ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 25, 2015

Nyumba zilizojengwa juu ya bomba la kupitisha maji Buruguni kuvunjwa.


Rais Jakaya Kikwete, jana alitembelea waathirika wa mafuriko Buguruni kwa Mnyamani na kuahidi kuwasaidia, huku akiagiza kuvunjwa kwa nyumba zitakazobainika kujengwa juu ya bomba hilo.

Kikwete alisema tathmini ya nyumba ziliozojengwa juu ya bomba hilo itafanyika, na wanaanchi watalipwa fidia zao.

Kadhalika, alisema bomba hilo lililosababisha mafuriko hayo litajengwa upya ili kuwezesha kupitisha maji mengi zaidi.

Kikwete pia ameagiza wilaya ya Ilala itoe msaada wa chakula kwa wakazi hao, pamoja na misaada mingine ya kibinadamu.

“Tatizo hili linashughulikiwa na litamalizika,” alisema na kuongeza: “Tatizo lililosababisha haya yote ni kuziba kwa bomba lililokuwa likipitisha maji ambalo limekutwa lina vyuma, vinu, mawe na mchanga, kwa hiyo maji yote yaliyotakiwa kupita yameshindwa kupita na kurudi kwenye makazi ya watu.

Nyumba zote zitakazobainika kujengwa juu ya bomba itabidi zipishe, zitavunjwa na serikali itawalipa fidia, ila tunaomba mkiondoka msirudi tena.”

Alisema serikali itazungumza na wahandisi ili kuhakikisha bomba hilo linajengwa katika viwango ambavyo havitasababisha tatizo jingine kama hilo huku akiwatahadharisha wakazi wa eneo hilo kuepuka kuharibu miuondombinu na kusababisisha kutokea kwa matatizo mengine ama hayo.

“Haya yatakwisha, lakini ninawaomba msije mkafanya tena kama haya, ninaomba bomba litakalojengwa msiliharibu tena, mkasababisha kutokea matatizo mengine kama haya, na wale mtakaolipwa fidia msirudi tena hapa,” alisisitiza Kikwete.
CHANZO: NIPASHE

No comments: