Janet Mwenda
Janet Sosthenes Mwenda ni Mmiliki na Mweneshaji wa kipindi cha 'Ongea na Janet Tv Show' ni mwanahabari mwenye taaluma ya Utangazaji na uandaaji wa vipindi mbalimbali kupitia vipindi mbalimbali vya Radio na Tv huku akiwa ni miongoni mwa watangazaji waliojizolea umaarufu mkubwa kutokana na vipindi vyake vya tv na radio kwa muda mrefu sasa.
“..KAA TAYARI KWA UJIO WA KIPINDI HIKI KIPYA, UNGANA NA JANET KUWALINDA WATOTO WETU!”
(Dar es Salaam). Mmiliki na Mweneshaji wa kipindi cha 'Ongea na Janet' Bi. Janet Sosthenes Mwenda kwa sasa anakuja na ujio mpya wa kipindi kinachoelezea masuala ya kuwalinda Watoto kwa kutoa elimu kiitwacho ‘Tuwalinde Watoto Wetu’ ambacho kinatarajiwa kuonekana kupitia kituo cha televisheni cha Clouds Tv na baadae pia ndani ya chaneli za Dstv.
Tuwalinde Watoto Wetu, kipindi kipya na cha kwanza kwa upande wa televisheni (Tv ambacho kinawatetea watoto moja kwa kwa moja kikiielimisha Jamii jinsi ya kumthamini mtoto, kumlinda na jamii kubadili mtazamo juu ya kundi hili kwa ujumla wake.
Sote tunaamini kuwa, Watoto ambao baadae ndio huja kulijenga Taifa wameonekana ni wadhaifu wanaoshindwa kujitetea hasa pale wanapofanyiwa vitendo vya kikatili, baadhi ya watoto hawa wamebaki na vilema vya kudumu na baadhi wamepoteza maisha kwa mateso na kujiona wakosaji katika dunia hii.
"Watoto wetu wengi wameathirika kisaikolojia inafika mahali wanaona kama wao kufanyiwa ukatili ni sehemu ya maisha yao. Wengine wamebaki na makovu na ulemavu na wengine hata wamepoteza maisha!" Anasema Janet
Swali: Unafikiri hali ya usalama ya watoto imepungua?
Jibu: Sana! Unyanyasaji wa majumbani umeongezeka, ukiacha kupigwa, kutengwa na kupewa majina si yao, kwa mfano kuna wazazi wanawaita watoto wao nyau, mbwa, ng'ombe na mengine yanayofanana na hayo lakini pia wimbi la watoto wetu kubakwa limeongezeka, na wabakaji hawatoki mbali, wanatoka kwenye familia hizohizo, wajomba, akina baba wadogo, walinzi, wafanyakazi na hata wapo akina baba wanaowabaka watoto wao wa kuwazaa! mbaya zaidi hawa watoto huwa wanapata vitisho vikali wasiseme, lakini hata ikigundulika kesi inamalizwa kifamilia bila kujali madhara aliyoyapata mtoto
Lakini pia swala la watoto kutelekezwa limekuwa kubwa, akina baba wamesahau wajibu wao juu ya familia zao, baba anapotelekeza familia hawa watoto wanaathirika na vitu vingi kuanzia afya, elimu na hata kisaikolojia ndio hapo zao la watoto wa mitaani linapokuja au la ajira za utotoni
Swali: Kwanini umefikiria kufanya kipindi kama hiki?
Jibu: (tabasamu) Nafikiri ni Mungu tu ameniongoza kufanya hivi, nikirudi nyuma, kama unakumbuka nikiwa Radio One pamoja na vipindi vingine, nilikuwa naendesha kipindi kilichokuwa kinatoa elimu juu ya kupinga mtoto kuishi katika mazingira magumu, kilikuwa ni kipindi kilichoigusa jamii moja kwa moja na kuleta mabadiliko kwenye jamii.
Binafsi licha ya kuwa muongozaji wa kipindi lakini pia niliguswa moja kwa moja, wakati mwingine nilikuwa napata shida kuongoza kipindi,unakuta unamhoji mtoto,anaelezea njia ngumu alizopitia au anazopita hadi inafika mahali anaanza kulia ,akianza kulia nami udhaifu moyo unaniingia naweka mziki ili nimbembeleze na wakati mwingine nilikuwa nafeli, namimi machozi yananitoka. Ilikuwa inaniuma na siku nzima kwangu haiwi nzuri tena,
Nilipotoka pale, kazi nyingine niliyoipata(Under the same Sun) nayo ililenga watoto moja kwa moja, hawa walikuwa ni watoto wenye Albinisim. Kitendo cha watoto wengi kutelekezwa au kutaliwa na wazazi wao kilikuwa kinaniumiza sana na kama haitoshi wengine wakawa wanauawa kitendo hiki kinaniumiza zaidi na ninakikemea kutoka moyoni.
Kama hiyo haitoshi, pamoja na kuamua kujiajiri nikaitwa tena na kampuni ya True vision ambao wanashirikiana na Wizara ya maendeleo ya jamii jinsia na watoto nikafanye tena vipindi vya watoto. Hapa sasa ndipo nilipoona Mungu anataka nifanye kitu cha ziada juu ya watoto,siku moja nikajikuta najiuliza kwanini nisifanye kipindi cha TV ili watu waone kinachoendelea? kama ni kusikia wanasikia kila siku na wanasoma habari za watoto zisizopendeza kila siku,sasa umefika wakati watu waone kwa macho. Nikafanya research,nikagundua hakuna kipindi cha aina hii kwenye Tv yoyote hapa nyumbani Tanzania nikaona bora nianzishe kitu kama hiki,nikiamini na wenzangu wataniunga mkono baadae na wao kutoa elimu kupitia Runinga baada ya Radio na Magazeti.
Swali:Hiki kipindi kitarushwa TV gani?
Jibu: Clouds TV, nashukuru Mungu nilipoenda na kipindi changu kilipokewa kwa mikono miwili na hiyo ikanipa moyo zaidi na kuona nimefanya uamuzi sahihi lakini pia baadae kitaruka kupitia DSTV
Swali: Tulikuzoea kwenye "Ongea na Janet" ,sasa unarudi na "Tuwalinde watoto wetu" vipi kuhusu Ongea na Janet umekiua?
Jibu: (kicheko) sijakiua,kipo na kitarudi msimu wa tatu October,nilichokifanya ni kuangalia,kipi nikipe uzito kwanza, nikaona watoto wamesahaulika katika matatizo yao hasa kwa upande wa Tv,hata ikitokea habari mbaya hata iwe ni ya kuogofya lakini haitatangazwa kwa muda mrefu au kufuatiliwa kwa undani. Nimeona ni jukumu langu na kama nilivyosema nina sauti inayonisuta na najiona mwenye kosa kuchelewa kulifanya hili,nahisi nadaiwa na hawa watoto na huko kote nilikopitishwa nilikuwa naambiwa ni jukumu langu kuielimisha jamii kuhusu thamani ya mtoto na ulinzi wake.
Swali: Una lolote la kumalizia?
Jibu:Ndio, hiki kipindi ni muhimu sana kwa wakati tuliopo,hatuwezi kuwa na Taifa bora kama hatujatengeneza msingi huku chini,vitendo vingi vibaya wanavyofanyiwa watoto vinakuja kuzaa Taifa lenye hasira,chuki,visasi na dharau. Hii inatokana na ukatili aliofanyiwa mtoto,na mtoto huyu akakua na maumivu ambayo anapokuwa mkubwa anajikuta analipiza kwa wengine,au kwa kujua au kwa kutokujua,kwa mtindo huu tusitegemee kuwa na Taifa lenye upendo, wote tunajua pasipo na upendo pana chuki na mazalio ya chuki tunayafahamu.Pamoja na hayo tusitegemee watoto hawa baadae waje kuwa wazazi bora,haitawezekana.Hivyo nawaomba sana wananchi wakiangalie hiki kipindi ili waone na kujua hali halisi ya mambo ambayo wengi bado hatufahamu juu ya usalama wa watoto wetu,itasaidia kutubadili sisi sote na kufanya yafaayo kwa watoto wetu
No comments:
Post a Comment