ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 4, 2015

WATANZANIA TEKNOLOJIA INATUPELEKA WAPI?

KWENU Watanzania wenzangu popote pale mlipo. Bila shaka kila mmoja wetu anaendelea na majukumu yake ya kila siku kuhakikisha mkono unaenda kinywani.

Binafsi mimi ni mzima wa afya. Naendelea na majukumu ya kila siku likiwemo hili la kuwaandikia barua.
Madhumuni ya kuwakumbuka Watanzania wenzangu leo ni kuhusu maendeleo ya teknolojia hususan suala zima la mitandao ya kijamii na simu hizi za kisasa.

Ndugu zangu, nimelazimika kuwakumbusha suala hili sababu hali sasa imekuwa mbaya. Busara haipo, utamaduni na maadili ya Mtanzania yanazidi kuporomoka, hakuna staha tena ya kibinadamu.Tumefika hatua sasa, mtu anaona tukio ambalo kwa kawaida linapaswa kustiriwa lakini yeye anaamua kuliposti katika mitandao ya kijamii, anawatumia rafiki zake kupitia simu ya mkononi.


Mtu anaona tukio liwe ni la ajali, watu wamefariki kwa kuharibika vibaya miili yao, pasipo kutumia busara anaziposti picha hizo katika mitandao ya kijamii sambamba na kuwatumia marafiki zake, jamani hivi kweli huu ni uungwana?

Nazungumza hivi sababu juzi tumeona kwenye tukio la kifo cha Mbunge wa Mbinga Magharibi (CCM), John Damiano Komba. Sekunde kadhaa tu baada ya kifo chake, picha ya mwili wake ilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Mbaya zaidi picha hiyo haikuwa na staha hata kidogo. Chukulia kama yule angekuwa ni baba yako, ungeweza kuisambaza picha ya namna hiyo? Kama huwezi kwa nini uisambaze ya mzazi wa mwenzako? Hii siyo sawa.

Kinachonisikitisha zaidi, mbali na kuweka picha hizo ambazo si za kistaarabu, bado wengine wamekuwa wakisindikiza na maneno ya kejeli. Tunamkejeli marehemu kweli? Tuna uhakika kwamba sisi ni wasafi? Tuna uhakika wa kuishi milele? Tubadilike.

Ni wakati sasa wa watu kubadilika. Kuheshimu staha ya ubinadamu, desturi zetu zinatufundisha kutokejeli maiti, basi tusifanye hivyo hata kama mhusika ana mapungufu yake, tusihukumu maana kazi hiyo si yetu bali ni ya Mwenyezi Mungu.

Umeona tukio, toa taarifa kwa wenzako na si kuweka picha ambazo hazina staha. Katika hili, serikali kupitia Wizara ya Sayansi na Teknolojia, ianze kudhibiti vitendo hivi kwani naamini inawezekana, kwani mifano ipo mingi tu, kuna nchi nyingi duniani wamefanikiwa kudhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii.

Mtu huwezi tu kukurupuka na kuposti picha mbaya na serikali ikakuachia. Inakusaka na kukutia hatiani. Baadhi ya vyombo vya habari (siyo Global Publishers Ltd) pia vimekuwa vikifanya makosa ya aina hiyo, vibadilike.

Siku zote tusimamie weledi wa habari. Kamwe tusichapishe picha za watu ambao hazina staha au hazipendezi kuonwa hadharani.Ni matumaini yangu mwenye masikio amesikia, tubadilike. Tuongozwe na busara katika maisha yetu.
GPL

6 comments:

Anonymous said...

Duh!! Nilidhani ni mimi mwenyewe nililiangalia hili kwa jicho la tofauti. Watanzania tunaiga mpaka tunapitiliza. Tunahitaji rehema ya Mungu ipate kutusaidia katika hili. Huwaga najiuliza kwani ikiwa na ndugu yako wa damu unaweza kulifanya jambo kama hilo kweli. Tufike mahali tuwe tunajiweka kwenye miguu ya wahusika. Asante kwa kushare hili!

Anonymous said...

Sijafahamu kinacholalamikiwa hapa!!! Ni kuonyesha picha ya marehemu wakati alishaaga dunia au vipi? Mbona ni jambo la kawaida kuagaa maiti zinaanikwa hadharani kwa vifijo na sherehe kubwa? Hivi tukitoa heshima za mwisho si huwa tunawaanika maiti wetu na picha zinapigwa. Au kosa hapa kuwa picha ile alikuwa tumbo wazi hajavishwa suti????
Nadhani hili kwa maiti wa kikristo si la kulalamikiwa wala kufanywa zogo labda kidogo angekuwa maiti wa kiislam ndio kidogo ingekuwa issue, kwa vile maiti wa kiislam hufunikwa mara baada ya kufariki hadi kuzikwa kwake.

Anonymous said...

Umesema ukweli mtupu. Nakupongeza kwa hilo. Hili jambo limenikera siku nyingi. Picha za maiti huwa zinatumwa kabla ndugu wa marehemu hata hawajajua kuhusu misiba.

Anonymous said...

Sad. Sad indeed. Mtu hana Huruma wala haya. Mstaarabu anakuwa na Subira kwanza kwa kujua wapo ndugu na picha kama hizo kwao ni machungu makubwa. Ahsante kulisemea.

Anonymous said...

muandishi wa makala hii kweli umesama kweli na umekanya vizuri na tuwe wastaabru maiti habuliwi wala kukashifiwa tumpe staha hata kama ana mapungufu yake nakubaliana na wewe mia kwa mia.

lakini upande wa pili si tuko katika karne ya digital age,karne ya 21 kila mtu mafacebook,matwitter,mawhatsapp,bbm,tuna simu bai mbaya tunajirusha tutakavyo tunajifanya wa mujini sana hasa hasa tukiwa majuu na ukijifanya unamcha mungu sana au huna mambo ya mitandaoni na huna ma facebook etc unaonekana mjinga,mshamba huna maendeleo wanakusema kila kukicha na kukuona wa ajabu sana.

na kama huna deal za mujini na kuiba unaoneka ni mjinga sana umepata nafasi ya kuiba,kutesa mtu kumtambia mtu kama hujafanya hivyo ni mjinga mjinga sana tena wewe si MUTOTOO WA MUJINIII.

so kwa wengi waliyo hivyo unadhani ukiwakanya watakanyika hata wakiwekewa sheria unadhani watafuata, sheria ngapi ulimwengu mzima zimewekwa na watu bado wana vunja.

mtu asipo muogopa muumba wake,mungu wake na kufanya anayoyataka na kumuabudu ipasavyoo,hana moyo wa uogo wa mungu wake basi ujuye chochote kilicho juu au chini ya juwa atakifanya tuu bila ya aibu yeyote ile na kwake ataona sawa tu.

kwa sababu na uogo wa mungu wake na hamuamini ipasovyoo.

mungu wangu wee tustiri waja wako sisi na tusamehe.ameeen.

shukran mwandishi wa makala hii.mungu akubariki daima na uwe na moyo huu huu daima amen ameen.

Anonymous said...

na mimi ni kama huyo mwaandishi wa pili, tatizo liwekwe wazi. (1) Ni kuonyeshwa picha ya marehemu (2) Ni kurusha picha kwenye mitandao ya kijamii (3) na sasa nimeona jipya limesemwa au ni kurusha picha ya marehemu kabla ya jamaa zake hawajapea taarifa ya msiba???
Mimi sioni lalamiko lolote hapo labda kwa kuwa ni bosi Fulani aliefariki lakini kwa picha za marehemu mbona zinaonyeshwa nyingi tu??????????