
Ngeleja (47), ambaye amewahi pia kuwa naibu waziri na Waziri wa Nishati na Madini, alisema hayo wakati akihitimisha utetezi wake baada ya kusomewa malalamiko hayo dhidi yake na wanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma mbele ya baraza hilo, linaloongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Hamisi Msumi, jijini Dar es Salaam jana.
“Naomba baraza lako litoe mwongozo utakaokuwa una unafuu kwangu, sababu sikutenda hili kwa nia mbaya, bali ni kwa utaratibu ambao unatumika Tanzania. Mimi ni Mtanzania, mzalendo, mwaminifu kama walivyo wengine,” alisema Ngeleja kwa upole na kwa unyenyekevu wa hali ya juu akiwa amesimama ‘kizimbani’ mbele ya baraza hilo jana.
Aliongeza: “Baraza lako litoe mwongozo. Rungu la mwongozo wako lisianzie kwangu, sababu imethibitika wabunge wengine wamehusika…sikuwahi kupotoka kwenda kinyume cha maadili ya utumishi. Baraza lako litafakari kabla ya kutoa maamuzi.”
Ngeleja alifikia kutamka hayo baada ya Mwanasheria wa Baraza hilo, Getrude Cyriacus, kuhitimisha hoja za malalamiko hayo akiliomba baraza lione umuhimu wa kupendekeza kwa mamlaka husika adhabu kali dhidi ya Ngeleja ili liwe fundisho kwa watumishi wengine wa umma.
Ngeleja alikiri kupokea fedha hizo kutoka kwa Rugemalira, lakini alisema hazikutolewa kwake kama fadhila za kiuchumi kama malalamiko yaliyowasilishwa dhidi yake katika baraza hilo jana yanavyoeleza.
Alidai fedha hizo aliomba na kupewa zikiwa ni msaada, ambao hautofautiani na misaada inayopokelewa na wabunge wengine, ambayo hubarikiwa na Bunge.
Ngeleja alidai mmoja wa wabunge walionufaika na misaada ya fedha za wafadhili, ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ambaye kisheria ni mtumishi wa umma.
Alidai Zitto alinufaika na msaada wa zaidi ya Sh. milioni 30 na dola za Marekani 5,000 kutoka kwa Kampuni ya Pan Africa Power (PAP) na Independent Power Tanzania Limited (IPTL) alizopata kwa matumizi yake binafsi.
Ngeleja alidai misaada mingine, ambayo Zitto amewahi kuipata ni pamoja na unaohusu Sh. milioni 119.9 na Sh. milioni 79, ambayo alidai kuwa aliipata kutoka Shirika la Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Alidai suala hilo kuhusu Zitto liliwahi kuelezwa na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde na Mbunge wa Kishapu, Seleman Nchambi wa CCM kwa nyakati katika mikutano ya 16 na 17, bungeni, mwishoni mwa Novemba, mwaka jana.
Hata hivyo, alidai pamoja na tuhuma hizo na vielelezo kuwasilishwa bungeni, Bunge halikumchukulia hatua zozote Zitto.
Kutokana na hali hiyo, aliliomba baraza hilo kutoa mwongozo kuhusu misaada inayoombwa na viongozi wa umma, wakiwamo wabunge ili kuepuka migogoro kama inayojitokeza kwa sasa na ikiwezekana lipeleke mwongozo bungeni ili sheria ibadilishwe.
Alidai wabunge wamekuwa wakiomba misaada kutoka kwa wafadhili ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ndani ya majimbo yao ya uchaguzi.
Ngeleja alidai misaada hiyo imekuwa ikitolewa na wafadhili mbalimbali, kama vile Mwenyekiti wa IPP, Dk. Reginald Mengi na Said Salim Bakhressa, mifuko ya kijamii, kama vile NSSF na mabenki.
Alidai misaada, ambayo wamekuwa wakiiomba kutoka kwa wadau, ni kwa ajili ya kutekeleza ahadi zinazotolewa na wabunge kupitia harambee zinazofanyika makanisani na misikitini, ambayo haikutengewa fedha kwenye bajeti ya serikali kwa ajili ya kusaidia maendeleo jimboni.
Ngeleja alitoa utetezi wake sambamba na kuwasilisha nyaraka mbalimbali kama vielelezo, ikiwamo taarifa rasmi ya Bunge (ansard), stakabadhi za malipo ya kodi ya Sh. milioni 13.1 ya fedha alizopewa na Rugemalira, ambazo alidai kuwa amelipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Nyaraka nyingine alizowasilisha kama kielelezo mbele ya baraza ni stakabadhi za michango aliyoitoa kwa baadhi ya watu, kikiwamo kikundi cha wana kwaya vijana wa Chang’ombe cha Kanisa la Inland Tanzania, lililoko jijini Dar es Salaam zikiwa ni msaada kwao kupitia fedha alizopewa na Rugemalira.
Pia alidai namba ya akaunti ya tawi la Benki ya Mkombozi iliyotumika kupitishia fedha alizopewa na Rugemalira iliyotajwa kwenye hati ya malalamiko siyo yake kwa kuwa yake haiishii na namba 01.
Alidai akiwa mbunge ameshiriki kutoa misaada jimboni mwake inayofikia Sh. milioni 84, hivyo akaliomba baraza kuzingatia utetezi wake.
Alikanusha malalamiko ya kutumia wadhifa wake kama waziri na mbunge kujipatia manufaa, kwani Februari 24, mwaka jana aliwasilisha tamko kwa Kamishna wa Maadili kueleza msaada wa Sh milioni 40 alizopokea kutoka kwa Rugemalira.
Hata hivyo, Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Getrude, akimhoji alimtaka Ngeleja kulieleza baraza kama alikwenda jana kujitetea au kulilalamikia Bunge.
Alijibu kuwa hakwenda kulalamika, bali kujitetea dhidi ya hati ya malalamiko iliyowasilishwa kwenye baraza dhidi yake.
Getrude alimhoji kama alifungua akaunti hiyo Februari 7, mwaka jana katika tawi la benki hiyo na kama jina lililomo kwenye taarifa ya akaunti yake benki limekosewa au la na kujibu halijakosewa.
Pia alimhoji kama Sh. 40,425,000 ziliingizwa kwenye akaunti yake na kwamba, baada ya hapo alichukua Sh. milioni 14, baadaye Sh. milioni tisa, Februari 18 Sh milioni 17 na Desemba 31 Sh milioni 3.3 na kujibiwa na Ngeleja kuwa ni kweli.
Vilevile, Mwanasheria mwingine wa Sekretarieti hiyo, Hassan Mayunga, aliliambia baraza kuwa sheria ya mfuko wa jimbo inataka fedha zake zihifadhiwe kwenye akaunti ya mfuko huo na Ngeleja alipohojiwa na mwanasheria huyo, alikiri fedha alizopokea kutoka kwa Rugemalira ziliingia kwenye akaunti yake binafsi.
Pia aliliambia baraza kuwa kama Ngeleja fedha alizoomba zilikuwa kwa ajili ya jimbo lake kwa nini alizitoa kwa nyakati tofauti na nyingine akapeleka katika kanisa lililopo Dar es Salaam wakati siyo sehemu ya jimbo lake na wala kamati ya maendeleo ya jimbo lake haikuwa na taarifa.
Pia Ngeleja alidai fedha hizo hazikuwa ni za mfuko wa jimbo.
Vilevile, Ngeleja alikataa kuwa yeye siyo mhasibu wa kamati ya maendeleo ya jimbo alipotakiwa na mwanasheria huyo kueleza kama yeye ni mhasibu wa kamati hiyo.
Pia mwanasheria huyo alilieleza baraza kuwa kanisa, ambalo Ngeleja alidai kulipa msaada kutoka fedha hizo, lipo Dar es Salaam, ambako siyo sehemu ya jimbo lake.
Mwanasheria huyo pia aliliambia baraza kuwa tamko kwa Kamishna wa Maadili, lilitolewa na Ngeleja wakati kwenye akaunti yake kukiwa kumebaki Sh milioni tatu kati ya Sh. milioni 40 alizopokea kutoka kwa Rugemalira.
Ngeleja analalamikiwa na sekretarieti hiyo kukiuka sheria ya maadili ya viongozi wa umma kwa kuomba fadhila za kiuchumi kutoka kwa Rugemalira.
Anadaiwa kuwa Februari 12, mwaka jana alipokea Sh 40,425,000 kutoka VIP Engineering and Marketing Limited iliyokuwa inamiliki asilimia 30 ya hisa katika kampuni ya IPTL na pia ilikuwa na mkataba na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wa kuongeza uzalishaji wa umeme nchini.
Fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti yake iliyopo tawi la Benki ya Mkombozi na kwamba, hakutamka kuzipokea.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa mahojiano, Ngeleja alisema ni mara ya kwanza kupata fursa ya kujitetea tangu sakata hilo lianze mwishoni mwa mwaka jana, huku akiitupia lawama Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kutoa nafasi ya kujieleza kwa watu waliotuhumiwa badala yake ikawahukumu moja kwa moja:
Wakati huo huo; Mkurugenzi wa Huduma za Sheria katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma, ameweka pingamizi kuzuia shauri lake lisisikilizwe na baraza hilo hadi kesi yake ya jinai kuhusu sakata la akaunti ya Tegeta Escrow iliyopo Mahakama ya Kisutu iishe.
Mujunangoma anadaiwa kuwa akiwa na wadhifa huo, alikuwa ni mshauri mwelekezi wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing LTD na Mabibo Wines and Spirits ambao ulimpatia manufaa ya kifedha ya jumla ya Sh. milioni 423.4 ninyume cha sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji Msumi alisema baraza litatafakari hoja zilizotolewa na pande mbili za shauri hilo na kuzitolea uamuzi, ambao litaupeleka kwa mamlaka husika kama sheria inavyoeleza.
Upande wa walalamikaji (Sekeretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma) ilipeleka shahidi mmoja, Waziri Mpacha (43), ambaye ni Katibu Idara ya Uchunguzi wa Sekretarieti hiyo, ambaye alimhoji Ngeleja.
CHANZO: NIPASHE
2 comments:
Wabunge wengine wanachukuwa; Zito amechukuwa; yeye ni mwaminifu na mzalendo!!! Please! This would be a huge joke if it weren't true. What a pity? Inaonyesha jinsi viongozi wetu wasivyoelewa maana ya maadili!! Hivi mpaka watu waingie mitaani. Tume haina budi kuchukuwa hatua Kali kwa kila mtu bila kujali vyeo vyao.
It is time to act. We may come to regret these serious indiscretions - no criminal acts - as a nation.
wameshikwa pabaya maccm wana haha na jamaa aliyewapa mipesa alijua tamaa zao na kuwambia wafunguwe tu benki mkombozi na stanbic so aliwanasa vizuri alishawajua wanapenda pesa.
watatafunana wenyewe kwa wenyewe waliowatega wanachekela na kula nyama zao choma poa.
chezea uraisi wewe kila mtu anautaka mkiwazibia wasiupata wanakukamateni pabaya kila mwananchi anakuoneni hamufaai.
yani nawapa big up walio chonga mchongo huu wakuwapa mipesa hawa mifisadi ya ccm na yeye anajisafishia njia nyeupe ya kupata uraisi.
Post a Comment