
Waziri mkuu Mstaafu Fedrick Sumaye.
Mbeya. Kazi ya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ya kusaka wadhamini juzi nusura iingie dosari baada ya wanachama kutaka kuchana fomu zenye orodha ya wadhamini kwa madai kuwa hawakupewa “nauli” ya kwenda ofisi za CCM kufanya kazi hiyo.
Wakati tafrani hiyo ikitokea mjini Mbeya, Balozi Amina Salum Ali alisema mjini Tanga kuwa hajawahi kuona nchi ambayo mtu anaiba fedha, halafu anaambiwa azirejeshe bila ya kuchukuliwa hatua zozote, akisema huo ni udhaifu mkubwa katika kudhibiti ufisadi.
Katika sakata la Mbeya, kundi la baadhi ya wanachama kutoka kata nne waliokabidhi kadi na kuandikwa majina yao kwenye ofisi za CCM za Wilaya ya Mbeya Mjini, liliambiwa kuwa hakukuwapo na posho kwa ajili ya kazi hiyo.
Kauli hiyo ilisababisha wanachama hao kupora na kutaka kuchana fomu iliyokuwa na majina yao.
Katibu wa CCM wilaya hiyo, Kulwa Milonge alisema tukio hilo lilikuwa kubwa na kuhatarisha usalama, lakini chama kiliingilia kati na kusawazisha mambo.
Milonge alisema hadi mwisho wa tukio hilo, ofisa aliyetumwa na Sumaye kukusanya saini hizo aliondoka na majina 45 ya wadhamini.
Sumaye ni mmoja kati ya wanachama wengi waliojinadi kuwa wanachukia rushwa na ameeleza bayana kuwa iwapo CCM itampitisha mlarushwa, atajiondoa.
Balozi Amina aikomalia rushwa
Mkoani Tanga, Balozi Amina alisema kwa kutumia uzoefu wake kimataifa katika masuala ya fedha, amebaini kuwa kuna tatizo la kushindwa kudhibiti ufisadi uliokithiri nchini.
“Sijapata kusikia nchi yoyote duniani mtu anapatikana na hatia ya kufanya ubadhilifu mkubwa wa fedha za umma, halafu anaambiwa tu arejeshe na hakuna hatua anazochukuliwa,” alisema Balozi Amina.
Alisema iwapo atapewa fursa ya kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, atatumia nguvu kubwa kupambana na ufisadi unaorutubishwa na tabia ya kulindana kwa sababu hata kama kutakuwa na uzalishaji mkubwa, kama kuna mifereji ya rushwa, uchumi hauwezi kukua.
Alisema Tanga ina uwezo wa kubadilika na kuwa kitovu cha uchumi wa Tanzania nzima iwapo Bandari ya Tanga itaboreshwa kwa kujengwa ya Mwambani na reli ya Tanga-Arusha-Musoma hadi Uganda.
Wingi wamtisha Pinda
Wakati mwakilishi wa Sumaye akipata matatizo hayo, hali ilikuwa tofauti kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye alikuwa ofisi ya CCM ya Mbeya Vijijini kusaka wadhamini.
Waziri Pinda alisema mbele ya wanachama waliojitokeza kumdhamini kuwa mwili wake unasisimka na kujaa hofu kwa jinsi wanachama wengi wanavyozidi kujitokeza kuomba urais. Alisema anatishwa zaidi na mitazamo ya baadhi ya wagombea ambao wanaonekana kuitaka dhamana hiyo kwa nguvu zote.
Lakini akasema anatiwa nguvu na idadi kubwa ya wanachama wanaomuunga mkono na kwamba anazidi kusonga mbele akimtumaini Mungu kwamba akipenda atafanikiwa.
“Nawaomba mtuombee wote tuliojitokeza kusaka urais ili apatikane mmoja ambaye itabidi aungwe mkono na wengine wote,” alisema.
Alisema wapo baadhi ya wagombea ambao wanaonekana kana kwamba hawatakubali matokeo watapokataliwa na jambo hilo linaweza kuleta mtikisiko ndani ya chama.
Lowassa adhaminiwa na maelfu
Mkoani Mtwara, zaidi ya wanachama 3,500 walijitokeza katika ofisi za chama hicho za wilaya kwa ajili ya kumdhamini Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
“Mapokezi ya leo ni historia kubwa kwangu na CCM, nawashukuru sana kwa sababu tangu nije Mtwara hii haijawahi kutokea na imani huzaa imani. Hapa mmenipa Imani,” alisema Lowassa.
Alieleza sababu za kugombea akisema: “nimechoshwa na umaskini, lazima tufanye maarifa kwa uwepo wawekezaji kutoka nje.”
“Msiichezee bahati ya gesi, uwepo wa kiwanda cha saruji, mbolea na vinginevyo vitakavyokuja, vyote vimeshuka kwa bakuli la neema na neema hii itaendelea kuwapo kama amani itaendelea kuwapo,” alisema.
Habari hii imeandikwa na Sadi Makomba, Silyvester Mkombe, Burhani Yakub, Justa Mussa, Godfrey Kahango na Haika Kimaro.
MWANANCHI
1 comment:
System ya Politics Tofauti
Marakekani: Wanachama wa chama au wafuazi wa kiongzi ndiyo wao wanachingia ili kiongozi huyo apite ugombea wa uchanguzi.
Tanzania. Kiongozi mgombea ndiye anayelipa wanachanma au wafuazi wake ili afanikiwe kupata nafasi anayoigombea.
Kiongizi wa Tanzania ambaye amezaliwa kwenye umaskini atapata wapi pesa nyingi hizo bila kulazimishwa kutumia mali ya uma na kuwapa uma kwa sababau ya kutumikia uma.
Post a Comment