Advertisements

Sunday, May 3, 2015

ISHU SIYO KUPEWA MIMBA, ANAYEKUPA NI NANI, WAKATI GANI?

NIJumamosi nyingine tena Mungu ametukutanisha katika safu yetu hii ya Show The Love, kwenye uwanja wetu huu tunaweza kupeana mawili matatu yahusuyo maisha ya uhusiano.
Niwashukuru wote walionitumia meseji kuonesha wameguswa na mada ya wiki iliyopita iliyokuwa inasema; ‘kuna ulazima wowote wanandoa kufichana vipato vyao?’
Hakika ulijifunza vya kutosha, moja kwa moja twende tukaitazame mada yetu ya leo iliyopo hapo juu.
Kizazi cha sasa kimebadilika. Kutokana na ongezeko la wanawake wengi wanaofikia hatua ya kuolewa na kutofanikiwa jambo hilo, wengi wao wamejikuta wakipatwa na tatizo la kutaka kuzaa kwa lazima.Yeye haangalii anayezaa naye ni nani wala kama hajui kwamba ni muda gani mzuri kwake anaostahili kupata mtoto na atamleaje.
Umri unakuwa umekwenda, kinachofuata hapo ni zile kauli za ‘acha tu nizae na mimi hata nipate mtu wa kuniliwaza.’
Hapo ndipo mwanamke anapolazimisha mwanaume ampe mimba. Haijalishi anayempa hiyo mimba ana historia gani. Yeye anachotaka kwa wakati huo ni mimba, mengine yatafuata baadaye.
Anataka eti akifa leo na yeye aache chata yake duniani. Kwa wakati huo ni rahisi sana kumpata mtu asiyekuwa na malengo yoyote ya maisha na kumruhusu ampe mimba.Matokeo yake, mtoto anapozaliwa anakosa malezi ya upande wa baba kama si pande zote mbili kama mama naye anakuwa hajiwezi, mtoto anajikuta akiishi katika mazingira magumu.
Furaha ile ambayo watoto wengine wanaipata, mtoto atakayezaliwa hapo ataikosa. Mama anakuwa na nia nzuri ya kuzaa lakini hafikirii tena kuhusu malezi.Tatizo lingine linaloweza kumkuta mwanamke huyo ni magonjwa. Atakutana na mtu ambaye hamjui historia yake, hajui afya yake lakini kwa kuwa anataka na yeye aitwe mama basi anaamua kukubaliana naye na kujikuta akiambulia magonjwa hatari ikiwemo Ukimwi.
Haya yote yanatokea kama hujayapanga vizuri maisha yako. Hujajipanga tangu ukiwa mdogo kwamba ujiheshimu ili kutengeneza mazingira mazuri ya kuwa ‘waifu matirio’ hapo baadaye.Wanaume wa siku hizi ni wajanja. Wanajua kucheza na akili za wanawake. Ili aamue kuzaa na mtu, lazima awe ameshampima vya kutosha kwamba aliye naye ni sahihi au si sahihi.
Hata akigundua si sahihi, wengi wao bado wanajua namna ya kuishi na mtu ambaye si sahihi kwao. Anajua kabisa huyu ni mtu wa ‘kuzugia’ lakini muolewaje yupo pembeni au atatokea baadaye.Kwa nini ukubali kuwa mtu wa kuzugia? Uamuzi ni wako kama utaishi katika misingi mizuri ya kuwa mke.Mwanaume ambaye amekufanya wa kuzugia, ukianza kutilia shaka penzi lake, anakuruhusu tu uende zako. Hana cha kupoteza maana hana malengo na wewe.

No comments: