NAIBU Waziri wa Fedha na Uchumi, Mwigulu Nchemba.
NAIBU Waziri wa Fedha na Uchumi, Mwigulu Nchemba, anatajwa kutaka kuvaa viatu vya urais, amrithi Jakaya Kikwete; awe kiongozi wa taifa wa awamu ya tano.
Kumkatalia au kumkubali kunahitaji hoja na siyo maneno. Kwa kuwa Mwigulu anajipitishapitisha kuwania nafasi hiyo ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), chama hicho kina vigezo ambavyo lazima avikidhi.
Moja ya vigezo hivyo ni kiwango cha elimu. Waziri Nchemba aliyezaliwa Januari 7, 1975, hana shaka katika hilo, ni msomi wa masuala ya uchumi. Amehitimu shahada mbili za uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na sasa yu mbioni kujinyakulia Shahada ya Uzamivu (PhD) katika fani hiyo muhimu katika maendeleo ya nchi.
Mwigulu ambaye kwa kabila ni Mnyiramba kutoka Mkoa wa Singida, ‘anatekenywatekenywa kisiasa’ kuwa, jina analotumia si lake. Wanaomfuatafuata kwenye mitandao ya kijamii wanasema kabila lake halina jina la Mwigulu Nchemba abadan na kwamba yeye kwa asili ni Lameck Mkumbo Madelu, mzaliwa wa Makunda Kata ya Kyangege, Tarafa ya Kinampanda, Wilaya ya Iramba.
Wanaojidai kumjua wanasema, jina la Mwigulu Nchemba ni la kabila la Wasukuma lenye maana ya MWIGULU (Mbinguni), NCHEMBA (Mkataji), analodaiwa kulipata katika harakati zake za kurudia Darasa la Saba ambapo anadaiwa kuchukua jina la mwanafunzi wa Kisukuma aliyeacha shule kwa sababu ya mwamko mdogo wa elimu.
Hayo ni ya walimwengu ambayo mtuhumiwa mwenyewe hajawahi kuyatolea ufafanuzi na hivyo kubaki kuwa ‘tipu’ ya kufuatilia katika Shule ya Msingi Makunda, Sekondari ya Ilboru (Arusha) na Mazengo (Dodoma).
MAISHA YA KISIASA YA MWIGULU
Mbali na kuajiriwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kati ya mwaka 2006 hadi 2010, kama afisa wa sera na uchumi maisha ya kisiasa ya Mwigulu yalianza 2001, alipochaguliwa kuwa mjumbe wa vijana wa Wilaya ya Iramba, 2008 akawa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) na mwaka huohuo akachaguliwa kuwa mjumbe wa Mkutano Mkuu kupitia Umoja wa Vijana (UVCCM).
Hata hivyo, vyeo hivyo havikumkoleza zaidi kisiasa mpaka pale mwaka 2010, alipojitosa rasmi kuwania Jimbo la Iramba Magharibi na kushinda kuwa mbunge. Hapo ndipo umahiri wake kisiasa ulipoanza kuonekana tangu kwenye kampeni mpaka alipoingia bungeni kwa mara ya kwanza. Alionesha kuwa anajua kuichanga karata ya siasa ipasavyo.
Mara kadhaa chama chake kilimtumia katika kampeni za marudio ya uchaguzi, mfano kule Igunga ambako mchuano ulikuwa mkali kati ya mgombea wa CCM na wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Hii ilikuwa na maana kwamba, CCM walimuona ni jembe. Hata alipoingia bungeni hoja zake zilikuwa mwiba kwa wapinzani huku mara kadhaa akitumia maneno ya ‘kuudhi’ kama: “Waongoza disko kupanga bajeti ya kambi rasmi ya upinzani bungeni,” akimaanisha Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye historia inaonesha kuwa alikuwa DJ wa muziki kabla ya kuwa mwanasiasa.
Mwaka 2012, Mwigulu aliwahi kukitupa kitabu cha hotuba ya bajeti ya kambi ya upinzani kwa kukifananisha na takataka. Mwaka 2013, akiwa bungeni kwa mara nyingine naibu huyo waziri aliwahi kukituhumu Chadema kuwa kinapanga vurugu na mauaji.
Akiwa kwenye vikao vya Bunge la Katiba mwaka jana, Mwigulu aliwataja Mbowe na Ismail Jussa (wajumbe bunge la katiba) kuwa ni watu wanaotaka kuleta ushoga na udini nchini na hivyo kuwataka wananchi kuwapuuza.
Hata Chadema nao kwa upande wake wamewahi kumtuhumu kuwa ni kinara wa siasa chafu, wakimhusisha na upangaji njama za kumrekodi Mkurugenzi wa Ulinzi wa Chadema, Wilfred Lwakatare, akionekana kupanga njama za kuwadhuru waandishi pamoja na lile tukio la kumwagiwa tindikali kwa kada wa CCM kwenye uchaguzi mdogo wa Igunga mwaka 2011.
Akiwa ndani ya tuhuma za kutumikia siasa chafu, nyota ya Mwigulu ndani ya chama chake ilizidi kung’aa. Akiwa mbunge, alifanikiwa kuukwaa ukatibu wa fedha wa chama chake na baadaye jicho la rais likamuona na kumpa cheo cha unaibu waziri wa fedha.
MWIGULU NA NDOTO YA URAIS
Akiwa wizarani akawathibitishia watu kuwa ni hodari na mtetezi wa wanyonge. Hakusubiri kauli ya waziri wake wa fedha katika kushughulikia kero na madudu ya wizara yake; akawa naibu waziri wa: “Naagiza.”
Akajipatia umaarufu mkubwa katika kushughulikia mianya ya mishahara hewa, ulipaji wa malimbikizo ya malipo ya waalimu na uzembe wa watumishi wa wizara yake. Mara kadhaa amesikika akiwakemea watumishi wazembe wa wizara yake kwa kuwaambia wale wasiotaka kuendana na kasi yake ni bora watafute kazi za kufanya.
Wananchi, wafanyakazi serikalini, waalimu, waseme nini tena zaidi ya: “Kiongozi si huyu jamani!” Funga kazi ikawa pale lilipoibuka sakata la akaunti maarufu ya Tegeta Escrow; mapema alianza kuwabana viongozi wenzake serikalini na ndani ya chama chake kuwa wanapaswa kushughulikiwa ipasavyo.
Alifanya hivyo huku akiwaacha baadhi ya wabunge kutoka chama chake wakitafuta njia ya kuwanasua watuhumiwa wasiaibike na chama kunyooshewa vidole. Huu ukawa ni mtaji mkubwa kwa Mwigulu.
Tangu hapo akaanza kuonja raha ya vigelegele vya wananchi kila alipopita. Nadhani hapo ndipo ndoto ya kuwa rais ilipomtokea na kuamua kuanza kujipitishapitisha. Lakini Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, hakupendezwa na tabia hiyo akamfunga ‘gavana’ na kumwambia aache kujinadi mapema; naye bila kinyongo akaufyata.
KIATU CHA URAIS KINAMWENEA, KINAMPWAYA?
Mwigulu ananadika. Hana skendo za wazi, hii inatokana pengine na kuwepo kwenye siasa ngazi za juu kwa muda mfupi, kimtazamo anakidhi kwa asilimia 80 kuvaa viatu vya urais na hasa sifa za mgombea anayehitajika na chama chake zikizingatiwa. Ameonesha dalili kuwa ni kiongozi anayeweza kusimamia uamuzi mgumu.
Lakini huo hauwezi kuwa ushindi wake wa jumla kwa sababu siasa zimebadilika mno nyakati hizi; zama za CCM kushinda hata kwa kuweka jiwe zimemalizika kitambo. Hivyo viatu vinaweza kumpwaya ikiwa hana mtaji wa kutosha wa wapigakura.
Rais anayemaliza muda wake Jakaya Kikwete ni shahidi, asilimia 81 zilizompa ushindi 2005, sizo zilizomrudisha ikulu 2010.
Alishuka kwa asilimia 20, vijana wa mjini wanasema chupuchupu kuangushwa.
Kwa msingi huo kufaa kwa Mwigulu kunaweza kusitokane na kukubalika na chama chake pekee bali wananchi kwa ujumla ambao wengi wao hawajamfahamu vya kutosha ukilinganisha na wagombea wengine ndani na nje ya chama chake ambao wametumia muda mwingi kujijenga binafsi tofauti na yeye aliyeanza kazi hiyo juzi tu.
CREDIT:GPL
No comments:
Post a Comment