Kocha wa Free State Stars ya huko Bondeni, Kinnah Phiri, amefichua sababu za kumsajili winga Mtanzania Mrisho Ngassa kwenye kikosi chake akisema anamtaka akafanye kazi ya ufungaji.
AMEZOELEKA kucheza nafasi ya winga hapa Tanzania, lakini ameandaliwa majukumu ya straika kule Afrika Kusini.
Kocha wa Free State Stars ya huko Bondeni, Kinnah Phiri, amefichua sababu za kumsajili winga Mtanzania Mrisho Ngassa kwenye kikosi chake akisema anamtaka akafanye kazi ya ufungaji.
“Nimeanza mipango ya msimu ujao na kwa kuanza nimemsajili Ngassa (Mrisho). Kikubwa ujio wake unakuja kutukomboa hasa kwenye ufungaji wa mabao.
“Awali tulikuwa na matatizo kwenye ufungaji na ilitokana na mastraika wetu kukosa umakini, lakini sasa ni wakati tumemsajili straika mahiri anayeweza kufunga mabao. Nitamtegemea sana Ngassa kwa sababu ninajua uwezo wake na ninajua atafanya kazi nzuri kama aliyokuwa akifanya akiwa na klabu ya Yanga.
“Pia kuna baadhi ya wachezaji wa Ligi Daraja la Kwanza watakaokuja kufanya majaribio kwa ajili ya kuwasajili na nafasi zinazotakiwa kujazwa ni ya kipa ambayo tunahitaji wawili, beki wa kulia na kushoto, winga mmoja na straika mmoja au wawili.”
Phiri aliongeza kusema: “Nafikiri tulikuwa na bahati mbaya kwenye michezo ya msimu huu. Kuna mara nyingi tumecheza vizuri lakini tulishindwa, hata hivyo nashukuru kuwa wachezaji wangu walipambana na tulifanikiwa kubaki, hivyo sasa nimepanga mikakati ya kuhakikisha timu inafanya vizuri msimu ujao.”
Kocha huyo aliteuliwa kuwa kocha wa Free State mwanzoni mwa msimu wa 2014/2015. Hivi sasa anajiandaa na msimu wa pili kwenye timu hiyo.

No comments:
Post a Comment