Mkazi wa mjini Moshi akipita katikati eneo la Kariakoo mji humo huku maduka yaki yamefungwa baada ya jumuiya ya wafanya biashara Mkoa wa Kilimanjaro kuwamasishana kuyafunga wakipinga kutumia mashine za EFD na kupandishwa kwa kodi ya mapato, mkoani humo jana. Picha na Dionis Nyato
Wauzaji na wamiliki wa maduka maeneo ya Mwanjelwa, Uhindini na Sido mkoani Mbeya jana waliwalaumu viongozi wao kwa kuwashinikiza kuyafunga maduka bila kutoa sababu za msingi na kuwasababishia hasara.
Wamesema tabia ya kufunga maduka inawaathiri wao na wateja badala ya Serikali inayolaumiwa.
Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao, wafanyabiashara hao walisema, viongozi wao wanawalazimisha kuyafunga maduka na kwamba atakayefungua atalipishwa Sh50,000.
“Kwa kweli nilifunga duka baada ya kushinikizwa na viongozi walionitishia kwamba watachoma moto duka nikifungua au kulipa Sh50,000,” alisema mfanyabiashara wa vifaa vya umeme.
Naye muuzaji wa bidhaa za jumla eneo la Sido, alisema tabia ya viongozi wao kuwalazimisha kufunga maduka bila maelezo ya kina inawayumbisha kiuchumi kwa vile, wateja wengi wanakosa kuchukua bidhaa zao.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Syonga Syonga hakupatikana kuelezea sababu za kulazimisha kufunga maduka hayo, lakini mjumbe wa kamati ya uongozi, aliyejitambulisha kwa jina la Amina Kyaro alisema, walifunga maduka ili kumuunga mkono Mwenyekiti wa Wafanyabiashara nchini, Johnson Minja ambaye jana alifikishwa mahakamani Dodoma.
Mkoani Mwanza, jana wananchi walikosa huduma baada ya wafanyabiashara kufunga maduka yao kwa kile wanachodai ni hatua ya kumsindikiza Minja aliyefikishwa mahakamani mjini Dodoma kujibu mashtaka yanayomkabili.
Maduka mengi katikati ya jiji la Mwanza jana yalionekana kufungwa, huku baadhi ya wafanyabiashara wakiwa wamesimama nje na wateja wakihangaika kutafuta huduma.
Wakizungumza baadhi ya wafanyabiashara waliokutwa nje ya maduka yao, walisema wamefunga maduka yao ikiwa njia ya kumsindikiza mwenyekiti wao mahakamani kusikiliza kesi inayomkabili.
Mkazi wa Nyakato, Mwanza, Rashid Mustafa alilaumu kitendo hicho na kusema hawakuwa na sababu ya kufunga maduka, tena bila kutoa taarifa kwa wateja, huku wakisababisha wananchi kukosa huduma za msingi kwani kufanya hivyo ni kuwanyanyasa kwa kuwanyima huduma.
Mkoani Kilimanjaro, pia wafanyabiashara walifunga maduka ili kuishinikiza Serikali kurekebisha mfumo wa mashine za Kieletroniki (EFD) pamoja na tozo la kodi la asilimia 100.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kuhusu tatizo hilo la mashine, baadhi ya wafanyabiashara, Grace Meela na Mbero Malya walisema kuwa mashine hizo zimekuwa zikifanya makadirio ya mauzo pekee badala ya faida, hali ambayo imekuwa ikimaliza mtaji.
“Sisi tunachotaka hizo mashine zirekebishwe na tupewe bure tusiuziwe kwa kuwa hizo mashine zimekuwa zikijumlisha mauzo badala ya faida,” alisema Malya.
Walisema kilio kikubwa cha wafanyabiashara ni Serikali kurekebisha mashine hizo ikiwa ni pamoja na kuondoa tozo ya asilimia 100.
Imeandikwa na Lauden Mwambona, Jesse Mikofu na Fina Lyimo wa Mwananchi
No comments:
Post a Comment