Mark Mwandosya (Kushoto) na Edward Lowassa (Kulia)
Dodoma. Profesa Mark Mwandosya, ambaye anawania kuteuliwa na CCM kugombea urais, amemtaka Edward Lowassa kujiunga na kambi yake kwa kuwa makada wengine wanne kwenye mbio hizo wanamuunga mkono.
Hata hivyo, wawili kati ya makada hao wanne wamekana kumuunga mkono.
Mwandosya, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), alisema tayari Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Steven Wasira, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta na waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe wanamuunga mkono na hivyo kumshauri Lowassa kujiunga na kambi yake.
“Kama (wagombea) wengi wananiunga mkono, aliyebakia basi atakuwa ni ndugu yangu, rafiki yangu, Edward Lowassa. Naye angesema hivyo ingerahisisha sana kazi ya chama, ingepunguza sana kazi, makundi yangekuwa yameisha,” alisema Mwandosya baada ya kurejesha fomu za kuomba CCM impitishe kugombea urais.
“Halmashauri Kuu isingepata shida, Kamati Kuu isingepata shida nadhani tungeweza kufika pale ambako tungefika tarehe 12 (Julai, siku ambayo Mkutano Mkuu wa CCM utamchagua mgombea urais), bila kikwazo, bila makundi,”alisema mbunge huyo wa Rungwe Mashariki jana.
Lakini kauli yake imepokewa kwa hisia tofauti na watu hao aliodai wanamuunga mkono, huku kambi ya Lowassa ikizungumzia kauli hiyo kuwa si ya mtu aliye makini kwenye mbio za urais.
Jumla ya makada 40 wamechukua fomu za kuomba ridhaa ya CCM kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25 na chama hicho kina kazi ngumu ya kumpata mwanachama atakayemrithi Rais wa sasa, Jakaya Kikwete ambaye katiba inamzuia kuendelee kuongoza baada ya kumaliza vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja.
Mgombea urais wa CCM pia ndio atakuwa mwenyekiti wa chama hicho.
Akizungumza mara baada ya kurudisha fomu jana, Profesa Mwandosya alisema mchakato huo umewafanya wanaoomba urais kuwa marafiki zaidi licha ya kupigana vijembe, akisema ingekuwa nchi nyingine wangefanyiana vurugu.
Aliwashukuru wagombea wenzake waliotamka hadharani kuwa watamuunga mkono endapo hawatapitishwa na Kamati Kuu ya CCM kugombea urais.
“Namshukuru Benard Membe ambaye ametangaza na kuandikwa (kwenye vyombo vya habari) kwamba yeye ameona katika orodha yote ya watu 40, kama si yeye basi ataniunga mkono mimi na yupo tayari kuzunguka nchi nzima iwapo chama kitaniteua kuwa mgombea,” alisema Profesa Mwandosya.
“Namshukuru pia Mheshimiwa Pinda, amelizungumzia hili katika vituo kama si kimoja viwili kuwa moyo wake utakuwa na furaha kama Profesa Mwandosya anaweza kuteuliwa na chama.”
Alisema pia kuna baadhi ya wagombea wenzake waliochukua fomu wamesema kwa kupitia mameneja wao wa kampeni kuwa nao wanafikiria kumuunga mkono Mwandosya na kwamba jambo hilo limempa faraja kubwa.
“Baadhi ya mameneja wa rafiki yangu sana Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira ni kati ya wale ambao wamesema, lakini hawajasema hadharani sasa sijui kama ninatoa siri au,” alisema Mwandosya ambaye alijitokeza mwaka 2005 kuomba ridhaa ya CCM na kushika nafasi ya tatu.
“Na sidhani kwamba Mheshimiwa Sitta atakataa... hataniunga mkono. Kama nikiteuliwa basi ni kundi kubwa. Hilo linatosha kabisa kunivusha, lakini yote haya tutategemea vikao na maamuzi ya chama.”
Alisema hayo ndiyo matarajio yake na bila shaka ni ya Watanzania wote.
“Mimi nimuogope nani tena? Mimi namuogopa Mwenyezi Mungu. Si kumuogopa tu bali ni kumnyenyekea na kumshukuru kwa yote,”alisema Profesa Mwandosya.
Bashe anena
Lakini kauli hiyo haikuwa nzuri kwenye kambi ya Lowassa.
Mjumbe wa kamati yake ya kampeni, Hussein Bashe alimtaka Prof Mwandosya atatafakari mara mbili wito wake.
Bashe alisema anafahamu kuwa waliotangaza kumuunga mkono (Profesa Mwandosya) sio wagombea urais kwa sababu nia yao si kuongoza nchi wala chama chao cha CCM.
Alisema Membe alitangaza kumuunga Profesa Mwandosya, akiwa mkoani Mbeya na akafanya hivyo tena mkoni Mara, lakini alimuunga mkono Makongoro Nyerere, ambaye pia anawania kuteuliwa na CCM kugombea urais.
“Mwandosya anafahamu katika uchaguzi wa mwaka huu kuna wagombea urais, wagombea vikoba, wachekeshaji na watu makini wenye nia thabiti ya kuongoza nchi na chama chetu,” alisema bashe.
“Vikoba ndio hao wagombea wanaotoa kauli ya kuunga mkono wenzao ili baadaye wakaungane kwenye saccos (vyama vya kuweka na kukopa), ambako huko pia wamo walevi wote wamechukuwa fomu za kutaka kuongoza chama chetu na nchi.”
Bashe alisema Lowassa amechukua fomu kwa ajili ya kuongoza chama na kuongoza nchi na sio kufanya kazi ya kuungaunga mkono mtu.
“Lowassa hajaenda kuchukua fomu kwa ajili ya kuunga mkono mtu, nia yake ni kuongoza chama chetu na nchi kwa jumla na amekuwa akisema nia yake ni kuwakomboa Watanzania katika kupambana na umaskini,” alisema.
“Kifupi Lowassa ndiye anakubalika kwa wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla hata Mwandosya kule Mbeya wana-CCM wamesema wazi kuwa Lowassa anastahili kuongoza na yeye anafahamu hilo. Kwa hiyo sisi tunamuomba ajiandae kumuunga mkono Edward Lowassa mwezi Oktoba,” alisema Bashe.
Msemaji wa Wassira
Kambi ya Wasira nayo haikukubaliana na kauli kuwa inamuunga mkono Profesa Mwandosya.
Msemaji wa kambi hiyo, Masiaga Matinyi alisema suala la kumuunga mkono mgombea yoyote ndani CCM aliyeomba kuteuliwa na chama kuwania urais, halipo.
“Wassira hategemei kushindwa na hili ameshalisema mara kadhaa, kwa hiyo suala la kumuunga mkono mgombea yeyote katika ngazi za uteuzi halipo kabisa,” alisema.
Hata hivyo, alisema msimamo wa Wassira ni kumuunga mkono mgombea yeyote atakayepitishwa na CCM kupeperusha bendera ya chama hicho.
Membe
Akiwa jijini Mbeya kusaka wadhamini, Membe alisema mbele ya umati uliokuwapo kushudia tukio la kudhaminiwa kwake na wanachama kuwa Mwandosya ni mtu safi na hivyo iwapo jina lake halitapita, atamuunga mkono mbunge huyo wa Rungwe Mashariki.
“Napenda watu wajue kuwa natamka hili kwa moyo wangu wa dhati. Jina langu lisiporudi ndani ya chama, nitampigia kampeni Profesa Mwandosya. Sina tatizo lolote hata wakisema mimi nimuachie Mwandosya nipo tayari kwani ndiyo viongozi wanaotakiwa kama yeye kwa sasa kuongoza nchi yetu,” alisema.
Kauli ya Sitta
Kauli kama hiyo ilitolewa na Sitta ambaye alisema Mwandosya hayupo kwenye kundi la watu wenye matatizo ya wizi na ufisadi nchini.
“Ni kweli kama kwenye mchujo jina la Mwandosya litapita, nitaliunga mkono kwa sababu yeye ni mmoja ya watu ninaowakubali na kuamini utendaji kazi wao na wenye rekodi nzuri katika utumishi wa umma,” alisema Sitta.
Mkutano Mkuu wa CCM utafanyika mjini Dodoma Julai 12 kupitisha mgombea urais wake na utatanguliwa na vikao vya Kamati Kuu, ambayo itachuja wagombea na Halmashauri Kuu ambayo itapitisha ajenda za kikao hicho cha juu cha maamuzi kwenye chama hicho.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment