Advertisements

Thursday, June 25, 2015

RAIA WA KUWAIT AKAMATWA UWANJA WA NDEGE DAR NA KOBE 173

 Jeshi la Polisi, Uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNAI), linamshikilia, raia wa Kuwait, Hussein Mansoor, kwa kukutwa na kobe hai 173 aliokuwa akiwasafirisha kueleka nchini kwake.
Kaimu Mkurugenzi wa Uwanja wa JNIA, Clemence Jingu alisema abiria huyo mwenye hati ya kusafiria yenye namba 003870237, alikamatwa usiku wa kuamkia jana akijitayarisha kupanda ndege ya Emirates iliyokuwa ikielekea Kuwait kupitia Dubai.
Jingu alisema raia huyo alikamatwa saa tano usiku katika eneo la abiria wanaoondoka, baada ya polisi wa JNIA kwa kushirikiana na maofisa wa Wizara ya Maliasili kufanya ukaguzi na kugundua kobe hao wakiwa wamefichwa kwenye masanduku makubwa mawili.
“Hii ni moja ya kazi kubwa ambazo tunazifanya kwa sasa hapa JNIA, ila tutahakikisha kuwa hakuna nyara za Serikali zitakazotaifishwa na kupitishwa hapa kwa kuwa tumeimarisha ulinzi maradufu,” alisema Jingu.

Jingu alisema kobe hao wenye thamani ya Sh 30 milioni ni miongoni mwa nyara muhimu za Serikali ambazo zimekuwa zikitaifishwa kupitia mbinu mbalimbali.
“Pamoja na kuimarisha ulinzi, lakini tutahakikisha JNIA inakuwa bora kuliko viwanja vingine vya Afrika Mashariki na zaidi hasa kuhakikisha ulinzi unapewa kipaumbele” alisema.
Kamanda wa Polisi wa JNIA, Khamis Suleiman, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa huyo anashikiliwa na jeshi hilo kwa uchunguzi zaidi.
Tukio hilo lilithibitishwa pia na Kamishna wa Interpol, Tawi la Tanzania, Gustav Babile ambaye alisema raia huyo alikamatwa na wanyama hao huku akiwa na vibali halali.
Mmoja wa wafanyakazi wa JNIA (jina linahifadhiwa) alisema kabla ya kukamatwa, ilionekana kuna mpango umefanywa ili kumpitisha raia huyo bila kugundulika kwani taa za eneo la ukaguzi zilizimwa kwa saa kadhaa uwanjani hapo.
“Si kawaida taa kuzimwa lakini wakati yeye anapita taa zilizima jambo linaloonyesha kuwa ni njama zilizopangwa lakini hata hivyo hazikufanikiwa,” kilisema chanzo hicho.
Kadhalika chanzo hicho kilisema raia huyo aligunduliwa na askari wa maliasili akiwa tayari ameshapita katika vizuizi vyote vya ukaguzi na ameshaingia katika eneo la abiria wanaoondoka.
Tukio hili linafanana kwa kiasi kikubwa na lile lililotokea Januari 8, mwaka huu, ambapo raia mwingine wa Kuwait, Ahmed Ally Mansour alikamatwa uwanja wa JNIA akiwatorosha kenge hai 149 wenye thamani ya Sh 6.3 milioni.
Kama ilivyo kwa tukio la jana, hata tukio la Januari lilitokea saa tano, likihusisha ndege ile ile huku watuhumiwa wakiwa na ubini unaolandana.

Kadhalika, Julai 31 mwaka jana, raia wa Vietnam, Dong Van (47) naye alikamatwa uwanjani hapo akiwa na meno 65 na kucha 447.

CHANZO: MWANANCHI

3 comments:

Anonymous said...

Hao kobe si tayari walikuwa wamenunuliwa kutoka serikalini; yaani, vitalu viliuzwa kwa watu binafsi. Sasa mnamlili nani na ninyi milishauza vitalu. Kwani kitalu ni jina au tembo na kobe waliomo ndani yake. Vitalu ni vyangu; tembo na kobe mimi nitawafanyia nini kam sio kuwauza nchi za nje?

Anonymous said...

Hao kobe si tayari walikuwa wamenunuliwa kutoka serikalini; yaani, vitalu viliuzwa kwa watu binafsi. Sasa mnamlili nani na ninyi milishauza vitalu. Kwani kitalu ni jina au tembo na kobe waliomo ndani yake. Vitalu ni vyangu; tembo na kobe mimi nitawafanyia nini kam sio kuwauza nchi za nje?

Anonymous said...

Who is this anonymous? saying stating about "vitalu" vilivyonunuliwa? na nani? hati ipo kuthibitisha? Muuzaji wa vitalu hivyo ni nani? Je ni Serikali? vithibitisho? Vitalu hivyo vilivyouzwa ni eneo gani ambalo linaweza kuwa na "Nyara za Serikali" bila ya Serikali yenyewe kujua ama UMMA wa Watanzania ? Hatua gani zitafuata baada ya huyo raia wa Kuwait kukamatwa? Je, atashtakiwa mahakamani?