Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
Dar/Kigoma. Siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza kumvua uanachama, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kesho atatua jimboni kwake kuzungumza na wananchi kupitia mikutano ya hadhara.
Uamuzi wa kumfukuza Zitto (pichani) ulifikiwa juzi ikiwa ni muda mfupi baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali kesi aliyofungua Januari 2, 2014, dhidi ya Bodi ya Wadhamini na katibu mkuu wa Chadema, iliyokuwa imeshikilia uanachama wake.
Mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ndiye alitangaza kutimuliwa kwa Zitto akisema ni kutokana na kufungua kesi mahakamani, kinyume na Katiba ya Chadema kipengele cha 8 (a) (x).
Jana, Zitto ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) aliongoza kikao cha kamati hiyo, kilichojadili taarifa ya Tanesco na baadaye alisisitiza kwamba hana taarifa rasmi ya uamuzi wa mahakama na atakapoipata atazungumzia hatima yake.
“Kama mnavyoona mimi naendelea na kazi na wala sina taarifa rasmi lakini nikipata taarifa rasmi na mimi nitatoa taarifa rasmi, Ijumaa (kesho) ninakwenda jimboni kuzungumza na wapigakura wangu ambao niliwaahidi kufanya hivyo kabla ya vikao vya Bunge kuanza Jumanne ijayo,” alisema Zitto ambaye taarifa zinasema alikuwa amepapanga kuwaaga wapiga kura na baadaye kutimkia kwenye chama kipya cha ACT alichokiasisi.
“Muhimu kwangu ni kufanya kazi ya Watanzania na nitafanya kwa mazingira yoyote yale. Siasa yangu inajikita katika masuala, siyo watu, ukiandika kuhusu Zitto siyo kwa ajili ya mtu bali masilahi ya Taifa.
“Nakuzwa, nakomazwa na hii ni changamoto, nitaendelea kufanya kazi zangu hadi nitakapopata taarifa rasmi.”
Mwanasheria wa Zitto, Albert Msando juzi aliliambia gazeti hili kwamba, anafuatilia uamuzi huo wa mahakama kabla ya kuona ni hatua gani watazichukua.
ACT wachekelea
Baadhi ya wanachama na viongozi wa Chama cha ACT mkoani Kigoma wamedai kufurahishwa na uamuzi huo, wakidai kuwa utakinufaisha chama hicho.
Mkazi wa Mwandiga, Dunia Pemba alisema Zitto alipaswa kujiondoa ndani ya Chadema pale tu alipovuliwa nyadhifa zake ili atazame sehemu nyingine yenye demokrasia pana kwa vile chama hicho kilionyesha hakimhitaji tena.
“Sisi tulitangulia huku ACT na sasa tunamsubiri kwa hamu, aje kujenga chama hiki ambacho ni tishio kubwa hapa nchini na bila shaka kitachukua viti vingi vya ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, ndiyo maana kutimuliwa kwa Zitto Kabwe ni faraja kwetu kwa sababu atapata muda wa kutosha kujenga chama,” alisema Pemba.
Pia, mwenyekiti wa vijana wa ACT Tawi la Mwandiga, Stili Chuma alisema anafurahia uamuzi ya Chadema ingawa kitendo cha jimbo lake kukosa mwakilishi kinasikitisha.
Katibu Mwenezi wa Chadema Jimbo la Kigoma Kaskazini, Shaban Kasugulu alipongeza uamuzi wa Mahakama Kuu akidai haki imetendeka kwa vile suala la Zitto na Chadema lilichukua muda mrefu na kusababisha watu kukosa mwelekeo.
Hata hivyo, Boaz Chuma aliitupia lawama Mahakama Kuu kwa kuibeba Chadema katika shtaka hilo kutokana na kutoa hukumu siku ambayo haikupangwa.
Dk Makulilo
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Alexander Makulilo alisema kufutwa uanachama kwa Zitto ni fundisho kwa wananchi ambao licha ya kuchagua mbunge wanayempenda, lakini anaweza kuondolewa na vyama vyao.
“Wananchi wanamchagua mbunge wao kupitia chama cha siasa lakini hawawezi kumwajibisha hadi baada ya miaka mitano,” alisema na kuongeza kuwa ni chama pekee kinachoweza kumwajibisha.
Dk Makulilo alisema katika rasimu ya Katiba iliyokuwa ikipendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kulikuwa na kipengele kilichotaka wananchi wawe na uwezo wa kuwajibisha wabunge wao, lakini kikaondolewa na Bunge Maalumu la Katiba.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Dk Emmanuel Mallya kuondolewa kwa Zitto ni taratibu na kanuni za chama kilichompitisha kugombea nafasi hiyo na hapo ndipo unaona umuhimu wa kuwapo mgombea binafsi ili wananchi wawe na nguvu zaidi,” alisema Mallya.
Mbunge wa Mbarali, Modesti Kilufi alisema bado wanaamini Zitto ni mbunge, bado ni mwenyekiti wangu na anaweza kukata rufaa.
Imeandikwa na Ibrahim Yamola, Anthony Kayanda na Raymond Kaminyoge wa Mwananchi
No comments:
Post a Comment