Advertisements

Tuesday, May 26, 2015

Niko tayari kupima afya - Lowassa.

Waziri Mkuu wa zamani ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.

Waziri Mkuu wa zamani ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, amesema kuwa kumekuwa na tabia ya watu kuombeana mabaya na mojawapo ni kuzushiana magonjwa na amependekeza kuwa wakati umefika kwa Chama Cha Mapinuzi (CCM) kupima afya za wagombea wake wa urais ili kujua ukweli nani mgonjwa.

Kadhalika, amesema kuwa yeye ni mzima wa afya na yuko tayari kwa chochote katika mchakato wa mapambano ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Lowassa aliyasema hayo jana nyumbani kwake mjini Dodoma alipokuwa anajibu maswali mbalimbali ya wahariri ambayo yalihusu mambo mbalimbali yanayomhusu, lakini siyo masuala ya sera na maono yake kuhusu uongozi wa nchi kwa kuwa hotuba yake anayoitarajia kuitoa Jumamosi ijayo mjini Arusha, ndiyo itaweka wazi maono yake kuhusu uongozi wa nchi.

“Leo hii hata nikikimbia kilomita 100 watasema Lowassa ni mgonjwa. Pale Dar es Salama nilifaya mazoezi na watu wale Albino km tano. Wakasema Lowassa amechoka sana amepata stroke amekimbizwa Ujerumani…. Huu ni uongo mtupu. Naomba tu kusema kuwa afya ni neema kutoka kwa Mungu,” alisisitiza na kuongeza:

“Twendeni tukapime afya zetu nami nitakuwa wa kwanza kupima tujue nani mgonjwa. Mengine nimewa-challenge kwenye speech yangu sitaki kuyasema hapa.”

RICHMOND
Akijibu swali kuhusu kadhia ya mkataba wa Richmond ambao ndio kiini cha kujiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu Februari mwaka 2008, Lowassa alisema jambo hilo linajulikana na limekwisha kuandikwa sana.

Hata hivyo, alisema kadhia hiyo ajenda haikuwa mkataba wa Richmond ila uwaziri mkuu.

Lowassa alisema awali alitaka kuvunja mkataba wa Richmond kama ambavyo alifanya kwenye mkataba wa City Water chini ya utawala wa Rais Benjamin Mkapa akiwa waziri wa maji na mifugo, serikali ikashitakiwa, lakini walishinda kesi kwa kuwa walifanya jambo kwa mujibu wa sheria na serikali ililipwa fedha nyingi.

Alisisiziza kuwa nia yake ilikuwa kuuvunja mkataba, serikali ilishirikishwa, lakini mamlaka ya kufikia uamuzi huo hayakuwa yake ingawa kila kitu kilikuwa kinajulikana wazi.

Lowassa alisema hakuna senti moja ya serikali ililipwa Richmond na kutaka aliyekuwa Waziri wa Fedha wakati huo, Zakia Meghji, aulizwe kama kuna senti ya serikali ililipwa Richmond.

Alikumbusha kuwa hata Rais Jakaya Kikwete alimweleza wazi aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati huo, Dk. Ibrahim Msabaha, kutokulipa Richmond fedha za umma kwa kuwa ilikuwa imeonekena kuwa haina uwezo wa kutekeleza mkataba wa kuzalisha umeme hadi kampuni hiyo itakapotekeleza kwa ukamilifu makubaliano yaliyokuwa kwenye mkataba husika.

Lowassa alisema kuwa aliwaita wataalam serikalini akiwamo Mwanasheria Mkuu wa serikali na kuwambia kwamba kuna habari zimeandikwa kwenye gazeti la The Guardian kwamba Richmond hawana uwezo wa fedha kutekeleza mkataba wake.
“Niliwaambia be careful. Nikaweka kwenye maandishi kwa Mwanasheria mkuu. Kwa wale makatibu wakuu kulikuwa na timu ya serikali ya kujadili chini ya Katibu Mkuu wa nafikiri Gray (Mgonja)… maamuzi yalichukuliwa na mnajua yaliyotokea,” alisema.

Aliwataka wananchi kujifunza kutokana na yaliyotokea kwa Richmond kwamba wakubwa wawili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hilary Clinton na Rais Barack Obama wa Marekani walifika Tanzania na kuihakikishia serikali kwamba mitambo ya Richmond/Dowans ilikuwa ni mizuri na salama na yenye uwezo wa kuzalisha umeme.

Alikumbusha kuwa kama isingelikuwa ni ubishi wa kisiasa jinsi suala la Richmond lilivyoshughulikiwa, leo Tanzania isingekuwa kwenye wakati mgumu kama ilivyo sasa kwani umeigharimu nchi Sh. bilioni 120 baada ya kushindwa kesi katika mahakama ya usuluhishi wa biashara huko Paris, Ufaransa.

AKUBALIANA NA MBOWE
Alisema suala la serikali kuingia katika madeni hayo pia liliibuliwa bungeni na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, kwamba serikali imeshindwa kesi kule Ufaransa ambayo iliamua na majaji Wazungu na sasa itatakiwa kulipa Dowans Sh. bilioni 120 kwa sababu tu ya ubishi wa kisiasa.

Akiwasilisha hotuba ya Kambi ya Upinzani Bungeni Mei 12, mwaka huu aliitaka serikali isimame na isema sasa ni nani walihusika katika kadhia ya Richmond ambayo ni matokeo ya minyukano ya kisiasa ndani ya CCM ambayo sasa yameliingiza taifa katika hasara ya Sh. bilioni 120 baada ya kushindwa kesi huko Ufaransa.

Mbowe alisema katika mlolongo wa kushindwa kusimamia nchi, kuendekeza makundi na vita vya kisiasa ndani ya CCM na serikali yake kwa gharama ya Taifa, sasa linadaiwa Sh. bilioni 120 baada ya kushindwa kwenye kesi ya Dowans/Richmond katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC) huko Paris.

“Serikali haijataka kuliweka jambo hili wazi na ni dhahiri kuna siri kubwa inayosababisha jambo hili kuwa la usiri mkubwa.

Huko mbele ya safari jambo hili litaligharimu Taifa mabilioni haya ya fedha ambayo yangeweza kuepukika kama ukweli, uwazi na haki vingetawala mchakato mzima wa kashfa ya Richmond. Serikali isimame sasa na ilieleze Taifa ni nani anasema kweli, ni nani alilidanganya Bunge na ni nani analindwa na serikali katika kashfa hii?” alisema Mbowe.

UTAJIRI WAKE
Akizungumzia madai kwamba ana utajiri mkubwa, Lowassa alisema ana ng’ombe kati ya 800 na 1,000 na nyumba chache. Ila kama kuna mwenye kutaka kujua kila anachomiliki taarifa hizo zipo kwenye fomu yake ya kutangaza mali na madeni inayowasilishwa kwa Tume Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Hata hivyo, alisema: “Ninauchukia sana umasikini, ninapenda utajiri. Napenda Watanzania wachukie umasikini. Ninautafuta uongozi wa nchi hii ili kuwasaidia wananchi kuachana na umasikini siyo kuukumbatia,” alisema.

Alitoa angalizo kuwa anatamani nchi hii iwe na watu wenye uwezo wengi kama Reginald Mengi (Mwenyekiti Mtendaji wa IPP), Said Bakhressa (Mmiliki wa AZAM), Nazir Karamagi, ili kusaidia kuondoa umasikini nchini.

Alisisitiza kuwa hana tatizo lolote na utajiri ambao umepatikana kwa njia halali, ingawa kuna watu wanawaonea wenzao wivu kwamba wamefanikiwa wakati wao walipata fursa, lakini kazi yao ni kuendekeza ulevi na wanawake.

Alitaka wanasiasa waache kuwadanganya watu kwamba umasikini ni kitu kizuri.

Akizungumzia madai kwamba amekuwa anatoa fedha nyingi katika harambee mbalimbali anazoendesha nchini, Lowassa alisema kwamba hana fedha ila ana marafiki.

Alisisitiza fedha zinazopatikana katika harambee zinachangwa na marafiki wake mbalimbali na yeye kazi yake ni kuongoza harambee hizo ambazo kwa maoni yake zimesaidia sana maendeleo katika jamii. Aliwashauri wabunge wainge mfao huo kwa kufanya harambee mbalimbali vijijini ili kusiadia kuchangia maendeleo ya jamii. Alikumbusha kuwa shule za kata zilijengwa kwa harambee.

ELIMU
Lowassa alisema elimu ya Tanzania imevurugwa sana na juhudi kubwa ni lazima zichukuliwe kurekebisha hali hiyo. Aliitaja elimu kuwa ndiyo mkombozi wa matatizo mengine makubwa ya taifa kama ukosefu wa ajira kwa vijana.

Alisisitiza msimamo wake kuwa sera inapashwa kuwa elimu kwanza na siyo kilimo kwanza, kwa kuwa ni kupitia elimu kilimo kinaweza kuboreshwa na kuleta tija.
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

pima baba jicho la kushota halioni vizuri sijui nao watakao kupima utakuwa umeshawapa rushwa.hivi why unanganania kuwa raisi? baba wa taifa nyerere alishakukataa.

Anonymous said...

Lowassa amejiuzulu uwaziri mkuu mwanzoni mwa 2008. Obama na Hillary wameanza Kazi WH 2009, mwaka mmoja baadae. Hizo baraka zao alizipata lini? Vile vile, BO na HRC siyo wahandisi, mambo ya mitambo wanayajulia wapi? This man, Lowassa has a lot more to explain to the Tanzanian ppl.