwi kujadili jambo lililopo mahakamani, lakini wabunge wanafanya kinyume. Kama ukimtukana mbunge au kumpiga ukiwa ndani ya Bunge, huwezi kujitetea eti nilikuwa natekeleza majukumu ya kibunge. Maana utaulizwa hayo ni majukumu ya kibunge?” alihoji.
Alisema Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge inamruhusu Mwanasheria Mkuu wa Serikali chini ya kifungu cha 12 kumshitaki mbunge kwa kosa la jinai.
“Pia Bunge lenyewe linaweza kuazimia kuwa mbunge fulani kafanya kosa la jinai, kupeleka suala hilo kwa Mwanasheria Mkuu ambaye akiridhika, analipeleka mahakamani na ushahidi wote,” alisema.
CREDIT:DARASAHURU BLOG

No comments: