ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 29, 2015

MJUE MAKONGORO NYERERE JITIRIRISHE HAPA CHINI


Moses Ng’wat, Mbeya

SIKU moja baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kusema kampeni za uchaguzi mkuu zitaanza Agosti 22, mwaka huu, Makongoro Nyerere ameonesha nia ya kuwania urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Makongoro ambaye ni mtoto wa mwasisi wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alitangaza nia yake hiyo jana mjini Mbeya.
Alisema wakati huu anajisikia yuko tayari kiafya, kiakili na ana nguvu ya kulitumikia taifa, hivyo atachukua fomu kugombea nafasi hiyo.
Makongoro ambaye mwaka 1995, alihamia upinzani kwa kujiunga na NCCR-Mageuzi na kufanikiwa kushinda Ubunge wa Jimbo la Arusha, alisema dhamira hiyo ataiweka wazi kwa kuzungumza na waandishi wa habari siku mbili au tatu kabla ya tarehe iliyopangwa na CCM kuanza kuchukua fomu.
Tayari makada kadhaa wa CCM wametangaza kuwania nafasi hiyo na wengine wakitajwa kuutaka urais.
Baadhi ya makada wanaotajwa kuutaka urais kupitia chama hicho ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, ambaye kwa sasa ni mbunge wa Monduli.
Wengine ni Bernard Membe, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Steven Wasira (Waziri wa Kilimo na Chakula), January Makamba (Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Wengine ni Dk. Hamis Kigwangalla, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha Rose Migiro, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.
CCM, ambayo imeshika nchi tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi, hujikuta katika wakati mgumu kila wakati inapotakiwa kutoa mgombea wa kurithi nafasi ya rais aliye madarakani baada ya kuongoza vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja.

Makongoro aliweka bayana nia yake hiyo wakati akipokea kwa niaba ya familia ya Baba wa Taifa, tuzo ya uongozi uliotukuka na uzalendo ambayo ilitolewa na Jukwaa la Wakristo Mkoa wa Mbeya kwa lengo la kutambua mchango wake kwa taifa.
Makongoro ambaye ni Kapteni msataafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) alisema; “Kwa kuwa kuna maneno yanapita na mimi nimeyasikia, na kwa kuwa nanyi mmenitaka niseme ninachoweza kuwaeleza hata mimi najisikia na niko tayari kulitumikia taifa katika nafasi hiyo (urais).

“Nimesikia CCM wametangaza ratiba ya kuchukua fomu, hivyo ninachoweza kuwathibitishia ni kwamba siku mbili au tatu kabla ya tarehe iliyopangwa na CCM kuanza kuchukua fomu nitazungumza na waandishi wa habari kuelezea uamuzi wangu kuhusu suala hilo,” alisema.
Kama Makongoro atagombea na kuibuka mshindi wa urais basi atakuwa ni mtoto wa pili wa mwasisi wa taifa kuongoza nchi, baada ya Amani Karume kuingoza Zanzibar.
Amani Karume ni motto wa mwasisi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Sheikh Abeid Aman Karume.

1 comment:

Anonymous said...

Uandishi gani huu? Kichwa cha habari hakiendani na kilichoandikwa:(