Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Agnes Kijazi anasikitika
kutangaza kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu mstaafu Dkt. Mohamed Mhita (pichani) aliyezaliwa
tarehe 17 Februari 1946 na kufariki siku ya Jumatatu tarehe 06 Aprili 2015 katika hospitali
ya Agakhan jijini Dar es Salaam.
Dkt.
Mhita alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa iliyokuwa Idara Kuu ya Hali ya Hewa kwa kipindi
cha miaka 8 kuanzia 1992 hadi 1999 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya
Hewa Tanzania kwa kipindi cha miaka 9 kuanzia 1999 hadi 2008. Dr. Mhita kwa
kushirikiana na uongozi wa iliyokuwa idara Kuu ya Hali ya Hewa alishiriki katika
kuishauri Serikali kuhusu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
kutoka iliyokuwa Idara Kuu ya Hali ya Hewa.
Pamoja
na nafasi ya Mkurugenzi Mkuu pia alikuwa Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika
Shirika la Hali ya Hewa Duniani kuanzia mwaka 1992 hadi 2008. Alichaguliwa kuwa
Mjumbe katika Baraza Kuu la Shirika la Hali ya Hewa Dunia kuanzia mwaka 1995
hadi 2007. Alichaguliwa kushika nafasi
ya Rais wa Jumuiya ya Hali ya Hewa katika Bara la Afrika (RA 1) kuanzia mwaka 1998 hadi 2007. Dkt Mhita
alikuwa Rais wa ‘Tanzania Meteorological Society’ sambamba na nafasi nyingine
nyingi mbalimbali alizoshika ndani na nje ya nchi.
Akielezea
baadhi ya mambo makubwa yatakayomfanya Dkt. Mhita aendelee kukumbukwa,
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Dkt. Agnes Kijazi alisema ‘Dkt.
Mhita atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika kuendeleza sayansi ya hali ya
hewa hapa nchini, katika Bara la Afrika na Duniani kwa ujumla hususani katika ushiriki
wake wa kuianzisha Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini kwa kuandaa dira (vision) na
dhamira (mission) ya Mamlaka kwa kipindi cha miaka kumi na tano (15) kuanzia
mwaka 2000 hadi 2015’.
Dkt.
Mohamed Mhita ni mmoja kati ya wanasayansi waliokuwa zao la chuo kikuu cha Stolkholm,
Sweden ambako alitunukiwa shahada ya hali ya hewa (BSc. Met) mwaka 1977. Kuanzia mwaka 1981 hadi 1984 alikuwa
mafunzoni katika chuo Kikuu cha Reading,
Uingereza ambako alitunikiwa shahada ya uzamivu (PhD). Hapa nchini alipata mafunzo
ya Sekondari katika shule za Tanga na Kamrimjee zote zikiwa mkoani Tanga.
Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania inajumuika na familia, ndugu, jamaa na marafiki katika
kuomboleza msiba huu.
IMETOLEWA
NA: MONICA MUTONI AFISA MAHUSIANO MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA.

No comments:
Post a Comment