Wastara Juma
KWAKO mwanamke unayejua kuuvaa vyema uhusika katika sinema za Kibongo, Wastara Juma. Za siku nyingi? Uko poa mama! yake?
Ukitaka kujua afya yangu mimi ni mzima wa afya, naendelea na mishemishe zangu za kila siku kuhakikisha mkono unakwenda kinywani. Nimekukumbuka hapa leo maana ni kitambo kidogo hatujaonana.
Dhumuni la barua hii ni kwanza kutaka kukukumbusha juu ya heshima niliyokuwa nakupa. Nilikuwa nakuheshimu kama mama wa watoto wawili, mtu mzima mwenye busara za kutosha.
Kwa levo ya heshima niliyokuwa nakupa, sikuwahi kuwa na shaka kwamba labda kuna siku unaweza ukabadilika. Niliamini kadiri siku zilivyozidi kusonga ndivyo busara zaidi zingeendelea kujaa katika kichwa chako.
Nilikuheshimu kama mama jasiri sana. Historia ya maisha yako inaonesha umepitia mitihani mingi, kwa namna ambavyo umepambana na kuvuka viunzi hivyo, hakuna ambaye anaweza kuwa na shaka na wewe zaidi ya kukupongeza na kukuona ni mfano wa kuigwa.
Ulipambana sana kutetea uhai wa mumeo hadi pale Mungu alipomchukua. Nikwambie Watanzania walikupa heshima ya juu. Mimi mwenyewe nilikuheshimu sana. Sikuwahi kutarajia kama siku moja unaweza kushusha heshima yako kirahisi kama wafanyavyo baadhi ya wasanii.
Sikuwahi kuwaza kama kuna siku ninaweza kukuona umevaa mavazi ya ajabu kama wafanyavyo baadhi ya wenzako, achilia mbali ulevi wa kupindukia.
Niliamini wewe ndiye mtu wa kukemea wenzako wanaotoka nje ya mstari wa kujiheshimu.
Licha ya kukuheshimu huko kwa muda mrefu, juzikati ulifanya tukio ambalo nilipoliona, akili yangu ilishindwa kuamini kama ni wewe yule ninayekuheshimu. Nazungumzia matusi mazito uliyoyaporomosha kwenye mtandao wa Instagram.
Ulimtukana mmoja wa mashabiki wako matusi mazito ya nguoni. Najua kabisa kwamba alikuudhi na kama binadamu unakasirika, lakini siku zote kabla ya kufanya jambo lolote lazima kwanza uangalie nafasi yako katika jamii.
Huwezi kumuona chizi anakutukana eti na wewe ukamtukana ili kumkomoa. Mwenye busara na hekima, akitukanwa na chizi, hukaa kimya na mwisho wa siku watu hubaini nani ni chizi!
Kwa matusi uliyomlipizia yule shabiki wako, waungwana walikujadili wewe uliyejibu badala ya shabiki wako.
Walikuona hukutumia busara. Kwa nafasi yako katika jamii, ukisema umjibu kila atakayekutukana, utawatukana wangapi? Jamii nayo itakuelewaje?
Nikuambie tu dada yangu hukufanya kitu kizuri hata kidogo, wewe ni staa mwenye heshima kubwa, huwezi kutukana matusi mazito kiasi kile hadharani, tena kwenye akaunti yako ambayo unaitumia kufanya biashara mbalimbali.
Binafsi tangu siku ile niliposoma posti yako nilijisikia vibaya, sikutegemea. Ningekushauri, ili kurejesha heshima yako, omba radhi na kubadilika. Kwa leo ni hayo tu.
Wasalaam
No comments:
Post a Comment