ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 7, 2015

ILO TANZANIA YAADHIMISHA MIAKA 5 YA KUWAWEZESHA VIJANA TANZANIA KUPITIA UJASIRIAMALI


Mkurugenzi Mkazi wa UNDP, Philippe Poinsot akizungumza wakati wa kongamano
Mshauri Mkuu wa Ufundi wa Mradi, Bwana Jealous Chirove, akielezea mafanikio ya mradi
 Naibu waziri wa kazi na ajira, Mheshimiwa Makongoro Mahanga akimkabidhi cheti cha kutambua mchango wa serikali ya Zanzibar katika mradi wa ujasiriamali, ndugu Ameir Ali Ameir, ambaye ndiye Mkurugenzi wa Ajira kutoka Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma, Zanzibar.
Mkurugenzi wa Ajira kutoka Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma, Zanzibar.ndugu Ameir Ali Ameir akizungumza na waandishi wa habari.
 Mkurugenzi Mkuu wa ILO Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda Bwana Alexio Musindo akizungumza na waandishi wa habari.

Naibu waziri wa kazi na ajira, Mheshimiwa Makongoro Mahanga akizungumza na waandishi wa habari. 
   Baadhi ya wahudhuriaji wa kongamano la kuadhimisha Miaka mitano ya mradi wa Ujasiriamali uliokuwa unaendeshwa na Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO).

ILO Tanzania yaadhimisha miaka 5 ya kuwawezesha vijana Tanzania kupitia ujasiriamali. Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO) leo limeadhimisha miaka 5 toka kuanzishwa kwa mfuko wa ujasiriamali wa vijana (YEF) kwa kuandaa kongamano katika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere. 


Mfuko wa Ujasiriamali kwa vijana ulizinduliwa mwaka 2010 ukilenga katika kutengeneza ajira kwa vijana kwa kupitia ukuzaji wa sekta binafsi pamoja na kuongeza ushindani kwenye uchumi wa Afrika. 

Mradi ulijikita katika kuwatengenezea vijana ajira nzuri, kukuza ujasiriamali na kuwatengenezea fursa vijana wa kiafrika kupitia elimu, kuwaongezea ujuzi na uwezeshaji wa mtaji. Kwa kupitia mradi huu wa Kuwezesha Ujasiriamali, Mfuko wa Ujasiriamali kwa vijana ulilenga kutengeneza maelfu ya ajira kwa vijana katika nchi za Kenya, Tanzania na Uganda. 

Msingi mkuu wa mradi ulikuwa kukuza utamaduni wa ujasiriamali miongoni mwa vijana, kuingiza elimu ya ujasiriamali katika mitaala, kuongeza uwingi wa mambo yanayowezekana katika ajira kwa vijana, kuwezesha taasisi za vijana kutekeleza mawazo mazuri ya ujasiriamali na kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa vijana walio nje ya shule. 

Toka mradi umeanzishwa, umewezesha zaidi ya vijana 30,000 ambao ni wajasiamarali wapya na waliopo kupitia utoaji wa elimu ya biashara, kusaidia uanzishwaji wa biashara zaidi ya 17,000 pamoja na utengenezaji wa zaidi ya ajira 40,000 kwa vijana, ambayo vyote kwa pamoja vimevuka malengo ya mradi yaliyoaninishwa mwanzo. 

Pamoja na hayo, mradi pia umewezesha: 
· Zaidi ya biashara 16,000 zimeanzishwa ikiwa ni matokeo ya elimu ya biashara 
· Zaidi ya kazi 30,000 zimetengenezwa 
· Zaidi ya vijana1,000,000 wamefikiwa kupitia vyombo vya habari (radio, magazeti) na majukwaa mengineyo. 
· Zaidi ya wajasiariamali 30 wa mfano wametangazwa 
· Zaidi ya wanafunzi 50,000 wamepata elimu ya ujasiriamali 
· Zaidi ya walimu 340 wa shule za msingi, sekondari pamoja na vyuo wameendelezwa 
· Jumla ya tathmini 6 zimefanyika pamoja makongamano 3 ya kisera 
· Miradi 33 imefanyika na taasisi za vijana 
· Zaidi ya vijana 30,000 wamepata elimu ya biashara 

Akizungumza wakati wa kongamano, Mshauri Mkuu wa Ufundi wa Mradi, Bwana Jealous Chirove alisema tathmini yao kwenye mradi imeonyesha kuwa zaidi ya asilimia 50% ya vijana waliopata elimu ya biashara wameweza kuanzisha biashara ndani ya miezi 12 huku wastani kila biashara ikitengeneza ajira mbili. 

‘Mradi umepata mafanikio makubwa kwani kwa Tanzania pekee zaidi ya biashara 10,000 zimetengenezwa ambazo zimepelekea zaidi ya nafasi za ajira 20,000 ambazo kwa hakika ni mchango mkubwa katika kupambana na tatizo la ajira hapa nchini’ alisema Chirove. 

Mafanikio mengine ya mradi ni uanzishwaji wa mradi wa Kazi Nje Nje ambao unawatumia wahitimu kutoka vyuoni kuwafikia vijana walio mtaani na ujumbe kuhusu ujasiriamali pamoja na uanzishwaji wa mashindano ya kuandika mradi wa biashara uliowafikia moja kwa moja zaidi ya vijana 70,000. 

Mgeni rasmi wa Kongamano hili ambalo limehudhuriwa na wadau mbalimbali ni Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Mheshimiwa Makongoro Mahanga amepongeza mchango wa ILO na Mfuko wa Ujasiriamali kwa mradi wao huu. 

‘Tatizo la ajira kwa vijana bado ni changamoto kubwa kwa nchi zinazoendelea na bara zima la Afrika kiujumla hasa kutokana na ongezeko kubwa la wahitimu kutoka katika vyuo mbaliumbali hapa nchini, hivyo tunaishukuru ILO na serikali ya Denmark kwa juhudi zao za kuisaidia serikali kumaliza tatizo hili’ alisema Mheshimiwa Mahanga. 

Mheshimiwa Mahanga alisema mpaka sasa ni asilimia 25 tu ya watu wanaoingia kwenye soko la ajira ndio wanaajiriwa kwa mwaka kwenye sekta binafsi.

No comments: