Kiungo mshambuliaji Ramadhani Singano ‘Messi’ akisaini mkataba.
KIUNGO mshambuliaji Ramadhani Singano ‘Messi’, amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Azam FC, ikiwa ni siku moja baada ya kutamkwa kuwa ni mchezaji huru aliyemalizana na Simba.
Singano alisaini mkataba huo jana lakini nyuma ya pazia imebainika kuwa kumbe Simba nayo iliamua kutibua dili lililokuwa likinukia kwa mchezaji huyo kutakiwa kwenda nchini Austria kucheza soka la kulipwa.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffer Idd alisema Singano amesaini mkataba huo na sasa ni mali ya Azam FC.“Tumemsajili akiwa ni mchezaji huru kwa kuwa amemalizana na iliyokuwa timu yake ya zamani, Simba,” alisema na kuongeza:
“Kama ilivyokuwa kwa wachezaji wote wanaoichezea Azam, tumempatia nyumba ya kuishi kama walivyokuwa wenzake kwa kipindi chote atakachoichezea Azam na kesho Ijumaa (leo) ataanza mazoezi ya pamoja na wenzake chini ya kocha wetu, Stewart (Hall).”
Kuhusu dau lililotumika kumsajili ofisa huyo alisema wao siyo kama Simba na Yanga, hawana muda wa kutangaza dau la usajili kwa kuwa hiyo ni siri kati ya mchezaji na klabu.
Wakati Singano akianza maisha mapya klabuni hapo, imeelezwa kuwa Simba iliamua kupotezea mpango wa mchezaji huyo kwenda nchini Austria kwa kuwa dili hilo lilijitokeza wakati kukiwa na mgogoro wa kimkataba.
“Messi alitakiwa Austria kwa ajili ya majaribio lakini ndiyo hivyo mtafaruku umesababisha jamaa walipotezee dili hilo, maandalizi ya awali yalishaanza, visa na mambo mengine lakini baada ya kuibuka mgogoro huo, ndipo jamaa (Simba) wakaamua dili life,” kilisema chanzo kutoka Simba.
Alipoulizwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Simba, Zacharia Hans Poppe juu ya suala hilo alisema: “Ni kweli, kuna timu kutoka Austria ilimtaka lakini sasa hakuna tena kitu kama hicho.”
Singano alikuwa na mgogoro na Simba ambapo awali alisema Simba wamegushi mkataba kwa kuwa ulikuwa ni wa miaka miwili lakini wao wameutengeneza uwe wa miaka mitatu, baadaye akabadili madai na kusema klabu hiyo haikumlipa kodi ya nyumba kama walivyokubaliana katika mkataba, kipengele ambacho kiliiwezesha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumtangaza kuwa mchezaji huru kwa kuwa Simba ilikiuka masharti ya mkataba.
No comments:
Post a Comment