Wednesday, July 8, 2015

Kimondo: Mwashiuya sasa ruksa Yanga.

Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha.

Mshambuliaji Geofrey Mwashiuya ambaye alikuwa akidaiwa kujiunga na Yanga kinyemela, sasa ni mchezaji halali wa kikosi hicho kinachonolewa na Mholanzi Has van der Pluijm baada ya klabu hiyo ya Mtaa wa Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam kumalizana kimya kimya na Kimondo FC.

Klabu ya Yanga na Kimondo FC zilikutana jana jijini Mbeya kwa ajili ya kutafuta muafaka na inaelezwa kuwa kikao hicho kilichukua zaidi ya saa sita kulimaliza sakata hilo.

Akizungumza na NIPASHE jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha, alisema wamemalizana na viongozi wa Kimondo FC ambao wamekubali rasmi kuvunja mkataba na Mwashiuya na sasa ni mchezaji halali wa Yanga.

Tiboroha alipotakiwa na gazeti hili kutaja dau waliloafikiana ili kuvunja mkataba huo alisema: "Hatuwezi kusema kiasi cha fedha ambacho tumekubaliana isipokuwa tumeingia mkataba wa kusaidiana katika suala zima la kuuziana wachezaji pamoja na masuala mengine kwa ajili ya kuendeleza soka la wachezaji wa timu hiyo."

Alisema kwa sasa hakutakuwa na kelele tena za kugombea mshambuliaji huyo kwa sababu wamekamilisha usajili wake kama ambavyo viongozi wa Kimondo FC walivyowataka kufuata utaratibu.

Katibu huyo alisema kikao kilikuwa kirefu lakini chenye mafanikio makubwa baada ya pande zote mbili kukubaliana na kumaliza sakata hilo.

"Kuna gharama ambazo tumekubaliana kulipa lakini ni siri baina yetu," alisema Tiboroha.

Naye Mkurugenzi wa Kimondo FC, Erick Ambakisye, alisema ni kweli wamekutana na wamemalizana na Yanga kwa kuvunja mkataba na kwamba sasa Mwashiuya ni mchezaji halali wa Yanga.

"Tunashukuru Yanga wamefuata taratibu tunaomba na timu nyingine ziige mfano wa Yanga,"alisema Ambakisye.
Alisema kuna timu za JKT Ruvu, African Lyon na Majimaji ambazo zinawachezaji wa Kimondo, hivyo ni bora wafuate taratibu za usajili kama ilivyofanya Yanga na Mbeya City.

Akizungumzia makubaliano yao, alisema makadirio ilikuwa walipwe Sh. milioni 50, ambazo ndani ya mkataba wa makubaliano, Yanga kila inapoenda Mbeya kucheza mechi za Ligi Kuu, watacheza nayo mchezo wa kirafiki na mapato yote kuchukuliwa na Kimondo FC.

Alisema mbali na hilo, pia watakuwa wakija Dar es Salaam katika mechi za Yanga kwa gharama za klabu hiyo.
Ambakisye alisema sharti lingine ambalo wamekubaliana na Yanga ni kuwaomba radhi Kimomdo FC kwa maneno waliyotoa kupitia vyombo vya habari kuwa Mwashiuya alikuwa mchezaji huru ilhali walikuwa na mkataba wa miaka mitatu na mchezaji huyo.

Alisema baada ya makubaliano hayo, wameunga undugu na Yanga na sasa wao ni kitu kimoja na Mwashiuya katika safari yake ya kuitumikia Yanga.
CHANZO: NIPASHE

No comments: