ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 9, 2015

KAMATI YA BUNGE YA HUDUMA ZA JAMII YAFANYA ZIARA HESLB

Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii wakipata maelezo kutoka kwa mkuu wa moja ya idara za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Wa kwanza kulia ni Kaimu Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Gregory Teu.
Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Sheria wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Bw. Firmat Tarimo akielezea shughuli zinazofanywa na kitengo hicho.
Meneja wa Mifumo ya Kompyuta na Utunzaji wa Kumbukumbu wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Bw. Bahati Singa akiwaelezea wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii jinsi ambavyo kumbukumbu za wanafunzi zinatunzwa baada ya kupokelewa Bodi.
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii Mhe. Christowaja Mtinda akichangia maoni yake baada ya taarifa ya utekelezaji wa Bodi kuwasilishwa mbele ya kamati.


Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii imefanya ziara kwenye ofisi za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu jijini Dar es Salaam na kuitaka Bodi kuwasilisha changamoto za kisera ili ziweze kufanyiwa kazi kwa wakati. ikiwa ni pamoja na ufinyu wa bajeti ya fedha za ukopeshaji.

Akizungumza baada ya  taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi kuwasilishwa, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Gregory Teu amesema kuwa yeye na wanakamati wenzake wamejifunza kwa kina kupitia ziara hiyo na kwamba bila kufika Bodi ni vigumu kujua ni kwa jinsi gani shughuli za utaoji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu zinafanyika kwa weledi mkubwa na bila upendeleo.

Awali wakati akitoa neno la utangulizi kwa niaba ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Consolata Mgimba alielezea umuhimu wa ziara hiyo kwa Bodi na kuwashukuru wajumbe wa Kamati ya Huduma za Jamii kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wakiutoa kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na taasisi zake ikiwemo Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.

Baada ya taarifa ya utekelezaji wa Bodi kuwasilishwa, baadhi ya wajumbe wa kamati walichangia maeneo mbalimbali ya utoaji na urejeshwaji wa mikopo na kuitaka Bodi kuwasilisha changamoto za kisera ili ziweze kufanyiwa kazi, mojawapo likiwa ni ufinyu wa bajeti ya fedha za ukopeshaji ambapo kwa miaka mitatu mfululizo serikali  imekuwa ikitenga Shilingi bilioni 306 wakati idadi ya wahitaji wa mikopo inaongezeka kila mwaka. 

Wajumbe hao wa Kamati ya Huduma za Jamii wametembelea idara na vitengo mbalimbali vya Bodi kushuduhudia huduma zinavyotolewa kwa wanafunzi wa elimu ya juu wa ndani na nje ya nchi.

Ziara hiyo imewawezesha wajumbe wake kupata maelezo kutoka kwa watendaji wa Bodi kuanzia mchakato wa maombi ya mikopo, uchambuzi na upangaji, utoaji wa mikopo na uhifadhi wa taarifa za wanafunzi kwa ajili ya urejeshwaji wa mikopo hiyo baada ya kuhitimu masomo yao.

Ziara ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii ni sehemu ya majukumu yake ya kutembelea taasisi zinazotoa huduma kwa jamii na kupokea taarifa za utekelezaji wa utoaji huduma hizo.

No comments: