ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 14, 2015

Jaji Warioba amkubali Magufuli

Dar/Mikoani. Siku moja baada ya CCM kumpitisha Dk John Magufuli kuwa mgombea wake wa urais, Waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema chama hicho kimefanya uamuzi sahihi kwa kuwa waziri huyo wa ujenzi ni mchapakazi na hakutumia fedha kuipata nafasi hiyo.
Kauli hiyo ya Jaji Warioba imekuja wakati mgombea huyo akipokewa Dar es Salaam leo akiambatana na mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa kuwatambulisha kwa wananchi utakaofanyika Mbagala Zakhiem.
Juzi, Magufuli alipitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM kwa kura 2,104 na kuwashinda Balozi Amina Salum Ali aliyepata kura 253 na Dk Asha Rose Migiro kura 59.
Jaji Warioba ambaye awali aliwakemea baadhi ya wagombea wa nafasi hiyo ndani ya CCM kwa kukiuka kanuni, alisema mchakato huo ulikuwa umeingiliwa na kila aina ya michezo michafu ya rushwa na uvunjaji wa kanuni na taratibu, lakini alielezea kufurahishwa kwake baada ya mambo hayo kuwekwa kando wakati wa kupitisha mgombea.
“Nilikuwa na wasiwasi kama vikao vya chama vitatenda haki katika kupitisha mgombea kutokana na baadhi ya viongozi kujipambanua wazi kwa wagombea wanaowaunga mkono,” alisema Jaji Warioba jana.
Mwanzoni mwa mwezi huu, Jaji Warioba alieleza kasoro mbili zilizoibuka katika mchakato huo, moja ikiwa ni baadhi ya wagombea kueleza sera zao, wakati wakijua wazi kuwa sera za CCM ziko kwenye ilani yake ya uchaguzi na pili, kukiukwa kwa utaratibu uliowekwa na chama hicho kwamba yeyote anayehusika kwenye ngazi ya uamuzi, asimdhamini mgombea yeyote wa urais.
Mbali na Warioba ambaye ni Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, jambo hilo pia lilikemewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku na wajumbe wa iliyokuwa tume hiyo katika kongamano lililoandaliwa na taasisi hiyo lililofanyika Julai 9, Dar es Salaam.
“Nimefarijika jinsi hali ilivyokuwa nadhani kwa mara ya kwanza fedha haikushinda,” alisema Jaji Warioba huku akisisitiza kuwa ni jambo baya kumpata kiongozi kwa nguvu ya fedha.
Alisema pamoja na kuwa fedha haikushinda, lakini ukweli ulio wazi ni kwamba wapo waliotumia fedha nyingi katika mchakato huo kwa lengo na kupitishwa kugombea urais.
“Sote tunajua kuwa Magufuli hakutumia fedha wala viongozi wakati akisaka wadhamini mikoani. Yeye alikwenda kwa wanachama na kutafuta wadhamini kimyakimya. Ni mtu sahihi. Alifanya kazi hiyo bila kutumia fedha,” alisema.
Alisema makundi yalikuwa yanatishia kuvunja umoja ndani ya chama hicho na kwa sasa ana imani na Dk Magufuli kuwa atawaunganisha wanaCCM kutokana na rekodi zake za utendaji kazi.
Alisema mbunge huyo wa Chato ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi ni chaguo zuri kwa kuwa si mtu wa makundi na atakuwa na kazi nyepesi kuwaunganisha wanachama wa CCM.
Viongozi wa dini walonga
Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Sheikh Khamis Mataka alisema CCM imefanikiwa kumpata mgombea makini ambaye hana makundi wala kashfa za rushwa.
Sheikh Mataka alisema uteuzi wa Dk Magufuli ni tumaini jipya kwa Watanzania kwa sababu amejipambanua kwa utendaji wake wa kazi serikalini ikiwa ni pamoja na kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Nakumbuka kulikuwa na mfanyabiashara mmoja ambaye alitaka kusafirisha boti kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kwa njia ya barabara, Dk Magufuli alimzuia kwa sababu barabara hazihimili uzito mkubwa,” alisema.
 “Hakuna aliyedhani kuwa Magufuli atakuwa mgombea urais wa CCM, alichukua fomu kimyakimya, alitafuta wadhamini kimyakimya, alirudisha kimyakimya,” alisema Sheikh Mataka.
Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge, Ngara mkoani Kagera, Severini Niwemugizi alipongeza uteuzi wa Dk Magufuli kwa kuwa amekuwa mtendaji kazi na amekuwa akitenda haki kulingana na taratibu za kisheria.
Hata hivyo, Askofu Niwemuguzi alisema hana imani na mgombea mwenza, Samia kutokana na utendaji wake akiwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba.
Alisema kuwapo makamu wa rais aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bunge hilo haoni kama Watanzania watapata matumaini ya kupata katiba waitakayo kwa masilahi ya Taifa.
“Labda wapate ushauri mzuri wanaweza kuafikiana na kurudisha mchakato wa Katiba Mpya na kutuunganisha na kubaini chanzo cha kutugawa kutokana na Katiba Inayopendekezwa,” alisema.
Alishauri, iwapo Dk Magufuli atashinda asimamie maendeleo ya wananchi kwa kuweka mikakati ya kuboresha elimu ambayo inaweza kuinua maisha ya Watanzania dhidi ya umaskini
“Elimu ndiyo itaondoa maradhi na umaskini na watu kutumia fani mbalimbali katika mazingira yao kujikwamua kiuchumi,” alisema Askofu Niwemugizi ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC).
Mapokezi Dar
Akizungumzia mapokezi ya mgombea huyo, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba alisema Dk Magufuli na Samia watapokewa saa 8.00 mchana wakitokea Dodoma.
Simba alisema mkutano huo ambao utahutubiwa na wagombea hao wawili, utawakutanisha wanaCCM na wananchi kutoka katika wilaya za Ilala, Temeke na Kinondoni.
“Lengo la mkutano huo ni kuwatambulisha na kuwapongeza wagombea hao watakaopeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu,” alisema.
Simba alisema kwa kumteua Magufuli, mgombea yeyote atakayesimamishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuwania urais atashindwa.
Chavita wampongeza
Uteuzi wa Dk Magufuli umepokewa kwa mikono miwili na watu wenye ulemavu wa kusikia mkoani Morogoro kutokana na utendaji wake na kutokuwa na makundi ndani na nje ya chama.
Katibu wa Chama cha Viziwi Tanzania (Chavita) mkoani Morogoro, Henry Matasia alisema uchapakazi wa Dk Magufuli ndiyo uliowafanya wamkubali na kuwa na imani naye tofauti na kama angeteuliwa mtu mwingine.
Pia,  wafanyabiashara wa Soko la Mawenzi, John Peter na Tatu Bakari walisema Dk Magufuli ni kiongozi anayekubalika na wananchi katika utendaji wake.
Dk Shein apokewa Zanzibar
Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Dk Ali Mohamed Shein jana alipokewa Zanzibar kwa kishindo baada ya kuteuliwa tena kugombea urais wa Zanzibar.
 Akizungumza na wanahabari katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Aman Karume, Dk Shein alisema mchakato wa kumpata mgombea urais wa Muungano kupitia CCM haukutawaliwa na sintofahamu yoyote kama baadhi ya watu wanavyoeleza, bali ulizingatia utaratibu na kanuni za uchaguzi za chama hicho. “Tulijadili kwa kina sifa za wagombea na kushauriana hadi mwishoni tukafikia makubaliano na ndiyo maana tulipiga kura kwa utulivu na nidhamu kwa mujibu wa taratibu za chama chetu,” alisema Dk Shein.
Kuhusu malalamiko kuwa baadhi ya wananchi wananyimwa vitambulisho vya ukaazi na hatimaye kukosa kupiga kura, Dk Shein alieleza kushangazwa na baadhi ya wanasiasa kuwapotosha wananchi kwa kutaka suala hilo lishughulikiwe kisiasa badala ya kufuata sheria zilizopo.
“Baadhi ya wanasiasa wanajisahau na kuwapotosha wananchi. Sheria haikusema wanasiasa washughulikie matatizo ya vitambulisho badala yake imeelekeza wananchi wafanye hivyo kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Raymond Kaminyoge, Peter Elias (Dar), Esther Mwimbula (Morogoro) na Shaban Ndyamukama (Ngara).

Mwananchi

No comments: