ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 3, 2015

HUDUMA YA GOOD NEWS FOR ALL MINISTRY YAOMBA KUWEPO MJADALA WA WAZI KUJADILI TATIZO LA ULEVI NCHINI

 Askofu Charles Gadi wa Huduma ya Good News for All Ministry 
  Askofu Charles Gadi wa Huduma ya Good News for All Ministry (kulia), akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu kuongezeka kwa joto duniani na athari zake pamoja na tatizo la ulevi nchini ambapo kanisa hilo limeshauri kuwepo na mjadala wa wazi kujadili jambo hilo. Kutoka kushoto ni Mchungaji, Martin Ndaki na Katibu wa huduma hiyo, Palemo Massawe.
 Mchungaji Fabian Msimbe akizungumza katika mkutano huo. Kulia ni Mchungaji Leons Kajuna.
 Mchungaji Martin Ndaki (kushoto), akizungumza katika mkutano huo.
 Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
 Askofu Charles Gadi wa Huduma ya Good News for All Ministry (katikati), akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu kuongezeka kwa joto duniani na athari zake pamoja na tatizo la ulevi nchini ambapo kanisa hilo limeshauri kuwepo na mjadala wa wazi kujadili jambo hilo. Kutoka kushoto ni Mchungaji Martin Ndaki, Katibu wa huduma hiyo, Palemo Massawe, Mchungaji Fabian Msimbe, Mchungaji Leons Kajuna, Mchungaji Denis Kumbiiho na Mchungaji James Manyama.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
.........................................................................................
Taarifa kwa Umma

KUONGEZEKA KWA JOTO DUNIANI NA ATHARI ZAKE KWA NCHI ZETU NA HIVI KARIBUNI NCHI YA INDIA.

Ndugu waandishi wa habari, nawasalimu katika jina la Yesu. Kwanza nawashukuru kwa kufika kwenu kuja kunisikiliza. Jina langu ni Askofu Charles Gadi wa huduma ya Good News for All Ministry.

Ndugu waandishi wa habari napenda kuchukua nafasi hii kuzungumzia hali ya joto la la dunia. Tunashukuru Mungu kwa nchi yetu kupata mvua nyingi mwaka huu, ingawa baadhi yetu zilituathiri kwa njia moja ama nyingine kutokana na mafuriko. Lakini tunapaswa kujua kuwa hali ya joto la dunia kwa ujumla siyo nzuri hasa ukichukulia taarifa za mara kwa mara za kupungua kwa barafu ya mlima Kilimanjaro na kuyeyuka kwa mabonge ya barafu katika mabara ya barafu ya Actic na Antarctica. Taarifa hizo za kisayansi zinaonyesha kuwa ongezeko hilo la joto linatokana na uharibifu wa mazingira na kuongezeka kwa hewa ya ukaa (CO2  CARBON DAIOKSIDE).

Upungufu wa misitu ambayo husaidia kunyonya hewa ya ukaa inayotumiwa na miti kutengeneza chakula yaani phososynthesis na utumiaji wa madawa mbali mbali yanayoharibu mazingira pia huchangia ongezeko hilo la Joto. Sote ni mashuhuda wa jinsi misitu yetu inavyoendelea kuangamia kutokana na shughuli za kibinadamu.

Ndugu waandishi wa Habari, Hivi karibuni imeripotiwa kuwa wimbi kubwa la upepo wa Joto (heat wave) limeikumba limeikumba nchi ya India na kuua zaidi ya watu 2000 na bado wengine wanaendelea kupoteza maisha yao. Hiyo si habari njema kwetu sisi tunaokaa duniani kwani jambo kama hilo linaweza kutufika sisi wakati wowote maana hatuna kinga yoyote inayotuzuia na ongezeko hilo la joto Duniani.  Cha kusikitisha ni kuwa waliokufa wengi ni wazee, maskini na watoto ambao hawana uwezo wa kujikinga na wimbi hilo la joto kwani unahitaji uwe na viyoyozi (air conditioning) au maji baridi ya kujinyunyuzia wakati wimbi hilo la joto likipita.

Kwa sababu hiyo tumesukumwa na Mungu kuandaa mkutano wa maombi huko India ili Mungu atukinge na madhila hayo ya mawimbi ya hewa ya joto. Katika safari hiyo ya India tutaambatana na wachungaji zaidi ya 10 pamoja na waandishi wa Habari kadhaa  ili kufanya maombi hayo, yatakayoambatana na kutoa misaada kwa waathirika wa upepo joto huo. Ni muhimu kwetu kutoa misaada kwa sababu wale walioathirika ni maskini na wahitaji wa nchi ile na Biblia inasema kuwa unapomsaidia Maskini unamkopesha Bwana. Ina maana Mungu anaweza kutumia sadaka hiyo kutuepusha na sisi kupata tatizo linalofanana na hilo katika nchi yetu.

Ili kufanikisha safari hiyo, tunawaomba wananchi wote wenye moyo kutuchangia nauli na msaada wa kuwapelekea waathirika hao. Tunaiomba jamii ya kiasia katika nchi yetu kusaidia katika hilo, na hata taasisi mbali mbali za fedha na mashirika yasiyo ya kiserikali. Safari hiyo ni ya uhamasisho na itahusisha pia kushauri au kuelimisha dhana nzima ya utunzaji wa mazingira hasa misitu na kupunguza hewa ya ukaa inayochochea ongezeko hilo la joto duniani.


