Advertisements

Tuesday, June 23, 2015

MAKAMU WA KWANZA WA RAIS, MAALIM SEIF AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA UFARANSA NCHINI

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na balozi wa Ufaransa nchini Tanzania bibi Malika Berak, alipofika ofisini kwake Migombani kwa mazungumzo. Kulia ni ofisa wa ubalozi Philippe Boncour.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akisisitiza jambo wakati akizungumza na balozi wa Ufaransa nchini Tanzania bibi Malika Berak, ofisini kwake Migombani.

Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania bibi Malika Berak, akisisitiza jambo wakati akizungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ofisini kwake Migombani (Picha na Salmin Said, OMKR)


  Na: Hassan Hamad (OMKR)
 


Ufaransa inakusudia kukuza mahusiano yake ya kiuchumi na Zanzibar kwa kuyashajiisha makampuni ya nchi hiyo kuja kuwekeza miradi yake hapa nchini.
 


Hayo yameelezwa na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania bibi Malika Berak, alipofanya mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad ofisini Migombani.
 


Amesema nchi hiyo ina nia ya dhati ya kuendeleza uhusiano wake na Zanzibar katika nyanja mbali mbali ikiwemo ya kiuchumi, na kwamba itachukua juhudi za makusudi kuyashawishi makampuni ya nchi hiyo kuja Zanzibar ili kuendeleza uhusiano huo.
 


Balozi Malika ametaja baadhi ya maeneo ambayo makampuni hayo yanaweza kuwekeza kuwa ni pamoja na utalii pamoja na uvuvi wa bahari kuu.
 


Aidha amesema anafarajika kuona kuwa vijana wa Zanzibar wanajifunza lugha ya Kifaransa, hatua ambayo inasaidia kujua utamaduni wa nchi hiyo na kuendeleza uhusiano katika nyanja ya utamaduni.
 


Kwa upande wake Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad ameelezea kufurahishwa na hatua hiyo ya Ufaransa, na kwamba Serikali itashirikiana nayo katika kuhakikisha kuwa malengo hayo yanafikiwa.
 


Amefahamisha kuwa Serikali imekuwa ikiwashajiisha wawekezaji kuja kuwekeza miradi yao ya Kiuchumi hapa nchini, na tayari imeshaweka mazinigira mazuri ya uwekezaji kwa kuimarisha miundombinu yake.
 


Amesema Zanzibar imekuwa ikitekeleza mpango wake wa kushirikiana na taasisi binafsi katika kukuza uchumi wake (PPP), na kuzialika kampuni hizo za Ufaransa kuja kuwekeza miradi yao bila ya hofu yoyote.
 

Maalim Seif amesema Zanzibar inajivunia amani iliyopo nchini, na kuahidi kuwa itazidi kuendelezwa na kulindwa, ili kuhakikisha wawekezaji na wageni wanakuwa katika mazingira ya usalama wakati wote.



Amefafanua kuwa Zanzibar inayo maeneo mengi ya uwekezaji hasa katika sekta za Utalii, Uvuvi na Kilimo, na kuyashauri makampuni hayo kufanya utafiti wa kina ili kujua maeneo waliyovutika nayo kwa uwekezaji.
 

Ameeleza kuwa Zanzibar imekuwa ikihamasisha utalii wa hadhi ya juu, na tayari yapo mahoteli makubwa yanayoendana na hadhi hiyo, sambamba na kuwepo vivutio vingi vya utalii ikiwa ni pamoja fukwe, misitu ya asili na utamaduni. 

Akizungumzia kuhusu maendeleo ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, amesema imeleta mafanikio makubwa hasa katika kuwaunganisha na kuwaleta pamoja wananchi ambao kwa kipindi kirefu walikuwa wakihasimiana.


No comments: