ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, May 10, 2015

Ngassa ajiunga Free State ya Afrika Kusini

Mshambuliaji wa Yanga akiwapungia mashabiki wa timu hiyo baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Azam juzi. Ngassa yuko njiani kutimkia Afrika Kusini kucheza soka la kulipwa. Picha na Anthony Siame.

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa amesaini mkataba wa miaka mitatu wa kuichezea klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini.
Ngassa alifanya majaribio katika klabu hiyo ya Afrika Kusini alipokuwa na kikosi cha Taifa Stars nchini Botswana katikati ya mwaka jana.
Katika majaribio yake Ngassa alifuzu na kufanyiwa vipimo vya afya, na klabu hiyo ya Afrika Kusini ilikuwa tayari kuilipa Yanga Dola 80,000, lakini klabu hiyo ya mtaa wa Jangwani ilikataa ikitaka ilipwe dola 150,000, lakini sasa anajiunga na Free State Stars kama mchezaji huru.
Chanzo cha karibu na mchezaji huyo, kimelithibitishia gazeti hili kuwa, Ngassa ameshamwaga wino kwenye timu hiyo na ataanza kuitumikia rasmi Julai.
“Ngassa ameshamalizana na wale jamaa wa Afrika Kusini na anatarajia kujiunga nao mwezi wa saba. Amesaini mkataba wa miaka mitatu utakaomalizika 2018,” chanzo hicho kilibainisha.
Juzi, baada ya kumalizika kwa mechi dhidi ya Azam, Ngassa alizunguka uwanja akiwapungia mikono mashabiki wa Yanga, huku akiwa amevalia jezi iliyokuwa imebeba ujumbe ‘I will always love you Yanga... Thanx... Bye!!’
Hivi karibuni kupitia ukurasa wake wa Instagram, Ngassa aliwaaga na kuwashukuru mashabiki wake na timu kwa ujumla katika kipindi chote walichokaa pamoja.
“Kwa heri Yanga, Nakupenda, Nashukuru kwa kila kitu” aliandika Ngassa kupitia kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Hiyo ni uthibitisho kwamba Ngassa sasa amedhamiria kuachana na klabu hiyo ya Mtaa wa Jangwani na anaondoka nchini kwenda kukipiga katika klabu ya Free State Stars.
Wakati huohuo; Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm amekerwa na kitendo cha mshambuliaji wake Simon Msuva kutimkia nchini Afrika Kusini bila kuuaga uongozi wa timu hiyo.
Kauli ya Pluijm imekuja siku moja baada ya uongozi wa Yanga kudai kuwa hauna taarifa zozote za Msuva kwenda nchini humo na inasemekana kuwa anafanya majaribio kwenye timu ya Orlando Pirates inayoshiriki Ligi Kuu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Pluijm alisema kuwa Msuva alipaswa kuomba ruhusa kwa uongozi wake kabla ya kuondoka, kitendo alichokifanya ni sawa na utovu wa nidhamu.
Alisema kuwa hadhani kama uongozi wa Yanga ungemkatalia Msuva kwenda kufanya majaribio hivyo hakutegemea kama mchezaji huyo angeweza kufikia hatua ya kuondoka kimyakimya.
“Msuva bado ni mchezaji wa Yanga na alitakiwa kuujulisha uongozi wake ili wampe baraka zao kabla ya kwenda huko. Mwanzoni alinifuata na kuniambia nia yake ya kwenda kufanya majaribio, nikamwambia kuwa anatakiwa kuujulisha uongozi kwanza, lakini hajafanya hivyo ila ameondoka bila kuaga jambo ambalo siyo jema,” alisema Pluijm.
Mwananchi

No comments: