Advertisements

Sunday, May 10, 2015

Vigogo wawili jela kwa ubadhirifu wa Sh 13,395,800.

MAHAKAMA ya Wilaya ya Nachingwea mbele ya Hakimu Mfawidhi Joseph Hemela, imewatia hatiani washtakiwa wote wawili katika kesi ya ufujaji na ubadhirifu wa Sh 13,395,800 za wanachama wa Chama cha Ushirika cha Naipanga katika kesi namba CC 66/2013 iliyofunguliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mwaka 2013.
Hukumu hiyo inahusisha ununuzi hewa wa korosho katika msimu wa mwaka 2010/2011 dhidi ya washtakiwa hao waliokuwa watia saini benki katika akaunti ya biashara ya Naipanga AMCOS ambao ni Mhasibu Mkuu, Mustafa Kantelu na Mwenyekiti wa Naipanga AMCOS, Salum Tewa.
Washtakiwa walitiwa hatiani kwa kosa la kula njama kutenda uovu kinyume na kifungu cha 32 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCA) namba 11/2007 na Hakimu Hemela ameagiza walipe faini ya Sh 500,000 kwa kila mshtakiwa na wakishindwa wataenda kutumikia kifungo miezi 24 jela.
Kosa la pili ni ufujaji na ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28 cha PCCA namba 11/2007 na Hemela ameagiza kulipa faini ya Sh 600,000 kwa kila mshtakiwa na wakishindwa wataenda kutumikia kifungo miezi 24 jela.
Kosa la mwisho, Hemela amewaagiza washtakiwa kurejesha fedha kiasi cha Sh 13,395,800 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tangu tarehe ya hukumu na wakishindwa watapelekwa jela kutumikia kifungo cha miezi 24 na wakimaliza kifungo jela watatakiwa kuzirejesha.
Washtakiwa wote walishindwa kutekeleza hukumu ya kulipa faini na wamepelekwa jela kuanza kutumikia adhabu zao

No comments: