ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, June 21, 2015

Klabu ruksa kusajili wageni saba

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania Jamal Malinzi.

Dar es Salaam. Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) limekubaliana na ombi la klabu za Ligi Kuu la kusajili wachezaji saba wa kigeni badala ya watano wa sasa.
Bodi ya Ligi iliwasilisha uamuzi wa klabu zote za Ligi Kuu wa kuiomba TFF ibadilishe kanuni ili ziweze kusajili wachezaji wengi zaidi wa kigeni kwa lengo la kuinua kiwango cha ligi hiyo.
Jana, katibu mkuu wa TFF, Celestine Mwesiga alisema kikao hicho cha shirikisho hilo na sasa klabu zinaweza kusajili wachezaji zaidi wa kigeni.
Klabu hizo zimekuwa zikijikuta kwenye wakati mgumu kuamua kukata jina la mchezaji wakati zinapokuwa na wachezaji wengi wazuri kutoka nje, ikiwamo Yanga ambayo hadi sasa ina wachezaji sita wageni na ilikuwa ikisubiri uamuzi huo ili ikamilishe usajili wa wachezaji wageni.
Wakati hayo yakiendelea, Yanga imemruhusu kipa wake Juma Kaseja kusajiliwa na klabu yoyote inayomhitaji.
Mwanasheria wa Yanga, Frank Chacha aliliambia gazeti hili jana kuwa Yanga haiwezi kumzuia kipa huyo kujiunga na klabu nyingine yoyote kwa kuwa tayari ilishavunja mkataba wake, hivyo siyo mwajiriwa tena wa klabu hiyo yenye makao yake makuu makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani.
Timu mbalimbali za Ligi Kuu zilielezwa kuwa zimekuwa zikihitaji huduma ya kipa huyo aliyejipatia sifa kwa umahiri langoni, kiasi cha kujipatia jina la Tanzania One, lakini zilikuwa zikihofia kesi yake ya kimkataba dhidi ya Yanga iliyopo Tume ya Usuluhishi ya Mahakama ya Kazi.
Kaseja alisaini Yanga mkataba wa miaka miwili na alitumikia mwaka mmoja na kubakisha mkataba wa mwaka mmoja uliozua mgogoro.
Chacha alisema anashangazwa na watu wanaodaia kuwa klabu hiyo imemzuia Kaseja kujiunga na timu yoyote wakati si kweli.
“Sisi hatumzuii Kaseja kujiunga na timu yoyote na hata mwanasheria wake tulimwambia hivyo kuwa anaweza kutafuta timu wakati kesi yake inaendelea.
“Ndiyo ana kesi na Yanga, lakini kumbuka yeye ndiye alivunja mkataba na Yanga ikamshtaki hivyo haitapendeza kuwa hukumu inatoka halafu Kaseja hana timu yoyote inayomwingizia kipato, atailipa nini Yanga.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu jambo hilo, Kaseja alijibu kuwa hawezi kulizungumzia kwa sasa.
Siwezi kusema lolote bila mwanasheria wangu ambaye yuko nje ya nchi, subirini arudi tutakuwa na jambo la kusema,” alijibu Kaseja.
Timu hiyo ilimshtaki Kaseja kwa kuvunja mkataba na Yanga tangu Novemba 11, 2014 ambapo aliindikia barua klabu hiyo akiomba kuvunja nayo mkataba kwa madai ya kutokulipwa Sh20 milioni za usajili, hana bima na hapangwi kucheza mechi za mashindano.
Yanga ilichukua uamuzi wa kumfungulia kesi Mahakama ya Kazi na kumdai fidia ya Sh300 milioni, kurudisha fedha zote za usajili Sh40 milioni, pia kuilipa klabu hiyo mshahara wake Sh2.2 milioni kwa miezi 12 iliyobaki kuitumikia timu hiyo.
Kesi hiyo ilifikishwa kwenye Mahakama ya Kazi, Tume ya Usuluhishi na majaji wanaosikiliza kesi hiyo waliwapa muda Kaseja na uongozi wa Yanga kumaliza suala lao nje ya mahakama.
MWANANCHI

No comments: