ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 9, 2015

UKIONA UNACHUNGUZWA NA KUFUATILIWA SANA, KAA MKAO WA KUACHWA!

Mpenzi msomaji wangu, kilio cha wengi walio kwenye uhusiano ni kuhisi wanasalitiwa na wapenzi wao waliotokea kuwaamini sana. Kasi ya wapenzi kusalitiana imekuwa ikishika kasi kila siku kiasi cha baadhi kuhisi bila kusaliti hawasikii raha. Yaani wanapatilizwa kila kitu na wenza wao lakini bado wanatoka nje.

Unakuta mwanaume ana mke mzuri wa sura na tabia na anayejua mapenzi na kila kitu lakini bado mwanaume huyo haridhiki, anachepuka tena kwa wanawake wasio hata wa hadhi yake (mume wa mtu kutembea na machangudoa).

Pia wapo wanawake ambao wamebahatika kuwapata wanaume ‘handsome’, waliotulia, wanaojua mapenzi na kujali pia lakini bado tamaa za usaliti wanakuwa nazo. Ukiuliza kipi kigeni wanachofuata huko nje, huwezi kupata jibu la maana.

Nilishawahi kufanya uchunguzi huko nyuma kwa kuzungumza na baadhi ya wapenzi kuhusu hili suala la usaliti. Wengi walikiri kujua kwamba kuna uwezekano mkubwa wapenzi wao wanawasaliti lakini wenyewe wanadai ni mambo ambayo wakiyafuatilia sana wanaweza kujikuta wanaachana wakati huenda bado wanapendana.

“Hivi unadhani ni wakati wa kuaminiana kwa asilimia zote? Binafsi kwa ninavyomjua mpenzi wangu na huu utitiri wa wanawake micharuko huko mtaani, nahisi kwake itakuwa ngumu sana kuvumilia, ila kinachonifanya niwe na amani ni kwamba, ananiheshimu na sijawahi kumfumania.

“Hilo ndilo linalonifanya niwe mpole ila najua hakosi mchepuko na nikimfuatilia najua wazi kuwa nitamfuma, tutagombana na hata kufikia hatua ya kuachana, sasa ya nini hayo? “Maana ninachojua ni kwamba, ukimfuatilia sana mpenzi wako unatafuta sababu ili muachane, sasa kama hauko tayari muachane ni vyema ukamuamini na kama huko pembeni ana vichenchede, ni yeye na Mungu wake” alisema Suzana wa Kinondoni jijini Dar ambaye ndoa yake sasa ina miaka 10.

Mwingine ambaye nilibahatika kuzungumza naye alijitambulisha kwa jina la Salehe wa Magomeni jijini Dar. Huyu anaeleza kuwa, amekuwa akishuhudia wanawake wengi anaowaheshimu wakiwasaliti wapenzi wao. Hili linamfanya hata mpenzi wake asimuamini kwa asilimia mia moja.

Hao ni watu wachache tu ambao niliongea nao lakini wengi walikiri usaliti upo tena wanaoongoza kusaliti ni wale ambao wapenzi wao wanawaamini sana. Hii yote inaonesha ni kwa jinsi gani mapenzi ya sasa usaliti unachukuliwa kama fasheni. Yaani mwanamke fulani akimuona shoga yake ana kidumu (mwanaume wa pembeni) basi naye anatafuta ili waende sawa. Huu ni ulimbukeni uliopitiliza.

Nini cha kufanya?
Kutokana na kautafiti hako nilikofanya ambako naamini hata wewe unakubaliana nako, kuna kila sababu kila aliye kwenye uhusiano kumuamini mwenza wake kwa kiwango kinachostahili.
Sisemi umuamini tu hata kama unaona anakuchezea rafu huko kizani, lahasha! Muamini pale ambapo una sababu ya kufanya hivyo.

Ukiona dalili za wazi kwamba anakusaliti, ukafuatilia na kugundua ni kweli ana mchepuko, hutakiwi kuvumilia. Mtu huyo atakuwa hana nafasi kwenye maisha yako hivyo haraka muweke kando.Lakini sasa, hii tabia ya kumchunguza na kufuatiliana sana haifai. Kuna msemo usemao mkimchunguza sana bata huwezi kumla. Kwenye mapenzi nako kwa kuzingatia msemo huo ni kwamba, ukimchunguza sana mpenzi wako huwezi kudumu naye.

Hii ni kwa sababu ukiamua kufuatilia sana nyendo za mpenzi wako kuna mambo utayabaini na utashindwa kuendelea kuwa naye. Kwa maana hiyo unatakiwa kujenga hisia za lazima kwa mpenzi wako ili uwe na amani.
Hii kufuatilianafuatiliana kwa wapenzi kunaboa na kama nilivyosema huko nyuma kwamba kufanya hivyo unaweza kumpa hisia mpenzi wako kwamba humpendi na unatafuta sababu za kuachana naye.

Ndiyo maana wataalam wa masuala ya mapenzi wanasema kwamba ukiona mpenzi wako anakufuatilia na kukuchunguza sana, kaa mkao wa kuachwa!
Ni hayo tu kwa leo.
GPL

No comments: