Thursday, July 9, 2015

MASHTAKA 7 DHIDI YA LOWASSA


Na. M. M. Mwanakijiji
Wapo Watanzania ambao wanaamini na wanamtaka Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa awe rais wa awamu ya tano. Wana sababu zao za kufanya hivyo na wana haki zote za kumfanyia kampeni, kumuunga mkono, kumchangia na hata kujitolea kumsaidia apite kwenye mchakato ndani ya CCM na hata kwenye Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka huu. Haki hii ya kumchagua kiongozi unayemtaka ni haki ya msingi ya Kikatiba.
Wapo pia Watanzania ambao hawaamini na hawamtaki Lowassa kuwa rais wa awamu ya tano. Na hawa nao wana sababu zao na wana haki zote za kufanya hivyo. Wanao haki pia ya kufanya kampeni dhidi ya kugombea kwa Lowassa na kujaribu kuzuia asipitishwe ndani ya chama hicho na kama akipitishwa basi kufanya yote yanayowezekana kisheria kuhakikisha kuwa hachaguliwi kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 mwaka huu. Mimi niko kwenye kundi hili la pili na msimamo wangu juu ya Lowassa siyo siri kwa watu ambao wamekuwa wakinisoma kwa miaka hii karibu kumi sasa.

Kumkataa Lowassa na kukataa uongozi wake siyo suala la kuukataa ubinadamu wake au utu wake kama binadamu mwingine. Suala la kumkataa Lowassa kwa baadhi yetu siyo suala la chuki binafsi, wivu, husuda au kumuonea. Ni suala la tofauti za msingi ambazo hatujaona ni namna gani tunaweza kuzipatanisha tofauti hizi na sauti ya dhamira ndani ya mioyo yetu. Hatumtaki na tunataka kuwashawishi wengine wamkatae si kwa sababu ni Lowassa bali ni kwa sababu ya kile ambacho yeye anakiwakilisha kama kiongozi.

Ni kwa sababu hiyo nimeonelea ili kuweka sawa dhamira yangu na watu waelewe kwanini wengine hatujawahi kuvutiwa na uongozi wa Lowassa na kwanini hata akipitishwa kugombea Urais kwa tiketi ya CCM tutajitahidi kuwashawishi wengine wasimchague. Nitaweka kile ambacho naweza kukiita ni “mashtaka” yaani “charges” dhidi ya Lowassa ambazo muda wote tangu alipojiuzulu na hadi hivi sasa hajawahi kutoa majibu yenye kuweza kumfanya aonekane asiye na hatia (innocent). Ni mashtaka yanayohusiana na uongozi wake kwa muda wote aliokuwa Waziri Mkuu na wakati ambapo amekuwa mbunge hadi hivi alivyotangaza nia.

Mashtaka haya tunayaweka wazi ili kila Mtanzania mwenye kutanga kujenga dhamira yake kabla ya kupiga kura basi aijenge ili hatimaye aweze kuwa na sababu ama ya kumpigia kura au kumkataa. Kuweza kuelewa uzito wa mashtaka haya ni muhimu kuangalia dhana nzima ya “maamuzi” ambayo Lowassa amekuwa akiisimamia. Na hasa kile ambacho anakiita mara kwa mara kuwa ni “maamuzi magumu”. Tuangalie jinsi gani Lowassa alifanya maamuzi mbalimbali na kwa namna gani maamuzi hayo yanatuonesha kuwa Lowassa ni kiongozi wa namna gani. Mashtaka haya ni:

KWAMBA, Edward Lowassa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alionesha Kilele cha Udhaifu Kwenye Sakata la Richmond

Mojawapo ya mambo ambayo yameandika historia ya L owassa na ambayo yanamfuata kama kivuli ni kuhusika kwake katika sakata la kampuni ya Kimarekani ya Richmond iliyoingia nchini ikidai kuja kufua nishati ya umeme chini ya Mkataba na Tanesco. Watu wengi wanapozungumzia Richmond na Lowassa wengi huzungumza juu juu tu wakitoa madai ambayo ni vigumu kuyathibitisha. Kwa mfano, yamewahi kutolewa madai ya umiliki wa Lowassa (au familia yake) wa kampuni ya Richmond kiasi kwamba hata kampuni ikaitwa jina la utani la Richmonduli – ikichezea jina la jimbo analowakilisha Lowassa la Monduli, Mkoani Arusha. 

Madai mengine kama alipokea rushwa ili kuipitisha Richmond ni vigumu kuyathibitisha hasa kwa vile bila mtu au chombo maalum kushuhudia rushwa hiyo ni vigumu kuithibitisha hivi hivi. Hata kwa kuangalia ushahidi wa kimazingira mtu atapata shida kuweza kuona kiasi cha fedha ambacho Lowassa inadaiwa kupewa kilikuwa ni kiasi gani, kilitoka kwa nani na kuingia vipi. Ni kwa sababu hiyo kama rushwa ilikuwepo basi ilifanyika kwa namna ambayo ni ngumu mno kuithibitisha mahakamani.

Pamoja na hayo, kuna baadhi ya mambo ambayo hayana utata hata chembe wa kuhusika kwa Lowassa katika kuliingiza taifa katika Mkataba mbovu wa Richmond. Lowassa hajawahi kukanusha au hata kutoa maelezo yakueleweka ya nafasi yake kama Waziri Mkuu katika kuhusika kwake katika sakata hili. Kuelewa uzito wa mambo haya ni vizuri kujikumbusha madaraka ya Waziri Mkuu wa Tanzania kama yalivyoanishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Chini ya Ibara ya 52 na 53 ya Katiba yetu Waziri Mkuu ndiye mtu mwenye madaraka ya “udhibiti, usimamiaji, utekelezaji” wa shughuli za siku kwa siku za Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Na atafanya mambo yote hayo kwa maelekezo ya Rais na atawajibika kwa Rais moja kwa moja. Waziri Mkuu pia ni mtu wa tatu anayeweza kuongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kama Rais na Makamu wake hawapo na ndiye atakuwa kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni. 

Na pamoja na mawaziri wanawajibika Bungeni kwa niaba ya Serikali. Ni yeye pia ambaye kwa mujibu wa Katiba hiyo hiyo anashauriana na Rais kabla ya Rais hajaunda Baraza la Mawaziri – Rais ni lazima ashauriane na Waziri Mkuu kuunda Baraza la Mawaziri; Katiba haimlazimishi kukubaliana na ushauri wa Waziri Mkuu kuhusiana na baraza hilo hata hivyo. Pamoja na hayo majukumu Waziri Mkuu anatakiwa kumshauri Rais kabla hajafanya uteuzi wa Wakuu wa Mikoa ya Tanzania Bara.

Ni kwa msingi huo basi ni vizuri kuelewa kuwa Waziri Mkuu Lowassa alikuwa katika nafasi ya kipekee ya kuweza kumshauri Rais kuhusiana na kampuni ya Richmond kwani alikuwa na uwezo na nafasi ya kupata taarifa zozote ambazo zingemsaidia katika kutoa ushauri ama kwa Rais moja kwa moja au kwenye Baraza la Mawaziri. Lowassa hakufanya hivyo kwa ufanisi na kama alijaribu kufanya hivyo ni wazi kuwa hoja zake hazikusikilizwa na hakuwa na ushawishi unaotakiwa kitu ambacho kingetosha kumfanya ajiuzulu kabla hata ya kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge. Baadhi ya mambo ambayo yalitokea na kusababisha kuliingiza taifa kwenye kifungo cha Richmond Lowassa akiwa Waziri Mkuu ni haya:

1. KWAMBA, Yeye kama Waziri Mkuu alishindwa mara moja kukemea kitendo cha Wizara ya Nishati na Madini kuanza mchakato wa kutangaza tenda za ndani na kwa muda usioruhusiwa kisheria kinyume na maelekezo ya Baraza la Mawaziri. Baraza la Mawaziri ndiyo chombo cha juu kabisa nchini cha kumshauri Rais. Waziri Mkuu alipaswa kusimamia maelekezo ya Baraza hilo chini ya Ibara ya 52 na 53 ya Katiba yetu. Hakufanya hivyo.

2. KWAMBA, Lowassa akijua utata wote uliokuwepo kwenye kampuni ya Richmond LLC ambayo tayari ulishajulikana na akijua kuwa kampuni hiyo haikufanyiwa uchunguzi wa kina (due diligence) baada ya kujiingiza kwenye tenda aliridhia pendekezo la Waziri wa Nishati na Madini (Msabaha wakati huo) la Juni 19, 2006 aliyeshauri kuwa Tanesco iingie mkataba na Richmond. Tarehe 21, 2006 katibu wa Waziri Mkuu aliiandikia Wizara kuwa Waziri Mkuu ameridhia pendekezo hilo. Siku hiyo hiyo Waziri wa Nishati alimpa dokezo Katibu Mkuu (Nishati na Madini) aiagize Tanesco iingie mkataba na Richmond kufuatia Waziri Mkuu kukubali pendekezo lake la awali. Katibu Mkuu akamwandikia barua aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco Balozi Fulgence Kazaura ili Tanesco iingia mkataba na Rinchmond. Tarehe 23 Juni 2006 Richmond na Tanesco waliingia Mkataba.

Hakuna utata wala shaka tunaposema kuwa Richmond iliingizwa na Lowassa. Haijalishi kama hakupokea senti hata moja; ukweli ni kuwa kama yeye angetimiza wajibu wake vizuri na kama angefikiria matokeo ya maamuzi yake taifa lisingejikuta kwenye mkataba ule wa Richmond.

Hakuna utata kuwa Sheria ya Manunuzi ya Umma ambayo ilitakiwa kufuatwa kwenye mchakato ule haikufuatwa na haikufuatwa kwa sababu Waziri Mkuu aliamini yuko juu ya sheria; kwamba neno lake linaweza kuwa juu ya matakwa ya Sheria. Hili ni kosa ambalo nchi ya kidemokrasia kama ya kwetu haiwezi kulifumbia macho. Ni sawasawa na tulivyomkatalia Pinda pale alipotaka watu “wao nao wauawe” au pale alipotaka wengine “wapigwe tu”. Waziri Mkuu hawezi kuwa wa kwanza kuvunja sheria akaachiliwa.

Swali ambalo liliulizwa na Kamati Teule kwenye ripoti yake iliyosomwa na Mwenyekiti wake Dr. Harrison Mwakyembe kuwa “Je, uwazi gani na ushindanishi gani ulikuwepo kwa Wizara ya Nishati na Madini ikishirikiana kwa karibu na Ofisi ya Waziri Mkuu, kusitisha mchakato wa zabuni ndani ya TANESCO na kuunda chombo kipya nje ya taratibu ili kumteua mzabuni kwa niaba ya TANESCO?” Lowassa hajalibu. 

KWAMBA, Kwa Kuzira Kwake Uwaziri Mkuu Lowassa Alionesha Udhaifu Mwingine

Uamuzi mwingine ambalo Lowassa aliuchukua na ambao nao ulilitikisa taifa kwa muda ni kitendo chake cha kujiuzulu Uwaziri Mkuu kufuatia madai na hoja zilizotolewa kwenye ripoti ya Kamati Teule ya Bunge kuhusiana na kampuni ya Richmond na mkataba wake na TANESCO. Kinyume na watu wengi wanavyofikiria Lowassa hakujiuzulu kwa sababu alikuwa anawajibika kutoka na makosa ambayo yeye kama kiongozi na ofisi yake waliyafanya kuhusiana na mchakato wa Richmond. Lowassa hakujiuzulu kwa sababu alikubaliana na madai yaliyotolewa na kamati ya Mwakyembe. Lowassa alijiuzulu kwa sababu aliamini watu walikuwa wanataka tu kiti chake cha Uwaziri Mkuu na kuwa maadui wake walikuwa wanataka kumuangusha tu.

Tukumbuke alijiuzulu kwa sababu aliamini hakupewa nafasi ya kujitetea kwenye Kamati Teule na kuwa wangemuita hata kwa miguu angetembea. Alijiuzulu akipinga kile alichoona ni kutotendewa haki. Kwa maelezo yake mwenyewe alisema siku ile ya kukumbuka Februari 7, 2008:

Mheshimiwa Spika, lakini nimetafakari kwa makini sana jambo hili nikajiuliza hivi kulikoni mpaka watu wazima wenye uwezo wao, watu maarufu wenye heshima zao, mpaka wafike mahali waache jambo la msingi kama hilo kulikoni? Mimi nadhani there is a wish which I am going to grant, ni Uwaziri Mkuu. Nadhani tatizo ni Uwaziri Mkuu. Kwamba ionekane Waziri Mkuu ndio amefanya haya, tumuondolee heshima au tumwajibishe.


Hakuna shaka kabisa Lowassa aliuzira Uwaziri Mkuu. Hata kama hakupewa nafasi ya kujitetea kwenye Kamati Teule Spika wa Bunge la Muungano wa wakati ule Samuel Sitta alimpa nafasi ya kwanza kuzungumza na kujitetea. Kwa watu ambao tunaujua uwezo wa kushawishi wa Lowassa tulishangazwa sana na uamuzi wake wa kuweka manyanga chini kwani tulijua kama angetaka kujitetea Lowassa angeweza. Siyo tu kuwa angeweza alikuwa na kile alichokiita “ushahidi” ambao alimpatia Spika lakini alishindwa kuutoa mbele ya Watanzania.

Lowassa angeweza kabisa – kama angetaka – kutetea Ofisi ya Waziri Mkuu kwani kama kina Mwakyembe walisema “uongo” pale Bungeni alikuwa na wajibu wa historia na dhamira wa kuweka ukweli wazi. Alipaswa kuumbua uongo ule hoja kwa hoja na kulipa taifa nafasi ya kuuona ukweli. Hakufanya hivyo!

Lowassa aliweka mbele hisia zake za hasira, uchungu na msongo wa mawazo kiasi cha kutotumia muda kutafakari matokeo ya maamuzi yake hayo. Lowassa alipewa nafasi ya kujitetea mbele ya Bunge hakufanya hivyo; alizira. Alijaribu kujitetea masaa machache kwenye TVT (TBC1 ya sasa) alipohojiwa na Tido Mhando lakini pia hakuweka ushahidi wowote kinyume (contrary) wenye kuonesha kuwa yeye hakuhusika na kuibeba Richmond kitu ambacho hata akifanya bado kitamrudia kwani kama Waziri Mkuu alifanya nini kuzuia Richmond isiingie Mkataba?

Kama alitoa ushauri kwa Baraza la Mawaziri au kwa Rais mwenyewe kuwa Richmond isipewe mkataba ule (kama ambavyo amekuwa akidai baada ya kujiuzulu) kwanini hakujiuzulu mara moja ushauri wake mzito na muhimu kwa taifa ulipokataliwa? Si ndiyo sababu ambayo Nyerere aliwahi kuitoa ikasababisha Waziri Mkuu Malecela kujiuzulu kutokana na ushauri wake kwa Rais Mwinyi kuhusiana na uundwaji wa Serikali ya Tanganyika? Waziri Mkuu huwezi kumshauri Rais jambo kubwa akakataa na wewe ukabakia Waziri Mkuu! Lowassa alilikosa somo hili la Mwalimu?

KWAMBA, Katika Ujio wa Dowans Holding N.A Lowassa alionesha Udhaifu mwingine

Baada ya Richmond kushindwa kutimiza sehemu yake ya mkataba wake na Tanesco, kampuni nyingine ya Dowans ikaingia kati kuchukua mkataba ule. Kwa mara nyingine tena tuliopiga kelele tulipiga kelele; Dowans kama ilivyokuwa Richmond zote zilikuwa ni kampuni zilizoundwa kwa ajili tu ya kukusanya fedha za sekta ya nishati Tanzania kwa kisingizio cha kuja kufua umeme. Wakati ule nilionesha – kwa wanokumbuka – jinsi gani Dowans ilikuwa kampuni hewa ya mfukoni huo ilikoandikishwa. Niliweza hata kufuatilia hadi ulipo mlango wa inayodaiwa kuwa ni ofisi ya Dowans huko Costa Rica. Kama Richmond Dowans haikustahili kupokelewa na serikali yetu. Lakini ikapokelewa.

Kama kulikuwa na mtu ambaye angeweza kulikumbusha taifa na hata namna fulani kuonesha kuwa amejifunza ya Richmond ilikuwa ni Lowassa – sasa akiwa Mbunge. Lowassa hakupasa sauti yake wale kuonesha utetezi wa Tanzania dhidi ya utapeli mwingine. Asingeweza kupata sauti bila ya shaka kwa sababu Dowans ilikuwa ina mahusiano ya karibu na swahibu wake na mtu ambaye aliwasaidia kina Kikwete kuingia madarakani 2005 – Rostam Aziz. 

Siyo hivyo tu mmiliki halisi ambaye ni mzaliwa wa Zanzibar mwenye uraia wa Oman huko alikuwa ni mtu aliyechangia pia kampeni ya Kikwete (ukiamini vyanzo vya habari vya wakati ule). Ni vizuri kutaja hapa pia kuwa wamiliki halisi wa Richmond pia ni vijana wenye asili ya Tanzania (toka familia ya Gire) huko mkoani Pwani. Na wao pia wanaonekana kuchangia kampeni kadhaa mwaka 2005. Wakati ule kwenye Richmond nilikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuifunua kampuni ya Richmond ya Houston kuwa ilikuwa ni ya mambo ya printing na siyo masuala ya nishati.

Kama mimi mtu wa kawaida niliweza kupata taarifa hizi zote ni kweli inawezekana serikali ya Tanzania ikitumia uwezo wake wote ilishindwa kuwa na taarifa hizi kiasi cha kuingizwa mkenge mara mbili?

Lowassa alikuwa wapi? Huyu ambaye leo watu kama wenye ugonjwa wa usahaulifu (amnesia) wanamuona ati ni mtu mwenye “maamuzi magumu” mbona hakuonesha uamuzi hapa zaidi ya uamuzi uliolinda maslahi ya marafiki zake? Hivi Lowassa angesimama na kuinyoshea kidole Dowans na kusema ni mchezo mwingine si angalau watu tungemuona kweli analitakia mema taifa? Lakini alichukua uamuzi; uamuzi wa kukaa kimya! Uamuzi ambao uliingiza taifa kwenye kesi nyingine nzito ambayo isingeweza kushinda.

Ikumbukwe kuwa kama nilivyoonesha katika ripoti yangu ya wakati ule Dowans na Richmond ziliichezea mchezo TANESCO kiasi kwamba zilirithishana mkataba kinyume na Mkataba wa Richmond na Tanesco wa 23 Juni, 2006.

KWAMBA, Uamuzi wake wa Kukaa Kimya Bunge Ulifunua Udhaifu Mwingine

Baada ya kujiuzulu Uwaziri Mkuu katika namna ya kuzira vile Lowassa inaonekana aliamua hata kuzira kuzungumza Bungeni au hata kutoa mawazo yake juu ya mambo mengi ya kitaifa yaliyokuwa yanaendelea Bungeni. Alipokuja kuibuka aliibuka na ile hoja yake ya kuwa kuna “ugonjwa” ambao umeingia serikalini kwamba watu walikuwa hawafanyi “maamuzi magumu”. Kwanini Lowassa hakusimama kuonesha huu ugonjwa tangu alipoondoka? Si alikuwa ni Mbunge? Si wengine walikuwa wanachangia? Yeye aliamua kususa?

Ni kiongozi wa namna gani ambaye ameshikwa na machungu au hasira kiasi kwamba hataki hata kutoa mawazo yake lakini leo ati amepata mawazo ya kutatua matatizo ya wananchi kwa vile anautaka Urais sasa? Na wapo watu ambao wanaamini kabisa ‘nia’ yake hii ya dhati? Watu ambao wengine ati wanaapa “patachimbika”? Hapakuchimbika alipojiuzulu cheo alichokuwa nacho paje kuchimbika kwa kupoteza cheo ambacho hana?

Ukimya wake si ulipiga kelele kutuonesha yeye anaongozwa na nini hasa?

KWAMBA, Kwenye Sakata la Wanafunzi 21 Waliotelekezwa Ukraine Lowassa Alionesha Udhaifu Mwingine

Mojawapo ya mambo ambayo Lowassa amekuwa akiyadokeza na kuyazungumzia kwa nguvu baada ya kuanza tena kuzungumza Bungeni ni suala la elimu. Amefikia mahali pa kudai kuwa sera sahihi ya kuliinua taifa ni “Elimu Kwanza”. Hii ni kinyume na dhana iliyoanzishwa na Serikali ambayo yeye alikuwemo ndani yaani “Kilimo Kwanza”. Lowassa amesema hilo mara nyingi lakini mfano mzuri ni pale alipohojiwa katika kipindi cha Dakika 45 28 Augusti, 2012. Lowassa alinukuliwa kusema “Mpango huu wa Kilimo Kwanza umekosa nguvu kwa sababu kuanzishwa kwake hakukuzingatia dhana ya ukombozi wa mwananchi wa kawaida. Tangu awali ndani ya chama (CCM) nilieleza kuwa sitaunga mkono hoja hiyo mpaka kuongezwe mashiko na kuwa Elimu Kabla ya Kilimo Kwanza”

Baadhi yetu hata hivyo tunamkumbuka Lowassa kwa kushindwa kwake kuingilia kati na kutetea haki ya vijana wa Kitanzania 21 waliopelekwa Ukraine kusomea mambo mbalimbali wote wakiamini kuwa walifanya hivyo wakiwa na uhakika wa udhamini wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Kama nilivyoonesha hapo juu kuwa Waziri Mkuu chini ya Ibara ya 52 na 53 ya Katiba yetu ndiye mwenye jukumu la kufuatilia utendaji kazi wa kila siku wa Serikali yetu. Vijana wale – ambao wengi kama siyo wote wamehitimu katika mazingira magumu kweli kweli – walijikuta wanaachishwa masomo na wengine kujikuta kwenye hali ngumu ya maisha.

Hali ilipokuwa ngumu vijana wale walienda Ubalozi wa Uingereza Kiev, Ukraine kuomba msaada na hifadhi. Hawakuweza kupewa msaada mkubwa zaidi ya kuachwa kukaa na kulala nje ya Ubalozi wa Uingereza wakitumaini Serikali yao (ikisimamiwa na Lowassa) itakumbuka umuhimu wa elimu yao kule ugenini. Nilipata nafasi wakati ule ya kuzungumza na Lowassa – na sakata lile lilikuwa nimeliandika kwa kirefu nikiwakilisha sauti za watoto wale – na jibu lake hadi leo limeacha mwangwi kwenye moyo wangu. Nilipomwambia juu ya hali za watoto wale na kuwa wanapigwa na baridi kwanini Serikali isiingilie kati jibu lake lilikuwa “Nakula sasa hivi”.

Siwezi kusahau jibu lile. Yaani hata kuonesha kujali watoto wa Watanzania maskini, wako ugenini, wa kike na wa kiume wanapata taabu kisa wanataka kuendelea na elimu Waziri Mkuu wao anasema sasa anakula. Angalau nilipozungumza na Rais Kikwete yeye alisema tu kama hizo ngazi za chini wakishindwa basi litamfikia. Lowassa ambaye leo anaimba “Elimu kwanza” alisahau kabisa kuwa msingi mkubwa wa Katiba yetu ni “utu kwanza”!? Utaweza vipi kumsomesha mtoto kama huujali utu wake? Na cha kushangaza wapo watoto wengine wa maskini ambao labda sababu ya kutokufikiri vizuri au vinginevyo wanashangilia kuwa kweli Lowassa anawakilisha “elimu kwanza”.

Lowassa alishindwa kuonesha hili kwa vitendo; alifanya uamuzi wake; wa kula. Hili nilisema wakati ule inawezekana ni dhambi kubwa zaidi ya utawala wa Kikwete kwa wakati ule; na Lowassa litamrudia.

Lakini siyo kwenye hili tu; miaka hii michache tangu ajiuzulu Uwaziri Mkuu tumeona jinsi gani sekta ya elimu ikipata changamoto za ajabu hadi serikali kuamua kubadili vipimo vya watahiniwa ili angalau matokeo yapendeze kidogo. Muda huu wote Lowassa ametoa mchango gani wa mawazo? Hivi watu wanajua Lowassa anafikiria nini kuhusiana na kushuka kwa kufaulu? Amewahi kushauri kitu gani Bungeni ili kuinua ubora wa elimu? Hivi amewahi kuangalia ni kwa namna gani ufisadi unaathiri elimu na yeye msimamo wake uko vipi? Kama muda wote huu wote akiwa Mbunge hajawahi kuja na mswada wowote wenye lengo la kuinua elimu au kuchochea ajira leo hii anapotaka Urais anapozungumzia elimu au ajira ni vipi tumuamini?

KWAMBA, Kwa Kubadili Matumizi ya Barabara Kinyume cha Sheria Lowassa Alionesha Udhaifu Tena

Mojawapo ya maamuzi ya Lowassa ambayo naweza kusema yanadaiwa kuwa na matokeo makali zaidi ni pale alipoamua kutangaza kubadilisha matumizi ya barabara za Dar ili kupunguza foleni za magari wakati wa asubuhi na jioni. Mpango huu sijui aliufikiria kwa kina kiasi gani na alishauriana na nani; lakini aliamua kuutangaza mwaka 2007 kuwa matumizi ya barabara yatabadilishwa. Alifanya hivyo bila kujali matakwa ya sheria ya Usalama Barabarani. Na kwa vile neno lake lilichukuliwa kama sheria watu walianza kutekeleza. Matokeo yake – sijui takwimu zikoje – mpango ule ulikufa wenyewe kwa sababu ulileta vuguru barabarani, kusababisha ajali na hata watu waliopata ajali kutolipwa bima kwani walionekana wao ni wenye makosa.

Je, tukisema uamuzi huu wa Lowassa umegharimu maisha ya watu kwa sababu haukufikiriwa vizuri na haukupangwa vizuri tutakuwa tumekosea?

KWAMBA, Kwa Kutukuza Marafiki Wenye Kumpa Fedha za Kugawa Lowassa Ameonesha Udhaifu Mkuu

Sijui kama Lowassa amewahi kutafakari uzito na umaana wa kauli zake mbalimbali. Toka alipozungumzia habari za “Sungura” Bungeni hadi leo hii sijawahi kuona umakini wa kauli za Lowassa hasa ukizifuatilia kwa karibu. Lowassa amelisema hili la kuwa ana marafiki wenye kumchangia fedha mara kadhaa sasa. Alilisema kule Mbeya kwenye Kanisa la Moravian Usharika wa Ruanda. Alinukuliwa kusema “Nasingiziwa sana kuwa mimi ni tajiri, lakini utajiri wangu unatokana na Harambee hizi ambazo zinachangiwa na Marafiki na nina amini sitafilisika”

Hili amelirudia tena miezi miwili tu hivi nyuma wakati akizungumza na waandishi wa habari. Lowassa alinukuliwa kusema “Sina fedha ila nina marafiki wengi, nikipata mwaliko wa kuchangia nawatafuta marafiki zangu wanachanga. Mfano ‘juzi’ nilipomwakilisha Makamu wa Rais mjini Arusha, marafiki zangu walichangia Sh100 milioni, Makamu wa Rais alichangia Sh10 milioni na watu wa Arusha wakatoa Sh100 milioni. Hizo hazikuwa fedha zangu, ila ni watu walichangia.”

Mtu yeyote ni lazima afikirie sana anaposikia kuwa mwanasiasa ana marafiki wengi ambao wako tayari kumchangia mamilioni ati kwa sababu amewaomba tu. Kwenye nchi za wenzetu na ambazo zinaangalia sana mifuko ya wanasiasa au viongozi wa umma baadhi ya watu wakitoa michango na ikajulikana wamempa mwanasiasa mwanasiasa huyo anaweza kujikuta analazimishwa kurudisha michango hiyo. Lowassa anatuambia kuwa ana “marafiki”; hili peke yake siyo shida. Kwa mwanasiasa anayetaka kuwa Rais wa nchi suala la marafiki linakuwa siyo la binafsi tena bali la nchi na wananchi. Maswali yanahitaji kujibiwa:

Marafiki hawa ni kina nani na wanafanya shughuli gani kiasi cha wao kutoa fedha hizi kila wanapoombwa?

Marafiki hawa wanatarajia kupata nini pindi Lowassa akiwa Rais? Haiwezekani watu wachangie tu hivi hivi hasa kwa mwanasiasa. Tayari tuna ushahidi wa watu kuchangia kampeni ya Rais Kikwete mwaka 2005 kiasi cha kuwa kashfa kubwa tu. Kwanini tusiamini wachangiaji hawa wanaweza kutaka dili fulani fulani baadaye?

Marafiki hawa wa Lowassa ni Watanzania au wapo marafiki kutoka nje? Hili nalo ni swali zito. Na kiukweli maswali haya ya marafiki yanapaswa kuulizwa watangaza nia wote na wa wavyama vyote na ikiwezekana rekodi ya ‘hao’ marafiki inatakiwa iwekwe wazi. Vipi kama wanaomchangia ni majambazi? Wanaiba benki au taasisi fulani halafu wanatoa kidogo kwa mwanasiasa?

Hawa marafiki wenye fedha nyingi hivi ni kitu gani kinawazuia wao wenyewe ama kuanzisha taasisi za kutoa michango ya kibinadamu (philanthropic donations) kwa watu wenye kuhitaji hadi wamtumie Lowassa? Au ni kitu gani kinawafanya watu hawa wenye mihela hivi washindwa wao wenyewe kuchangia misikiti na makanisa hadi wamtumie Lowassa? Inawezekana wanayo sababu lakini ni vigumu kujua sababu kama hatuwajui watu hawa wenye kutoa fedha hizi nyingi kwa Lowassa bila kwa namna fulani kumuweka Lowassa kwenye mikono yao.

Hitimisho

Naweza kuonesha mambo mengine zaidi – ikibidi kufanya hivyo nitafanya endapo CCM wataamini huyo ndiye mpeperusha bendera wao – lakini hapa itoshe. Itoshe kusema tu kuwa kwa kuangalia mambo haya machache niliyoyaita mashtaka mtu yeyote anaweza kuona mambo kadhaa ambayo yanamfanya Lowassa kuwa ni miongoni mwa viongozi wabovu, wasiofaa na ambao wanapaswa kukataliwa kupewa nafasi ya Urais. Si kwa sababu ya chuki, husuda au wivu bali kwa sababu tuna ushahidi wa kutosha wa maamuzi yake na gharama ya maamuzi hayo kwa taifa iwe kwenye mali au kwenye maisha ya watu.

Tumeona Lowassa bila ya shaka ni mtu ambaye sababu ya cheo chake anaamini anaweza kuamuru lolote na kufanya lolote hata kama sheria inasema vinginevyo; hatuhitaji na tusije kuwa na Rais wa namna hii. Haijalishi kisingizio chake ni nini cha kutaka kuvunja sheria. Kama kila mtu mwenye sababu ya kweli ya kuvunja sheria angeruhusiwa kuvunja sheria tungeweza kweli kuishi pamoja?

Tumeona Lowassa ni kiongozi ambaye hafikirii kwa mbali sana na kwa kina matokeo (consequences) ya maamuzi yake zaidi ya kujaribu kufanya maamuzi yenye kuleta manufaa fulani ya kisiasa kwake (political expediencies).

Tumeona Lowassa kwa maamuzi yake mwenyewe ya kujiweka na watu wenye kutumia fedha nyingi ili kumsaidia kwenye harambee mbalimbali amejiweka yeye mwenyewe kwenye deni kwao? Siyo kwamba hata hivi sasa anawiwa na watu hawa tusiowajua; atawalipa nini na kivipi?

Kwa ufupi, CCM inajukumu la kuliokoa taifa na Tatizo la Lowassa. Majibu yake mbalimbali kuhusiana na baadhi ya maswala haya hadi hivi sasa hayajaridhisha na hivyo mashtaka haya bado yanasimama. Inawezekana siyo yeye tu lakini kati hawa waliotangaza nia inaonekana yeye ameweka nia yake juu zaidi kuliko wengine kiasi kwamba hata hawezi kukemea vitendo vya kutishia ambavyo vimefanywa na baadhi ya wapambe wake au mashabiki wake. 

Na inaonekana hata ndani ya CCM wenyewe inahitajika ujasiri wa hali ya juu kwa watu kuweza kusimama na kufanya uamuzi wa lazima. Vinginevyo, siyo tu CCM itaonekana kushikiwa kisu kichwani lakini pia inaweza kufanya ionekane imeshindwa sehemu zisizostahili kiasi kwamba hakuna mtu ndani yake mwenye uwezo hata wa kukoa.

Lakini kama CCM itashindwa kumzuia Lowassa – wenyewe wameambiwa kuwa hawawezi kuzuia marufiko kwa mkono – basi tutabakia masalia ambao hata kwa ndimi zetu au kalamu zetu tutajitahidi kuzuia kwani tunajua – ushahidi uko wazi – Lowassa akiwa Rais Tanzania itakuwa kwenye janga jingine la kiutawala kwa miaka mingine mitano. Hili halipaswi kutokea na hatuwezi kuacha litokee kwani kuna vizazi vya Watanzania vinaweza kulipia endapo litatokea. 

SEMA "HAPANA LOWASSA"

7 comments:

Unknown said...

Nadhani kama ilivyo desturi ya nchi yetu, kila mtanzania ana uhuru wa kuongea kile anachokiona kwake kinamantiki kwa hilo sikutilii shaka kwasababu umeonyesha hisia zako bila kificho ila ukumbuke kwamba ukiachana na lowassa ni kiongozi yupi unayemfahamu wewe aliyemkamilifu na hana hata chembe ya RUSHWA? na kama yupo nipo tayari kuungana na wewe katika fikra zako!. Ninachokiona mimi hapo hakuna kiongozi yeyote ndani ya CCM atakayeweza kusimama na kujinadi kuwa yeye ni msafi, HAKUNA kwasababu kila kiongozi anakula kutokana na urefu wa kamba yake. Suala la kumchagulia mtu kiongozi limepitwa na wakati na si muda wa kukariri aliyofanya mtu fulani, swali ni kutathimini je serikali ya CCM imewezaje kuwasaidia watanzania katika kujikwamua na umaskini toka tupate uhuru hadi ivi leo?. ukipata jibu ndiyo utaona kwamba hakuna ukweli wa kuwaaminisha watanzania waone eti mtu fulani hafai. mimi nadhani imefika wakati sasa wa kufanya mapinduzi ya kisiasa kwasababu hata hao unaowaamini wakipewa nafasi iyo ya uongozi ita

Anonymous said...

Lowassa ni fisadi papa, hafai.

Anicetus said...


Mr. Lowaasa was a prime minister because he had the 10 qualities of leadership to transform Tanzania citizen for a better life. With his leadership style, Lowassa is profiting from his charismatic style and people like him regardless of his past decisions. People feel good if a leader is empathetic to his or her audience: Furthermore, Mr Lowassa is profiting from his ability to collectively unite people, and in this approach, his followers are responding to his call like mpiga filimbi wa hamelini.

IBRA THE BRAIN said...

Wewe umekamilika?

Anonymous said...

Mwanakijiji umeshapotea na hata hoja zako zimejaa mapungufu kadha wa kadha. Ukweli utabaki pale pale hakuna mgombea yeyote wa CCM aliye safi, sasa basi katika hali hiyo si ajabu kutafuta shetani mwenye afadhali kuliko wengine. Kwa kifupi, wengi wa viongozi na watia nia wa CCM ni wale waliokatika upande wa wanaofaidi hali ilivyo sasa, na kiuwazi kabisa hali hii sio njema kwa watanzania walio wengi. Kwa hiyo basi, hao watanzania walio wengi wanatafuta shetani mwenye afadhali katika hao watia nia wa CCM, na hii inaletwa zaidi na udhaifu wa upinzani. Sasa basi kama tutamnyooshea kidole Lowassa pekee tunakosea sana, maana Membe, Januari na wangine wameshiriki kuifisadi nchi hii. Kama tunavyojua hao wote wanshiriki katika kula mapande makubwa ya keki ya taifa ama kwa ufisadi au kwa kutumia mipenyo katika sheria zetu kujinufaisha. Sasa basi kwa kuwa wagombea wote wana ufisadi, kwa namna moja ama nyingine, tunaangalia suala la kiutendaji na uthubutu, na hapo ndipo watu kama Lowassa wanapowazidi watu kama Membe, Makamba, Mwigulu ambao wanalaumu serikali ambao na wao ni sehemu ya serikali. Hawa akina Membe, Mwigulu, Makamba na wengine wanashindwa hata kufanya ubunifu katika wizara zao leo hii wanaimba alfu ukela ulela za mabadiliko? Jamani tuache ushabiki, Tanzania ya sasa inahitaji mtu wa kuthubutu na sio watu wa kuhudhuria ofisini bila TIJA

Anonymous said...

Inasikitisha kusikia watanzania kuja na sababu ya kwamba hakuna aliye msafi kwenye ccm kwahio tuende tu na Lowassa. Who have we become? Ni uzembe wa hali ya juu kujaribu kuchagua yule mwenye corruption ndogo badala ya mwenye mafanikio katika historia yake. Hongera Mwanakijiji kwa kujenga hoja ya mshiko.

Anonymous said...

I support the last anonymous post. Its true kuwa hamna mtu msafi, but that doesnt mean tuchague mtu asiye msafi. Watanzania tubadilike. Tusikubali kuongozwa na mtu mwenye historia isiyo nzuri just because siyo kila mtu ni msafi. Asante kwa hii post.