Nyumba hiyo iliyoteketea iko Mtaa wa Gulam katika eneo la Buguruni Malapa na baba wa familia hiyo, Masoud Matal hali yake ni mbaya. Marehemu hao walizikwa jana katika makaburi ya Kisutu.
Wakizungumza na mwandishi, majirani walisema marehemu hao walikutwa wamekumbatiana baada ya kupiga kelele kwa muda mrefu wakiomba msaada bila mafanikio kutokana na waokoaji kushindwa kupenya nyumba hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lucas Mkondya, alithibitisha watoto watano na watu wazima wanne wamekufa katika kadhia hiyo. Kamanda huyo amesema kwamba chanzo cha moto ni hitilafu ya umeme, lakini alisema uchunguzi unaendelea kufahamu sababu ya moto huo.
Mashuhuda wazungumza
Mmoja wa majirani, Munira Haji alisema alfajiri akiwa usingizini alishtushwa na kelele za watu wakiomba msaada na alipotoka nje, alishuhudia nyumba hiyo ikiwaka moto.
Alisema aliwaamsha watu wa familia yake na kisha kutoka nje kwenda kusaidia kuokoa majirani zake hao, lakini hali aliyoikuta aliishia kulia. Kwa mujibu wa majirani, waliokufa katika ajali hiyo ni mama wa familia hiyo, Samira Mahmoud na watoto wake wanne.
Watoto hao ni Ahmedi aliyekuwa Kidato cha Kwanza, Aisha wa Darasa la Sita, Abdullah mwenye umri wa miaka mitano pamoja na Ashraf mwenye umri wa miaka mitatu.
Alisema wengine ni Wadha (mtoto wa kaka yake Samira) ambaye alikuwa na mtoto mchanga ambaye hakufahamika jina. Pia ndani ya nyumba hiyo, kulikuwa na bibi ambaye alijulikana kwa jina la Bi Mdogo ambaye ni mama mzazi wa Samira. Pia kulikuwa na msichana wa kazi ambaye jina lake halikujulikana.
Kwa mujibu wa majirani, juzi familia hiyo ilitembelewa na wageni kutoka Oman ambao baada ya tukio, ilidhaniwa pia wameteketea kwa moto lakini baada ya miili kutolewa , ilionekana ni watu tisa wa familia moja.
Alisema baada ya kuhangaika kuwaokoa bila mafanikio, Wadha akiwa amembeba mtoto wake , alifika mpaka mlangoni na kurusha funguo nje wafunguliwe lakini majirani walishindwa kutokana na mlango kuwa mgumu huku funguo zikiwa za moto.
“Majirani tuliokuwa nje tulijaribu kufungua lakini hatukufanikiwa na baadaye wanaume walianza kurusha mawe mazito ili mlango uachie lakini bila mafanikio, huku masikini ndani wakiendelea kupiga kelele za kuomba msaada,” alisema.
Mashuhuda wanasema baadaye walisikia mtungi wa gesi ukilipuka kwa nguvu na kufanya mabati ya nyumba hiyo kufumuka na kuruka katika nyumba za jirani. Waliokuwa wakisaidia kutaka kuokoa kila mmoja alikimbia kuokoa maisha yake.
Alisema baada ya kukaa sawa na watu kuanza kurejea, hawakusikia tena sauti za watu ndani ya nyumba hiyo. Vile vile muda mfupi kabla ya mtungi kulipuka, ilielezwa kuwa walisikika watu hao wakisema wamekata tamaa hivyo wanakwenda katika chumba alichokuwa yule bibi wafe pamoja ambako ndiko walikutwa wamekumbatiana.
Zimamoto
Majirani walipiga simu Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji na wengine kukimbilia kituo cha Polisi Buguruni.
“Baada ya kuona hakuna mafanikio ya kuja zimamoto, ikabidi nimpigie simu binamu yangu anayekaa Kariakoo ambaye alichukua bodaboda na kwenda pale Fire Makao Makuu lakini alipofika hapo, walimwambia atangulie nao watakuja, lakini alikataa mpaka walipokuja nao lakini watu ndani walikuwa wameishakufa,” alisema Munira.
Aina ya nyumba
Nyumba hiyo iliyoteketea, ina vyumba vinne na wanafamilia walikuwa wakitumia zaidi mlango wa nyuma. Milango yote miwili ya kutokea nje, ni ya chuma na wakati huo huo madirisha, yana nondo. Miili yao ilitolewa saa 12;00 asubuhi huku mama mwenye mtoto mchanga akikutwa pia amekumbatia mwanawe.
Mashuhuda wanasema viungo vya miili yao ilikuwa ikiokotwa kimoja kimoja. Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Bunguruni Malapa, Karim Malapa, alisema ni msiba mkubwa kwa mtaa wake kuondokewa na watu tisa kwa wakati mmoja na Serikali ya Mkoa inahudumia msiba huo.
Alisema chanzo cha tatizo ni hitilafu kwenye soketi ya umeme. Malapa alisema Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadiki pamoja na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Suleiman Kova, walitembelea eneo hilo na kusema watasimamia gharama zote za msiba.
Baba wa familia
Akizungumzia hali ya baba mwenye nyumba , Imam wa Msikiti wa Ghulaam, Jamaldin Ayub alisema alfajiri wakiwa msikitini na Masoud (aliyefiwa), walisikia nyumba yake ikiwaka moto na walitoka na baadaye kuamua kumrudisha msikitini.
Kwa mujibu Imam huyo wa Msikiti, baba huyo alipotoka alfajiri ya saa 10 kwenda msikitini, aliacha mkewe anataka kuwasha jiko kuandaa maji ya kuoga na kupika uji kwa ajili ya watoto kabla ya kwenda shule.
Alisema alikaa msikitini na wazee wenzake mpaka saa 4 asubuhi walipompeleka kwa ndugu zake katika mtaa wa pili na baadaye aliomba kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kuandaa maiti tayari kwa maziko saa 10 jioni (jana).
Alisema mpaka mchana wa jana, baba huyo wa familia alikuwa bado ameshikwa na bumbuwazi. Maziko Akizungumza baada ya maziko, msemaji wa familia, Suleiman Bashraf alisema walizikwa kila mmoja na kaburi lake kwa kukisia kutokana na miili kuharibika.
Bashraf ambaye miongoni mwa waliokufa yumo mama na dada yake, alisema alivyosikia, tukio limetokana na jiko la umeme waliloacha likiwaka baada ya umeme kukatika hivyo uliporudi uliingiliana na gesi iliyokuwa karibu na kusababisha moto.
Ameomba elimu ya matumizi ya vizima moto iwe inatolewa majumbani kama ambavyo wanavyofanya kwenye magari kuhakikisha vinakuwepo.
Alishauri jamii pia kuwa na utamaduni wa ujenzi wa milango ya dharura ambayo haitaathirika baada ya kutokea moto. Alisema kwa sasa msiba wanaupeleka kwa mjomba wao, Kigogo ingawa baba wa nyumba, bado ana hali mbaya na hawezi kuongea.
Habari Leo
No comments:
Post a Comment