Hata hivyo, pendekezo hilo limekataliwa na chama anachotoka Maalim Seif, yaani Chama cha Wananchi (CUF), kwa maelezo kwamba muda wa kujadili mambo hayo haujafika bado.
Gazeti hili linafahamu pia kwamba pendekezo hilo la Chadema liliwasilishwa kwanza na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kwenye kikao maalumu cha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kilichofanyika Zanzibar mwishoni mwa wiki iliyopita.
Viongozi wakuu wa Ukawa kutoka vyama vya CUF, Chadema, NCCR Mageuzi na National League for Democracy (NLD), walikutana mjini hapa kwa ajili ya kuangalia namna ya umoja huo utakavyosimamisha wagombea katika uchaguzi huu.
“Mtu wa kwanza kutoa pendekezo hilo la Maalim Seif kuwania Umakamu wa Rais wa Muungano alikuwa ni Mbowe na baadaye Makamu Mwenyekiti, Profesa Abdallah Safari, naye aligusia suala hilo.
“ Hata hivyo, majadiliano hayo hayakwenda mbali sana kwa sababu CUF walisema muda wa kujadili suala hilo haujafika kwa vile Ukawa bado hawajakubaliana kila kitu kuhusu majimbo ya ubunge na hivyo suala la Urais linaweza kusubiri,” kilisema chanzo cha gazeti hili kilichozungumza kwa masharti ya kutotajwa jina kwa maelezo kwamba si msemaji rasmi wa umoja huo.
Mmoja wa viongozi wa Ukawa aliyekuwa Zanzibar wakati wa mkutano huo, alisema suala hilo linaweza kuwa gumu kukubalika na CUF kwa sababu mbalimbali za kisiasa na kiuchumi.
“Kisiasa, kama CUF itakubali Chadema ndiyo itoe mgombea Urais na yenyewe itoe mgombea mwenza maana yake itakuwa inajiua. Labda nikwambie kwanini. Kwanza, kama mtu mwenyewe ni Maalim Seif, itabidi atoke CUF na kuhamia Chadema.
“Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa sheria za nchi, mgombea urais na yule mwenza ni lazima watoke katika chama kimoja. Sasa kweli Maalim Seif ahame CUF? Hiyo inaingia akilini kweli? Hapo kuna ugumu. Kwa kifupi naweza kusema hilo haliwezekani ng’o.
“Lakini pia usisahau, chama kitakachokuwa na mgombea urais ndicho kitakachozunguka nchi nzima kuomba kura na ndicho kitakachoonekana. Sasa kwa minajili hiyo, kama CUF haitakuwa na mgombea urais, maana yake kisiasa itakuwa inajiua yenyewe.
“ Kwenye uchumi, kuna hasara yake pia. Ruzuku ya vyama hutolewa kwa kuzingatia wingi wa kura za urais na zile za ubunge. Hata wingi wa wabunge wa viti maalumu pia unategemea wingi wa kura hizo. Ukiacha kuwania urais, maana yake unapunguza kura zako. Utapata ruzuku kidogo na itasumbua kichama.
“Tatizo ninaloliona kwa Chadema ni kwamba, nao wamekuwa kama CCM siku hizi. Wanataka kila jimbo wapewe. Ukiona mgawanyo wa majimbo utaona wao ndiyo wanaongoza. Na bado wanautaka urais. Sasa hapo unataraji nini?” alisema mmoja wa viongozi wa Ukawa aliye karibu na duru za mkutano huo.
Kama Maalim Seif angekubaliana na wazo hilo la Chadema, maana yake ni kwamba angelazimika kujitoa kuwania urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu; ambayo ingekuwa ni mara ya kwanza kwake katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.
Baada ya CUF kukataa kujadili suala hilo ambalo linadaiwa kutokuwapo kwenye ajenda za kikao hicho na kwamba ‘lilichomekewa tu’, wajumbe waliendelea na kikao hicho ambacho hatimaye kilifikia mwafaka wa namna mgawanyo wa majimbo ya ubunge utakavyokuwa katika uchaguzi wa mwaka huu.
Tayari Ukawa imeeleza mafanikio ya kikao hicho kwa kuweza kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja wa umoja huo katika majimbo yote nchini isipokuwa 30 tu, sita ya mkoa wa Dar es Salaam, ingawa nayo yanatafutiwa ufumbuzi.
Viongozi wakuu wa Ukawa waliohudhuria mkutano huo wa Zanzibar ni wenyeviti wa vyama hivyo, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia (NCCR Mageuzi), Emmanuel Makaidi (NLD) na Mbowe.
Uwezekano wa Ukawa kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu wakiwa pamoja unategemea zaidi na namna watakavyoweza kukubaliana katika ngazi ya majimbo na urais kabla ya kuingia kwenye uchaguzi.
Raia Mwema
No comments:
Post a Comment