ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 14, 2015

Lipumba sasa rasmi CCM

LIPUMBASRichard Manyota na Oscar Ndauka, GPL
SIKU chache baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Haruna Lipumba kujiuzulu wadhifa wake huo, sasa mwanasiasa huyo mtaalamu wa mambo ya uchumi ametajwa waziwazi kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Uwazi Mizengwe ya Uchaguzi limedokezwa.

Chanzo chetu cha habari kimesema Prof. Lipumba alifikia uamuzi huo hivi karibuni jijini Dar es Salaam baada ya kupata ushawishi mkubwa kutoka kwa viongozi waandamizi wa CCM, rafiki zake wa karibu wenye mapenzi na chama hicho tawala pamoja na baadhi ya maofisa usalama wa taifa.

“Mtu wa kwanza kabisa kumshawishi Lipumba ni… (anamtaja kwa jina kigogo mmoja wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, NSSF ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sasa kwa vile hakupatikana kuzungumzia jambo hili). Alipofanikiwa alimkabidhi kwa viongozi wa chama ambao walimpokea.

“Kigogo huyo wa NSSF anatajwa kuwa rafiki yake mkubwa na wa miaka mingi kiasi cha kuwa kama ndugu kutokana na ukaribu wao.


APEWA AHADI YA UWAZIRI

“Kwa kuwa profesa ni mchumi, walikubaliana na viongozi wa CCM kuwa ikishinda kwenye uchaguzi mkuu ujao (Oktoba) itamteua yeye (Lipumba) kuwa waziri wa fedha,” kilieleza chanzo chetu kutoka ndani ya CCM na kuongeza:

“Ilibidi wakubaliane hivyo kwa sababu si unajua profesa ni mtaalam wa kimataifa wa uchumi! Kwa hiyo nafasi hiyo inamfaa sana kuliko nyingine.

“Hata safari ya mwenyekiti huyo wa zamani wa Cuf kwenda Kigali, Rwanda kwa kile alichosema mwenyewe eti ni kwa ajili ya kufanya kazi ya utafiti, iliandaliwa na CCM kwa kushirikiana na Serikali ya Rwanda. Lengo kubwa ya ile safari ni profesa kwenda kupumzika kwa muda ili atakaporejea iwe ni kutangaza tu.”

PICHA MITANDAONI ZAZUA MASWALI

Katika hali iliyoonesha ni kuyapa nguvu madai hayo, chanzo chetu kilizungumzia pia baadhi ya picha zilizozagaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii zikimuonesha Lipumba na kijana mmoja wakiwa hotelini jijini Kigali wakipata vinywaji.

“Yule kijana aliyepiga picha na Lipumba nchini Rwanda mimi namfahamu, ni rafiki mkubwa wa familia ya Rais Jakaya Kikwete. Sisi huwa tunamwita kwa jina la utani la Kibakuli. Tunamfahamu kama afisa usalama wa taifa.

“Halafu mbaya zaidi kuna picha amepiga na viongozi wa juu wa CCM. Sasa hapo kwa kupiga picha na Lipumba wakiwa nje ya nchi we unadhani kimebaki nini?” kilihoji chanzo chetu.

CHOMBO CHA HABARI CHATAJWA

Mbali na kutoa ufafanuzi huo, chanzo chetu kiliendelea kudai kuwa, mpango wa Lipumba kujiuzulu nafasi ya uenyekiti ulifahamika mapema ndani ya CCM ndiyo maana gazeti linalomilikiwa na chama hicho tawala la Uhuru la Agosti 5, mwaka huu lilikuwa la kwanza kuripoti habari hiyo kabla ya Prof. Lipumba kutangaza rasmi siku iliyofuata.

“We hata ukitumia akili ya kawaida tu utajua. Kwa nini Gazeti la Uhuru liwe la kwanza kuripoti ile habari? Ni kwa sababu wao ndiyo wenye chama kwa hiyo walijua mapema. Uongozi wa Cuf ulikanusha, wengine walitaka gazeti hilo lifungiwe kwa kuandika uongo lakini siku moja mbele, Lipumba mwenyewe pale Peacock Hotel akasema amejiuzulu uenyekiti,” kilisema chanzo hicho.

ALICHOSEMA LIPUMBA MWENYEWE

Kwa upande wake, Prof. Lipumba alieleza hatua yake ya kuachia ngazi ya uenyekiti wa Cuf kuwa ni uamuzi wake binafsi uliotokana na yeye kuonekana kikwazo cha mustakabali wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Cuf, NCCR-Mageuzi na NLD na kwamba hakuwa tayari kuona taratibu walizojiwekea zikikiukwa.

Kwa maana hiyo, kwa mujibu wa chanzo chetu, Lipumba alijua anapindisha ukweli kwa kulalamikia mchakato mzima wa Ukawa katika kusimamisha mgombea urais ambapo wenzake walimkubali Edward Lowassa aliyehamia Chadema kutoka CCM hivi karibuni.

Kwa upande wa CCM, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Moses Nnauye hakupatikana kuzungumzia habari ya Prof. Lipumba kuhamia kwenye chama hicho lakini mara kadhaa amekuwa akinukuliwa akisema kuwa hawapo tayari kupokea makapi.

KADA MWINGINE WA CCM


Naye mwanachama mwingine wa CCM ambaye aliomba hifadhi ya jina lake, alipozungumza na Uwazi Mizengwe kuhusu madai ya Lipumba kujiunga rasmi na CCM, alikuwa na haya ya kusema:

“Hiyo kwetu siyo kazi kubwa. Unajua CCM ni chama tawala. Hilo lazima watu walijue. Lipumba alitoka CCM kwenda Cuf. Kwa hiyo amerejea CCM. Si yeye tu, Dk. Willbroad Slaa naye alitoka CCM, akaenda Chadema. Hata mwenye chama cha Chadema (anamaanisha Edwin Mtei, mwanzilishi) naye alitoka CCM.

“Kwa hiyo kama ni maajabu ni mtu wa CCM kuhamia upinzani lakini si mpinzani kuamua kurudi kwenye chama chake kilichomlea. Kwa mfano Lowassa kuhamia Chadema ndiyo iwe gumzo japo kuhama kwake si tishio kwa CCM. Sasa Lipumba kuja CCM gumzo lake ni nini?” alihoji kada huyo.

Akaendelea: “Unajua watu hawajui kitu kimoja. Hawa viongozi wa upinzani, karibu wote bado wana kadi za CCM. Hii inamaanisha nini?

Wanajua kuna siku watarudi nyumbani.”

TUNDU LISU AILIPUKIA CCM

Naye Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alipozungumza na gazeti hili juu ya uwepo wa taarifa hizo, alisema:

“Si jambo la ajabu Lipumba kuhamia huko kwa sababu tunajua kuwa CCM wanafanya kila mbinu kuihujumu Ukawa. Ila wafanye wafanyavyo mwisho wao wa kuwa madarakani umefika na mwisho ni Oktoba mwaka huu.”

6 comments:

Anonymous said...

Shemeji ndo kamrabisha CCM

Anonymous said...

Tulijuwa tangu mwanzo

Anonymous said...

Hana Lolote akazikwe na ccm.

Anonymous said...

Hilo halitarudisha msimamo nyuma. Wazi kabisa alichukua mshiko mkubwa tu toka CCM na ndio mwisho wake ulingoni mwa siasa. Pumbaahh pumbahh.

Anonymous said...

Kigogo wa NSSF ? Kigogo umeutoa wapi NSSF ?

Anonymous said...

Lipumba Kama pumba