ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 29, 2015

Kashfa Escrow imeharibu nchi



Dotto Mwaibale
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimetoa ripoti ya mwaka 2015, inayoonesha kuwa kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow iliyohusisha idara mbalimbali za Serikali imeharibu sifa ya nchi.
Imesema Tegeta Escrow imekuwa ni mojawapo ya matukio makubwa ya kashfa za rushwa kupata kutokea nchini, ambapo inahusisha watu kutoka kada mbalimbali za jamii kuanzia Serikali Kuu, Idara ikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na pia Rita.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Helen Kijo-Bisimba alibainisha hayo Dar es Salaam jana, wakati akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari na wadau wengine kwenye maadhimisho ya miaka 20 ya LHRC ya uangalizi na utetezi wa haki za binadamu.
Kashfa hii pia ilihusisha viongozi wa taasisi za kidini ambao walihusishwa na kupokea fedha zilizotokana na kashfa hii kupitia akaunti katika Benki ya Mkombozi.
“Kwa ujumla ni kwamba kashfa hii imeharibu sana muonekano wa Serikali kuu. Idara nyingine muhimu za Serikali pia zilihusishwa katika kashfa hii, ikiwamo Idara ya Mahakama kupitia kwa majaji ambao walihusishwa na kupokea miamala kutokana na kashfa hii. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaihusisha kashfa hii moja kwa moja na mmomonyoko wa maadili katika jamii unaotokea nchini.
“Hii ni kwa sababu taasisi zinazoaminika ndizo zilizohusika katika kashfa hii. Utendaji wa kifisadi na manunuzi kinyume cha sheria yanaathiri utaratibu mzima wa manunuzi ya Serikali, lakini pia yanaathiri uchumi wan chi na wananchi kwa ujumla,” alisema Bi Simba.

Huduma za kijamii
Mkurugenzi huyo alisema taarifa hiyo pia inaonesha maelezo ya upatikanaji na usambazi wa huduma za kijamii hususani huduma za afya, elimu na maji, utoaji mbovu wa huduma za afya unahatarisha moja kwa moja haki ya kuishi kama ilivyoanishwa na Katiba ya Jumhuri ya Muungano wa Tanzania.
Na kwamba upungufu wa upatikanaji wa huduma za maji kwa nchi yenye vyanzo vikubwa vya maji kama Tanzania inanyima haki za wanawake na watoto hasa mtoto wa kike, kwani wanatumia muda mwingi katika kusaka maji.

Alisema utoaji wa elimu isiyo bora inaathiri kwa kiwango kikubwa haki ya ukuzi na maendeleo ya kitaaluma ya mtu mmoja mmoja na kuwa kiasi kikubwa cha fedha kilichopotea kupitia Akaunti ya Escrow zingeweza kusaidia kuimarisha huduma hizo za kijamii hasa maeneo ya vijijini.

Migogoro ya ardhi

Bi Simba alisema kwa mwaka 2014, migogoro inayohusisha matumizi na umiliki wa ardhi yalikithiri nchini pote, ambapo katika maeneo mengine ilisababisha vifo na majeruhi kwa wananchi wengi.
Ambapo Januari mwaka jana, watu kadhaa waliuawa wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara. Na kwamba taarifa hiyo imeangalia sababu ya migogoro na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kupunguza au kumaliza kabisa migogoro ya aina hiyo kwa siku za usoni.
Kituo hicho kimependekeza kuwe na mipango madhubuti wa matumizi bora ya ardhi kwa ngazi ya vijiji. Kwa sasa mpango wa matumizi ya ardhi katika ngazi ya kijiji umeshindwa kwa kiasi kikubwa kutekelezeka, kiasi cha kusababisha jamii ya wafugaji zishindwe kuishi kwa amani na jamii ya za wakulima katika eneo moja.
Ukiukwaji kisiasa
Alisema mwaka 2014, kulikuwa na matukio ya kadhaa ya ukiukwaji wa haki za kisiasa kwa mfano watu kadhaa walishindwa kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa sababu ya matatizo ya kiutaratibu kama kushindwa kujaza fomu.
Pia, taarifa hiyo inaeleza kuwa kulikuwepo matukio ya ukiukwaji wa haki ya kuishi kupitia matukio yanayohusiana na imani za kishirikina, kujichukulia sheria mkononi na vile vile mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Matukio hayo yalisababisha vifo vya watu 320 kutoka na imani za kishirikina, kujichukulia sheria mkononi watu 473 na watu watatu wenye ulemavu wa ngozi.

Uvamizi vituo vya polisi
Alisema kuwa katika kipindi hicho kulikuwepo kwa matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi, matukio ambayo yalisabisha vifo vya kinyama kwa askari polisi watatu na wengine kujeruhiwa.
Matukio hayo yalienda sanjari na kuibiwa kwa silaha za jeshi la polisi ambazo zinaaminika zinaenda kutumika kwa uhalifu, hivyo LHRC kinaishauri Serikali kuhakikisha kuwa vituo vya polisi vinakuwa na ulinzi madhubuti ili kuzuia kutokea tena kwa matukio hayo.
Deni la Taifa
Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa kumekuwepo kwa ongezeko kubwa la deni la taifa. Kwa sasa deni hilo lipo katika asilimia 42.7 ya Pato la Taifa (GDP). Tanzania kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na deni kubwa la taifa miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki.

No comments: