ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 18, 2015

KILA ALIYEJIANDIKISHA ANA WAJIBU WA KUPIGA KURA

Jaji Mstaafu, Damian Lubuva.

Kwanza nimshukuru Mungu kwa kuweza kutupa uhai leo na kujiona tuko katika nchi yetu iliyojaa amani.

Naamini kwamba katika maeneo yote ya nchi, wazalendo wa nchi hii walijitokeza bila kulazimishwa kwenda kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (BVR)kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25.

Mkoa wa mwisho kuhitimisha rasmi kazi hiyo iliyoanza kwa kusuasua mwanzoni mwa mwaka huu ni Jiji la Dar es Salaam.Kabla ya uandikishaji, tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ilikuwa imekadiria kwamba mwaka huu kutakuwa na watu milioni 24 wenye sifa za kujiandikisha na hatimaye kushiriki katika uchaguzi huo wa kuwachagua madiwani, wabunge na rais.

Kwa dalili zinavyojionesha, idadi hiyo ya watu milioni 24 inaweza isifikiwe kwa sababu ya matatizo yaliyojitokeza wakati wa uandikishaji ambayo yaliwakatisha tamaa baadhi ya watu kutokana na usumbufu uliokuwepo.
Hata hivyo, kama idadi hiyo itakaribiwa, itakuwa si haba na jambo muhimu baada ya hapo ni waliojiandikisha kuhakikisha kila mmoja anapiga kura. Unapopiga kura ndipo unapoonesha uzalendo wako, kwani unasababisha kupatikana kwa kiongozi bora, usipopiga kura elewa kwamba unachangia kwa kiwango cha juu kusimika viongozi wasiofaa katika nchi hii yenye changamoto nyingi za maendeleo.

Nimesema hivyo kwa sababu kumeanza kutokea tatizo la watu kutotaka kupiga kura na badala yake kutumia zoezi la uandikishaji kupata vitambulisho tu, yaani ile kadi ya mpiga kura kugeuzwa kitambulisho.
Nilisikitika sana kuona katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, zaidi ya nusu ya waliojiandikisha kupiga kura hawakupiga kura, hii ilinisikitisha sana na kwa kweli yule ambaye hakupiga kura ajiambie katika nafsi yake kwamba hakuitendea haki nchi yetu.

Hili ni tatizo kwa sababu kila aliyejiandikisha anatakiwa kupiga kura. Kutopiga kura maana yake ni kuacha masuala muhimu ya nchi yaamuliwe na wachache badala ya walio wengi na ambao hawakupiga kura wakati walikuwa wamejiandikisha mwaka 2010 wajue kwamba walichangia kupata viongozi wabovu katika nchi hii.

Najua kwamba zoezi la uandikishaji wapiga kura ulikuwa na kasoro nyingi na za kukera kwa wananchi waliojitokeza. Baadhi ya matatizo hayo yalikuwa ya kujirudia kiasi kwamba wengine walianza kuhoji kama wahusika wanajifunza kutokana na mwenendo wa mchakato mzima wa uandikishaji.

Naamini kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi chini ya Jaji Mstaafu, Damian Lubuva na serikali kwa ujumla itakuwa imejifunza kutokana na mchakato huu na taifa litajiepusha na mkanganyiko kama huu kwenye chaguzi zijazo.
Binafsi nitafurahi kuona idadi kubwa ya waliojiandikisha kupiga kura wanafanya hivyo. Tunajua kuwa katika chaguzi nyingi duniani, si rahisi kwa watu wote waliojiandikisha kupiga kura wapate fursa ya kupiga kwa sababu tofauti.
Lakini, kama tunavyoona kwa jirani zetu wa Kenya, tunaweza walau kupata wapiga kura waliofika asilimia 75 ya waliojiandikisha.

Katika baadhi ya nchi za wenzetu, wako wananchi ambao husafiri kutoka Ulaya na Marekani kwa lengo la kuwahi kupiga kura nchini mwao, huo ni uzalendo ambao nasi tunatakiwa kuujenga.Watanzania hawawezi kuacha kupiga kura kwa sababu yoyote ile. Kama unataka kiongozi unayemtaka ashinde katika uchaguzi, unatakiwa kupiga kura.

Watu wengi wakipiga kura, hata uongozi unaoingia madarakani unakuwa na amani kwa vile unafahamu umeingia kwa mamlaka ya walio wengi. Ndani ya moyo wako weka dhamira kwamba ‘uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni lazima nipige kura’, vinginevyo wote watakaoacha kupiga kura wataonekana ni wasaliti wa nchi yao wasio wazalendo.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

GPL

No comments: