ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 29, 2015

Mawaziri wa sasa,wa Nyerere ,mbingu na nchi


Peter Ambilikile
BARAZA la Mawaziri la sasa ambalo lina asilimia 95 ya wasomi na wenye umri zaidi ya miaka 50, limekuwa likikumbwa mara kwa mara na kashfa za ufisadi na kukosa uwajibikaji, ukilinganisha na baraza la Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Amani Abeid Karume.
Uchambuzi uliofanywa na gazeti hili unaonesha kwamba kati ya mawaziri 31 kamili, ni mawaziri sita tu ndiyo wenye umri wa miaka chini ya 50.
Mawaziri hao ni Waziri wa Fedha, Saada Mkuya (40), Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu (45), Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (47), Waziri wa Ulinzi, Dk. Hussein Mwinyi (49), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama (48) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia (49).
Mbali ya mawaziri wa Rais Jakaya Kikwete kuwa idadi kubwa ya mawaziri wenye umri mkubwa, lakini hata mawaziri waliokuwa katika awamu iliopita iliyoongozwa na Rais Benjamin Mkapa, wengi walikuwa na umri mkubwa.
Hali hiyo ya kuwa na baadhi ya mawaziri wasiotimiza majukumu yao ipasavyo, tumeshuhudia Rais Kikwete na hata Mkapa wakifanya mabadiliko ya baraza la mawaziri mara kwa mara.
Baadhi ya kashfa nzito zilizoitikisa nchi hii katika miaka ya hivi karibuni ni ufisadi katika Mfuko wa Kuwezesha Uagizaji wa Bidhaa Kutoka nje ya Nchi (Commodity import Support-CIS), kashfa ya rada, EPA, Richmond, Operesheni Tokemeza na uchotwaji wa mamilioni ya fedha kutoka katika Akaunti ya Escrow.
Kushindwa kuwajibika kwa baadhi ya mawaziri kumedhihirishwa pia na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo kila mwaka imekiwa ikianika madudu na ulaji mkubwa wa fedha za umma.

Hali hii imekuwa tofauti na Baraza la Serikali ya Mwalimu Nyerere ambalo lilikuwa na mawaziri vijana wenye umri wa chini ya miaka 40 ambao walikuwa na elimu ya kati.

Serikali ya sasa

Umri wa viongozi wa juu wa Serikali na miaka yao katika mabano ni kama ifuatavyo; Rais, Jakaya Kikwete (65), Makamu wa Rais, Dk Mohamed Ghalib Bilal (70), Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (67) na Waziri wa Uchukuzi Samuel Sitta (73).
Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nangu (63), Waziri wa Ujenzi, John Magufuli (56), na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais asiyekuwa wizara Maalumu, Prof. Mark Mwandosya (66).
Wengine ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira (70), Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa (58), na Waziri Jinsia na Watoto, Sophia Simba (65).
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Kimataifa, Benard Membe (62), Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe (64), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika (67) na Waziri wa Utumishi, Celina Kombani (56).
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (60), Waziri wa Ushirikano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe (60), Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara (60), na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda (62).
Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan (55).

Utawala wa Nyerere
Umri wa safu ya uongozi wa Mwalimu Nyerere ulikuwa kama ifuatavyo;
Rais Julius Nyerere (39), Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Oscar Kambona (33), Waziri wa Fedha, Amir Jamal (40), Paul Bomani (37), na Waziri wa Elimu, Solomoni Eliufoo (40).
Aidha, wengine ni Waziri Mkuu, Rashid Kawawa (37), Waziri wa Viwanda, Nsilo Swai (35), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Usalama wa Taifa, Bhoke Munanka (34), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Job Lusinde (31) na Chediel Mgonja (36).
Wengine ni Waziri wa Ushirika na Maendeleo ya Jamii, George Kahama (32), Waziri wa Umeme, Jeremiah Kasambala, na Waziri wa Sheria, Abdallah Fundikira (40).

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
Hata mawaziri waliounda Serikali ya Mapinduzi Zanzibar nao walikuwa na umri usiopungua miaka 45.
Mawaziri hao ni Abdulaziz Twala (Msaidizi Waziri katika Ofisi ya Rais), Aboud Jumbe (Waziri wa Siha na Majumba), Hasnu Makame (Waziri wa Fedha na Maendeleo), Othman Shariff (Waziri wa Elimu na Mila), Abdulrahman Babu (Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara), Abdallah Hanga (Makamu wa Rais ZNZ), Saleh Saadalla (Waziri wa Kilimo), Idris A. Wakil (Waziri wa Kazi Njia na Nguvu za Umeme), Hassan Nassoro Moyo.

Aliyekuwa Waziri Mkuu Hayati Moringe Sokoine na pia Dk. Salim Hamad Salim wote walianza kazi na kutekeleza majukumu hayo kwa ufanisi mkubwa wakiwa na umri kati ya miaka 30-40.
Hassan Nassoro Moyo
Muasisi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hassan Nassoro Moyo, amesema mawaziri wengi wa sasa wapo kwa ajili ya kutengeneza fedha na si kutumikia wananchi kama zamani.
Mzee moyo anakubaliana na utendaji uliotukuka enzi za serikali ya wasisi wa taifa, Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume ambao walikuwa viongonzi wa mfano katika historia ya nchi hii.
Anasema pamoja na kuogoza wakiwa na elimu ya kawaida, lakini walifanikisha mahitaji muhimu yalioitajika kitaifa ambayo yalikuwa elimu, afya na elimu.

Akizugumzia upande wa Zarzibar, Mzee Moyo anasema baada ya Rais Karume kufanya mapinduzi alitaka watu kusau manyanyaso waliyokuwa wakipata wakati wa ukoloni.

“Ndiyo maana kuliundwa Wizara ya kuweka sawa hali za wananchi ili kila mwananchi apate sawa mahitaji bila ya kubaguliwa,” anaeleza.
Anasema wasisi pia walizingatia matumizi ya rasmali sawa, ambapo kila kilichokuwa kikipatikana kiliweza kugawanywa sawa bila ya kujali nani kafanya au nani ajafanya.

Pia, anasema baraza la mawaziri la za zamani lilifanya kazi kwa bidii zaidi na lengo kubwa kila kiongonzi aliyekuwa akichaguliwa alizigatia miiko na maadili ya kazi tofauti na ilivyo sasa, ambapo nidhamu imekuwa mbovu na ufasadi umetawala.

“Leo viogonzi wanaimba wimbo ..’How to become rich’ (Jinsi ngani akikamata madaraka ajitajirisha haraka) tofauti na zamani ambapo kiogozi alikuwa akipimwa kutokana na ufanisi wa kazi.

Anashauri wananchi wa sasa kusimamia na kuchagua watu safi wasio na ndoa kuwaongoza kuliko kupelekewa viongonzi wala rushwa na wasiotilia mkazo maslahi ya taifa.

Kasori
Aliyekuwa Katibu Binafsi wa Rais wa Mwalimu Nyerere, Samuel Kasori, akizungumzia uandilifu wa mawaziri, alisema rushwa katika nchi hii ilikuwepo kabla na baada ya uhuru, lakini kwa sasa rushwa imepanuka zaidi na kuwa na mizizi yake.

Alisema kuna rushwa ya kawaida, rushwa ya ndogo, rushwa kupitia misaada na rushwa ya kuyumbisha Serikali.
Kasori alisema rushwa au ubinafsi unasababishwa na kutoweka kwa uzalendo kwa watendaji ndani ya serikali na tasisi zake wakiwemo baadhi ya mawaziri tofauti na zamani.

Anasema wasisi walipozikomboa nchi za Tanganyika na Zanzibar kitu kikubwa walichokieneza ni uzalendo na kuhamasisha upendo na amani katika nchi zote mbili.

“Zama hizo watu walikuwa na elimu ya kati, lakini walieshimika katika kuchangia yale yaliyohitajika kuendeleza nchi,” alisema na kuongeza kuwa tofauti ya sasa wananchi wengi ngazi ya chini hawashirikishwi ipasavyo katika uamuzi wa kitaifa.
Anasema wasisi walithamini sana kutatua matatizo makubwa ya kitaifa yaliyojitokeza ghafla na kuondoa malalamiko ya wananchi wake.

Kasori anasema mfano suala la ajira na masuala ya migomo ilikuwa nadra kutokea enzi za Mwalimu Nyerere, lakini kadiri miaka ilivyokuwa ikienda hali ilibadilika kulingana na mazingira.
Anasema misimamo yake ya kusimamia maamuzi yake alifanya bila kuteteleka hata kidogo.
Kasori anasema miaka ya 1990 wanafunzi waligoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakipinga kukatwa mshahara pindi walipokuwa wakiajiriwa na baada ya kulitumikia jeshi la kujenga taifa.
Anasema uzalendo ulianzia kwa Mwalimu Nyerere mwenyewe ambaye alithubutu kukata kupumguza asilimia 20 ya mshahara wake ili fedha hiyo itumike katika kusaidia jamii, tofauti na sasa, ambapo hakuna kiongozi anayeweza kufanya kitu kama hicho.
Sarakana
Eliakimu Sarakana (75), ambaye alifanya kazi katika taasisi mojawapo ya fedha hapa nchini na kustaafu mwaka 2000, amesema mabadiliko yaliyoletwa na nchi za magharibi ndiyo chanzo cha kuwepo na matabaka katika kipato.

“Uongonzi wa sasa ambao ni wa kibinafsi kwa kujari familia bila kutumikia taifa ipasavyo na kutupa uzalendo wa nchi ndio ulianzia hapo hadi leo.”

Kuhusu mawaziri, Sarakana alisema igawa siyo wote wanaovurunda katika wizara zao, lakini kutokana na wao kujiusisha na vitendo vya rushwa, hali sio nzuri.
Alisema kutokana na kukua kwa teknolojia mawaziri wazee wameshindwa kwenda sambamba nayo na matokeo yake kujikuta wakiibiwa fedha za umma na vijana.

“lazima nchi itafute mahali ilipojikwaa na kujitathimini, uzalendo wake umepotelea wapi, kabla ya kunyosheana vidole na kikubwa ninachokiona ni maamuzi magumu ya kuchagua viongonzi wazalendo katika uchaguzi mkuu ujao,” alisema.
Mbatia
Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi James Mbatia pia amesema viongonzi wa sasa wanapeleka taifa katika machafuko kutokana na kutoshirikisha wananchi katika masuala makuu yanayolikabili taifa.

Akiongea na kituo mojawapo cha televisheni hapa nchini, Mbatia alisema uzalendo katika nchi hii ulishapotea zamani na kubaki wachache wenye maamuzi serikalini kukumbatia mabepari.

Alisema pembezoni mwa nchi bado kuna wananchi wanakunywa maji yasiosafa, miundombinu mibovu, kula mlo mmoja na kufanya kuishi katika dimbwi la umasikini tofauti na miaka ya nyuma baada ya uhuru ambapo serikali ilikuwa ikijitoa kipaumbele kusaidia wananchi.

No comments: