Viongozi wa Tanzania na Comoro, katikati ni Rais wa Visiwa vya Comoro Mhe. Dk. Ikililou Dhoinine, akiwa na Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania na kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania kwenye Kongomano la Biashara wakifuatilia
Rais wa Visiwa vya Comoro Mhe. Dk. Ikililou Dhoinine, akizungumza na Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania wakati wa ufunguzi rasmi tarehe 23 Aprili 2015 Moroni.
Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania akihutubia kongomano kubwa la biashara baina ya Tanzania na Comoro jijini Moroni Alhamis tarehe 23 Aprili 2015.
JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA
MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Nukushi: 255-22-2116600 |
20 KIVUKONI FRONT,
P.O. BOX 9000,
11466 DAR ES SALAAM,
Tanzania.
|
Membe awahimiza Watanzania
kuchangamkia fursa za kibiashara na kuwekeza katika Visiwa vya Comoro
Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) amewahimiza wafanyabiashara wa Tanzania
kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji Visiwani Comoro kwani uhusiano
baina ya nchi hizi mbili umeimarika.
Mhe. Membe alitoa
kauli hiyo wakati akilihutubia Kongamano la Biashara baina ya Tanzania na Comoro
lililoandaliwa na Balozi za Tanzania na Comoro kwa kushirikiana na sekta
binafsi za nchi hizo mbili jijini Moroni, Comoro tarehe 23 Aprili, 2015.
“Watanzania tunathaminiwa sana hapa kutokana
na mchango wetu mwaka 2008 tulipokikomboa Kisiwa cha Anjouan kutoka kwa Kanali
Bacar. Sasa Serikali ya Umoja wa Visiwa vya Comoro imeimarika na uhusiano wetu
umeshamiri. Wanatukaribisha sisi kwanza kushirikiana kibiashara, tuchangamkie
fursa hii” alisema Waziri Membe.
Vilevile, Mhe. Membe alisifu jitihada za ofisi za
ubalozi wa nchi hizi mbili kwa kuitikia wito wa kuimarisha uhusiano wa
kibiashara kwa kuandaa kongamano hilo la kihistoria.
“Rais Kikwete
alipofanya ziara yake hapa mwaka 2014, aliahidi kukuza uhusiano wetu na kutoa
wito wa kushirikiana kibiashara kwa manufaa ya nchi zetu. Nawapongeza sana
Balozi Kilumanga na Balozi Fakih kwa kushirikiana na sekta binafsi na
kutekeleza hili kwa wakati”alisema Waziri Membe, ambaye aliongoza ujumbe wa
Tanzania kwenye kongamano hilo.
Kwa upande wake, Rais
wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Ikililou Dhoinine alisema kuwa yeye na Serikali yake
wanathamini mchango mkubwa wa Tanzania kwa watu wa Comoro na hivyo atahakikisha
uhusiano wetu unakua kwenye nyanja zote, Serikalini, sekta binafsi na hata
baina ya watu wa nchi zote mbili.
Aidha, baada ya
ufunguzi rasmi wa kongamano hilo, wafanyabiashara wa Tanzania walikutanishwa na
wenzao wa Comoro kwenye makundi madogo madogo ili kuibua changamoto zinazokwaza
biashara baina ya nchi hizo. Mikutano hiyo inatarajiwa kuibua njia bora zaidi
ya kuwezesha biashara baina yao na kuimarisha uhusiano baina ya watu wake.
Akiwa jijini
Moroni, Mhe. Membe alipata fursa ya kutembelea fukwe za bahari ambazo ni
vivutio vikubwa vya utalii kwenye nchi hiyo ya visiwa akiwa na mwenyeji wake
Mhe. Dkt. Alanrif Said Hussane, Waziri wa Mambo ya Nje wa Visiwa vya Comoro.
Serikali ya
Tanzania ilifungua ofisi zake za ubalozi mwaka 2013 ambapo inawakilishwa nchini
humo na Mhe. Chabaka Kilumanga, Balozi wa Tanzania, mwenye makazi yake Moroni.
Kwa upande wa Serikali ya Comoro ilifungua Ubalozi wake nchini Tanzania mwaka
2014 na inawakilishwa na Mhe. Ahamed El Badaoui Mohamed Fakih Balozi wa Comoro
mwenye makazi yake Dar es salaam.
Kongamano hilo la
siku mbili lililofunguliwa na Mhe. Ikililou Dhoinine, Rais wa Visiwa vya Comoro,
lilifanyika kwenye ukumbi wa bunge jijini Moroni, mojawapo ya visiwa vitatu
vinavyounda Umoja wa Visiwa vya Comoro, na kuhudhuriwa na wafanyabiashara
takriban mia moja kutoka Tanzania. Visiwa vingine vinavyounda umoja huo wa
Comoro ni Ngazija (Grand Comoro), Anjouan na Moheli huku mji mkuu ukiwa Moroni.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa
Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Dar es Salaam
24 Aprili 2015



No comments:
Post a Comment