TATIZO LA ULEVI KWA TAIFA

Ndugu waandishi wa habari, Kuna habari kwenye vyombo mbali mbali vya habari na mitandao ya kijamii, na hata Bungeni jambo hilo limetajwa kwamba vijana wetu na wanandoa wengi wameathirika sana kwa ulevi wa kupindukia utokanao na matumizi ya pombe za kienyeji zenye vilevi vikali. Eneo la Rombo limetajwa kwa taarifa iliyotolewa na mkuu wa Wilaya hiyo na kushuhudiwa pamoja na baadhi ya  akina mama waliohojiwa na vyombo vya habari  kuwa limeathirika sana. Lakini napenda kuwaambia kuwa wilaya hiyo ni mfano tu, hilo nitatizo la kitaifa kwani tunaona mara nyingi katika vijiji, miji na mikoa watu walivyoathirika na ulevi, hadi kushindwa kutimiza majukumu yao ya kulijenga taifa hilli. Pamoja na kuwepo kwa habari ya aibu kuwa baadhi ya wanawake wanakodisha wanaume toka nchi jirani ya Kenya, lakini kinachotakiwa kuangaliwa hapa ni hali halisi ya kuathirika kwa  wananchi wetu.

Sisi tunatoa ushauri kuwa uwepo mjadala wa wazi juu ya tatizo hilo la ulevi badala ya kutumia nguvu nyingi kumkemea Mkuu wa wilaya aliyejaribu kutumia nguvu zake kukomesha unywaji huo mbaya wa pombe. Inasemekana kuwa ndani ya wilaya hiyo kuna aina za pombe za kienyeji zaidi ya 50 na nyingi huwekwa kweye chupa maalum kama zile za kiwandani huku zikiwa hazina viwango vya TBS. Baadhi yake zina kilevi (Alkohol) zaidi ya asilimia 58% jambo ambalo ni hatari kubwa kwa maini na figo za wanywaji. Uwezekano wa kupuguza nguvu za kiume upo kwani wengi huamka asubuhi na mapema kunywa vilevi hivyo na hivyo kushindia bila kula jambo ambalo linawathoofisha kimaumbile.

Hivi karibuni dada mmoja mwanasheria alitufuata na kutaka tuombe sana kwa ajili ya tatizo la ulevi katika taifa  kwa wanaume kwani amefanya utafiti katika kazi yake na kugundua kuwa kwenye ndoa nyingi wanaume hawana nguvu za kiume baada ya kuzoelea ulevi na wamama wengi wanalalamika. Hii inaonyesha kwamba hili si tatizo la wilaya moja tu, bali ni la kitaifa, na tunashauri lichukuliwe kwa uzito na kuwekewa mjadala mpana zaidi  wa kitaifa ili ufumbuzi upatikane. Tunamwomba waziri mkuu aliundie tume ili hatua za haraka na  za kimakusudi ziweze kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na za kiroho, kwa kushirikisha wadau mbali mbali ikiwa ni pamoja na serikali, vyombo vya sheria, vyombo vya kiroho (viongozi wa dini) kutafuta usuluhishi.

Sisi tunaona kuwa ni tatizo la kiroho kwani upo msemo kuwa ulevi unachangia uzinzi, lakini kinyume chake sasa inaharibu nguvu za kiume. Ukisoma Kumbukumbu la Torati 28:30  katika Biblia inasema, “Utaoa mke na mume mwingine atalala naye . . . .” Andiko hilo linamaanisha mtu aliyelaaniwa. Kama mtu akishindwa kulala na mkewe amelaaniwa.

 Maana ikiwa kwa sababu ya pombe wanawake wa Rombo wanaazima wanaume Kenya, basi na wa Mtwara wataazima Msumbiji na wa Kagera na Kigoma wataazima Burundi Rwanda na uganda. Sasa ikiwa ulevi huo uko nchi nzima, wale walio mikoa ya kati wataazima wapi? Napenda muone kuwa tatizo hili litafika pabaya kama halijachukuliwa hatua stahiki.

Kutokana na hali hiyo tunashauri itafutwe namna ya kuwashauri wananchi na vijana kwa ujumla nchi nzima namna ya kuepukana na ulevi huo, na pia sisi kama viongozi wa dini kushirikiana kuwaelimisha kwa kanuni za kiroho na kimwili, kwani bahati nzuri madhehebu mengi ya dini hukemea utumiaji wa pombe. Pia watengenezaji wa  vilevi hivyo washauriwe kutafuta miradi mingine ya kuwaingizia kipato badala kutegemea pombe hizo  zinazoumiza vijana wetu.

Sasa tatizo la pombe hizo za viroba na kienyeji ni tatizo kubwa kwa vijana wa primary, secondary, waendesha bodaboda, madereva wa noa, bajaji nk hata kupunguza kiwango cha elimu, ajali za mara kwa mara, na nguvu kazi ya nchi kwa ujumla. Hili tatizo ni kubwa mno na linalenga kuharibu (generation) au kizazi hiki cha vijana na kutengeneza jamii ambayo haitafundishika au kutawalika kwa urahisi.

Tunawashukuru sana kwa kutusikiliza.

Wako Charles Gadi Mwenyekiti: GOOD NEWS FOR ALL MINISTRY. (Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com)

No comments: