ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 2, 2015

WIZARA YA AFYA ZANZIBAR YAKABIDHIWA MAGARI YA MSAADA TOKA UINGEREZA

Na Makame Mshenga- Maelezo Zanzibar
Shirika la Shistosomiasis Control Initiative (SCI) la Uingereza limetoa Msaada wa Magari mawili aina ya Toyota Double Cabin kwa Wizara ya Afya Zanzibar kupitia kitengo chake cha Maradhi yasiyopewa umuhimu (NTD).

 Akikabidhi msaada huo leo Mwakilishi wa Shirika hilo Dkt. Khalfan Abdallah Mohamed amesema lengo la Msaada huo ni kuiwezesha Zanzibar kupiga hatua katika mapambano yake na Maradhi hayo ambayo yanawaandama watu wengi. 
Maradhi hayo ni pamoja na Matende, Minyoo,Kichocho ambayo ni vigumu kupata Misaada ya matibabu kutoka kwa Wafadhili wa jumuiya za kimataifa.

“Ni rahisi sana kuomba Msaada wa Maradhi kama UKIMWI kwa vile yanapewa kipaumbela na Wafadhili lakini maradhi mengine kama Minyoo au Matende ni vigumu sana kumshawishi mfadhili akasaidia” alisema Mwakilishi huyo wa SCI. 

Amesema Gari hizo ni kwa ajili ya kazi za kitengo cha Maradhi yasiyopewa umuhimu na kwamba zitatumika zaidi katika zoezi la ulishaji Dawa.
 Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo amelishukuru Shirika la SCI kwa mashirikiano ya muda mrefu na Wizara ya Afya kupitia kitengo cha NTD kinachoendesha zoezi la ulishaji Dawa Mashuleni na katika jamii kwa ujumla.

Aidha ametowa wito kwa Mashirika mengine ya maendeleo kuunga mkono jitihada za Wizara ya Afya Zanzibar katika kupambana na Maradhi mbalimbali ambayo yanadhoofisha afya za Wazanzibari kupitia Vitengo mbalimbali.
 Waziri Mahmoud amezipokea gari kwa niaba ya Waizara ya Afya na kuliahidi Shirika la SCI kuzitunza ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa. Gari hizo mbili zitagawiwa ambapo Unguja itabakia moja na Pemba kupelekwa moja ili kusaidia mapambano ya Maradhi yasiyopewa umuhimu.

Imetolewa na Maelezo Zanzibar

No comments: