ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 7, 2015

Simba wanakuja mdogomdogo VPL.

Kikosi cha Simba.

Simba imezidi kuongeza kasi katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Kagera Sugar.

Kwa ushindi wa mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mjini hapa baada ya kushindikana kuchezwa Jumamosi kutokana na mvua kubwa iliyonyesha, umeifanya Simba kufikisha pointi 35 moja nyuma ya Azam FC iliyopo nafasi ya pili na tano nyuma ya vinara Yanga.

Hata hivyo, Simba imecheza mechi tatu zaidi ya Azam FC na mbili zaidi ya Yanga kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 14 huku Tanzania Prisons ikiburuza mkia.

Matokeo hayo pia yanaifanya Simba kulipa kisasi cha kipigo cha bao 1-0 walichokipata kutoka kwa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa katika mzunguko wa kwanza huku ushindi pia huo ukiwa wa kwanza kwao katika Uwanja wa CCM Kambarage.

Katika kipindi cha kwanza ambacho kilimalizika timu hizo zikishindwa kutambiana, Simba wangeweza kuandika bao la kwanza dakika ya 10 baada ya beki wao wa kushoto Mohamed Hussein kupiga krosi iliyomkuta Dan Sserunkuma ambaye alionana vema na Ramadhani Singano lakini mabeki wa Kagera Sugar wakawa makini kuzima mashambulizi hayo.

Dakika 16 baadaye Sserunkuma aliwatoka mabeki wa Kagera Sugar na kuachia shuti kali kwa guu lake la kushoto ambalo liligonga mwamba na mabeki wa Kagera kuwahi na kuokoa.

Emmanuel Okwi aliwatoka mabeki wa Kagera katika dakika ya 33 na kubetua mpira uliompita kipa Agaton Anthony, lakini mabeki wa timu hiyo waliwahi kuokoa wakati mpira ukiwa karibu kuvuka mstari wa goli.

Dakika moja kabla ya kuelekea mapumziko, Simba ilipata faulo nje ya eneo la hatari lakini mpigaji Singano shuti lake hafifu liliokolewa na kipa Anthony.

Kagera Sugar pia walipata faulo nje ya eneo la hatari katika muda wa nyongeza wa kipindi cha kwanza, lakini walishindwa kuitumia nafasi hiyo.

Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kulishambulia zaidi lango la Kagera, na katika dakika ya 49, Wekundu wa Msimbazi hao walipata bao la kuongoza kupitia kwa Singano aliyeuwahi mpira uliookolewa na beki wa kati George Kavila nje ya eneo la hatari la Kagera na kupiga shuti kali lililomshinda kipa Anthony.

Kuingia kwa bao hilo kuliamsha ari kubwa kwa safu ya ushambuliaji ya Kagera, ambayo dakika 10 baadaye ilisawazisha kupitia kwa Rashid Mandawa aliyeitendea vema pasi kutoka kwa winga wa kulia Paul Ngwai ambaye aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Juma Mpola.

Bao hilo linamfanya Mandawa kufikisha mabao 10 sawa na Didier Kavumbagu wa Azam FC aliyeongoza msimamo wa wafumania nyavu kwa muda mrefu zaidi msimu huu kabla ya kinara Simon Msuva ambaye kwa sasa ana mabao 11 kumpiku.

Mchezaji pekee mwenye hat-trick msimu huu, Ibrahim Ajibu, aliifungia Simba bao la pili kwa njia ya penalti na la saba kwake msimu huu katika dakika ya 68 baada ya beki mmoja wa Kagera kuzuia shuti la Okwi kwa mkono.

Mara baada ya mchezo huo, Kocha wa Kagera Sugar, Mganda Jackson Mayanja, alisema hakufurahishwa na uamuzi wa mwamuzi, Erick Onoka kutoka Arusha, kutokana na kuibeba zaidi Simba.

"Tungeweza kushinda mechi hii, lakini refa alikuwa na matokeo mfukoni, kwani hata penalti waliyopewa Simba haikuwa halali," alisema Mayanja.

Kagera Sugar: Agaton Anthony, Erick Murilo, Salum Kanoni, Erick Kyaruzi, Geroge Kavila, Malegesi Mwangwa, Juma Mpola/Paul Ngwai, Babu Ally, Rashid Mandawa, Atupele Green na Adam Kingwande.

Simba: Peter Manyika, Nassor Masoud, Mohamed Hussein, Hassan Isihaka, Joseph Owino, Awadh Juma, Ramadhan Singano, Said Ndemla, Dan Sserunkuma, Ibrahim Ajibu na Emmanuel Okwi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: