ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 29, 2015

Mwakyembe Amshambulia LOWASSA Kuhusu Sakata la Richmond Mwigulu Nchemba naye Adai Lowassa Ni Mpiga Dili Tangu Kijana


Mwakyembe Akihutibia Umati
Aliyekuwa mwenyekiti wakamati teule ya bunge ya kuchunguza kashfa ya mkataba tata wa Richmond iliyomuondoa madarakani aliyekuwa waziri mkuu Mh Edward Lowassa, Mh Harrsion Mwakyembe amewahakikishia watanzania kuwa walijiridhisha pasipo shaka kuhusika kwa Edward Lowassa katika sakata la Richmond na kwamba hawakumsingizia kama anavyojitetea hivi sasa.
Mwakyembe aliyasema hayo mbele ya maelfu waliojitokeza katika mkutano wa hadhara wa mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli katika viwanja vya Luandanzovwe jijini Mbeya, jana.

Akizungumzia madai ya kwa nini baadhi ya wahusika hawakupelekwa mahakamani kama kuna ushahidi, mhadhiri huyo wa sheria alisema kosa la jinai, halina ukomo na wakati wowote linaweza kufunguliwa mashitaka, huku akiapa kuwa anaweza kumfungulia mtu mashitaka hata kesho.

Alionya viongozi na makada wa Chadema na vyama vinavyowaunga mkono katika umoja wa Ukawa wanaozindua kampeni zao leo jijini Dar es Salaam, kwamba wasithubutu kujibu hoja zake.

Dk Mwakyembe alisema ikilazimika kusema ukweli, ataweka hadharani uchafu wote uliofanyika, ambao alisema bungeni kuwa asingeuanika na kuifanya Richmond hoja ya kila siku mpaka Watanzania waelewe kilichofanyika.

“Tunao ushahidi. Hawa walitakiwa kuwa jela badala ya kuimba nyimbo za ajabu,” alisema Dk Mwakyembe katika mkutano huo uliorushwa moja kwa moja nchi nzima na kuongeza kuwa Dk Magufuli akiingia madarakani, anakwenda kuanzisha Mahakama ya Ufisadi.

Alisema yeye na wenzake walipewa kazi ya Bunge kuchunguza ilikuwaje viongozi waandamizi wakaamua kuipa kampuni hewa zabuni ya mabilioni ya fedha, ambayo imesababisha mpaka leo kuna shida ya umeme nchini.

Dk Mwakyembe alikumbusha kuwa walikwenda mpaka Marekani kuchunguza uwepo wa kampuni hiyo iliyodaiwa kutoka katika nchi hiyo, na kukutana na kampuni ya kuchapisha kadi za harusi.

Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, baada ya kubaini ubadhirifu huo, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alishinikizwa kujiuzulu na kumaliza suala hilo na hivyo hatua ya kiongozi huyo kutaka kwenda Ikulu, wazalendo hawawezi kuikubali.

“Hatutaruhusu watumie demokrasia kuingia Ikulu na hiyo ndiyo shida ya kuazima wagombea,” alisema Dk Mwakyembe akimaanisha kuwa chama cha Chadema, kimeazima mgombea bila kumfahamu.

Dk Mwakyembe alisema suala hilo lilishafungwa bungeni, lakini anashangaa kusikia linarejeshwa kinyemela.

Mwigulu
Naye Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Mwigulu Nchemba, alisema mgombea wa Ukawa, Lowassa, tangu akiwa kijana alikuwa ‘mpiga-dili’.

Kwa mujibu wa Mwigulu, Rais Kikwete alipoingia madarakani, alidhani kuwa Lowassa alikuwa ameonewa, akamteua kuwa Waziri Mkuu, lakini kabla ya kumaliza miaka miwili, akaendeleza tabia yake ya ‘kupigadili’.

Mwigulu alionya kuwa, Watanzania wakimpeleka ‘mpiga-dili’ Ikulu, shida yake na wenzake si changamoto za watu wa Mbeya wapate maji, huduma bora za afya na nyingine bora za umma, bali kurejesha fedha walizotumia wakati wa kutafuta urais.

“Mkimpeleka mpiga dili Ikulu, ‘wapiga-dili’ wenzake hawatalipa kodi, mtalipa nyie wanyonge ili wale ‘wapigadili’ warejeshe fedha zao,” alisema na kufafanua sababu za vyama vya Chadema, CUF, NCCRMageuzi na NLD kuungana pamoja katika Ukawa.

Kwa mujibu wa Mwigulu, kilichowaunganisha ni maslahi ya aina mbili; moja aliyetoa fedha kwa ajili ya kwenda Ikulu, ambaye anatafuta nafasi hiyo ili arejeshe madeni yake na wengine ni waliouza vyama ambao ‘wameshakunja’ chao.

“Nawaambia mwisho wa mbwembwe na maigizo, ni Oktoba 25 na baada ya hapo ni kazi tu,” alisema Mwigulu na kuhoji iweje Lowassa apande daladala leo, ambalo hakulipanda miaka 40 iliyopita?

Mwigulu alisema Watanzania wana siku 60 za kujadili hatima ya taifa lao na katika hilo, hakuna namna zaidi ya kuelezana ukweli mtupu.

8 comments:

Anonymous said...

Asante sana kwa ufafanusi huu mheshimiwa. Hii ndiyo sababu tunashindwa kupigia kura CCM maana you failed us. Huu uchaguzi sio CCM itakachokifanya bali ilichokifanya (results based). Kama makosa kama hayo mliyajua na mkakaa kimya na sasa mnaongea ili kupata kura ni nyie mnakiangusha chama. kwangu mie, kama yaliyosemwa hapo juu ni kweli, then you are just as guilty kwa sababu Watanzania waliwapa resposibilities na mkashindwa kazi. Pia kumbuka, it takes two to tangle.

Anonymous said...

Acha unafiki ww ulishasema bungeni mambo unayasitili kuinusuru sirikali, Kama ww ni mkweli kaulize kiwete Hilo card printing alilijulia wapi?toka EL kumfanyia fitina na kujiuzuru, tumeona kivuko feki, mabehewa yako, meno ya tembo na escrow waliochukua hela stanbic ni akina nani. Bado hakuna dawa, elimu duni kila kitu kinaenda kombo hiyo PhD yako itakuwa na walakini.

Anonymous said...

Mwigulu maneno yako hayatofautiani na ya NAPE AU MKAPA na umetufikisha hapo unapotaka. Makyembe una ya kujibu mbele ya haki usione unalo la ziada umefunika mambo.mengi sana ndani ya serikali hiii na nin
mwiba kwa wananchi. menginsanaUnataka kuendelea hadi lini??? Nani asiyewajua kuwa mnatetea unga wenu mnaoona unaingia vumbi ili muendelee kuwatesa waTanzania!!!

Anonymous said...

Tatizo sio Lowassa bali ni ccm yenyewe. Tokea Lowassa kujiuzulu hivi ufisadi umemaliza? au ndio ulizidi?? Kama umezidi basi tatizo kuu ni CCM sio Lowassa.

Anonymous said...

Mwakyembe huna jipya...same politics as usual

Anonymous said...

Mwakyembe anamengi ya kuwaeleza watanzania kuhusu sakata la Richmond . Kwanza tunataka kujua nani alimlisha sumu karibu kupoteza maisha yake wakati anashughulikia hilo sakata la Richmond.

Anonymous said...

Wenzetu mnaoshabikia ufisadi mlie tu. Watanzania hawajakata tamaa kiasi cha kukabidhi nchi yao kwa UKAWA, ambao wamejidhihirisha kuwa ni genge la wapiga dili na wasanifu wa siasa za ukabila/ukanda. Poleni UKAWA; Tanzania ya Nyerere na Karume haikuasisiwa kwa misingi hiyo!

Anonymous said...

Ukisoma vizuri alichokisemwa Mwakyembe,utagundua kuwa hasemi ukweli... Anasema swala la Richmond liliishia bungeni hivyo wapinzani wasiliongelee tena. Lakini akaongeza kuwa kama watu wanataka aseme ukweli,basi atafanya hivyo. ... Ulio wazushia ndio hao hao wanaotaka kuyazungumzia uliyo wasema,lakini wewe unakataa wasiyarudishe kwenye majukwaa. Kuna kitu kimejificha ndani ya hii Richmond,ambacho yeye hataki watu wakijue. ... Je Mh,aliitwa nakuojiwa?...Ninapata shida kidogo na maneno yako. Ndugu Mwakyembe.