
Dar es Salaam. Wakati timu mbalimbali za Ligi Kuu nchini zikiendelea kukamilisha usajili kwa ajili ya kuimarisha vikosi vyao msimu ujao, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa mpaka sasa zaidi ya Sh1.5 bilioni zimetumiwa kwa wachezaji wao.
Kiasi hicho cha fedha kimetumika kuwasajili wachezaji wapya pamoja na kuwaongezea mikataba wachezaji ambao mikataba yao ilikuwa ikikaribia kumalizika.
Katika gharama hizo, Yanga inakadiriwa kutumia zaidi ya Sh 800 milioni, ambazo ni sawa na asilimia 53.33 ya kiasi chote cha fedha zilizotumika na klabu 16 kwenye usajili msimu huu.
Nyota wa Yanga walioongezewa mikataba na gharama zao ni Mbuyu Twite, Dola 25,000 (Sh52 mil), Haruna Niyonzima (Dola 70,000), Deogratius Munishi (Sh10 mil), Simon Msuva (Sh 25 mil).
Wapya ni Deus Kaseke ( Sh35 mil), Malimi Busungu (Sh25 mil), Haji Mwinyi (Sh25m), Matteo Simon (Sh20 mil), Benedicto Tinoco (Sh5 mil) na Geofrey Mwashiuya (Sh 10 mil).
Wachezaji wengine na fedha zao kwenye mabano ni Joseph Zuttah (Dola 30,000), Amissi Tambwe (Sh40 mil), Donald Ngoma (Dola 50,000) huku wapya, ambao ni, Mudathir Khamis, Thabani Kamusoko na Vicent Bossou wakitajwa kuigharimu klabu hiyo zaidi ya Sh250 milioni za Kitanzania.
Klabu ya Mwadui ya Shinyanga ambayo msimu huu imepata udhamini wa Kampuni ya Acacia Mining inafuatia kwa mbali baada ya kutumia asilimia 20 ya gharama za jumla za usajili wa wachezaji.
Kwa upande wake imetumia Sh300 milion kuwanasa, Maregesi Mwangwa, David Luhende, Anthony Matogolo, Razack Khalfan, Nizar Khalfan, Jabir Aziz ‘Stima’, Rashid Mandawa, Zahoro Pazi na Paul Nonga. Pia, imewaongezea mikataba Athumani Iddi ‘Chuji’, Kelvin Sabato, Bakari Kigodeko na wengineo.
Simba na Azam zimetumia zaidi ya Sh 400 milioni katika kipindi hiki cha dirisha la usajili. Simba imewaongezea mikataba Said Ndemla (Sh35 mil), Hassan Isihaka (Sh 30 mil) na kipa Ivo Mapunda.
Pia, imewasajili Mohamed Fakhi, Peter Mwalyanzi, Samih Nuhu, Emery Nibomana, Mussa Hassan ‘Mgosi’, Mwinyi Kazimoto kwa zaidi ya Sh100 m, huku pia ikiwa mbioni kuwasajali Danny Lyanga, Justice Majabvi na Vincent Angban, ambao gharama zao hazipungui Dola 80,000.
Azam imemsajili Ramadhani Singano ‘Messi’ kwa kiasi kinachotajwa kufikia Sh50 mil, Ame Ally (Sh25 mil), Mkenya Allan Wanga akigharimu kiasi kinachokadiriwa kufikia Dola 30,000, imewaongezea mikataba Erasto Nyoni, Didier Kavumbagu na Said Morad.
Kiasi hicho kilichotumiwa na Simba na Azam, ni asilimia 27 ya jumla ya fedha zote zilizotumiwa na timu zote 16 zitakazoshiriki Ligi Kuu msimu ujao.
Licha ya kutotaka kuweka wazi gharama ambazo zimetumiwa na timu zao kwenye usajili, gazeti hili limebaini kuwa usajili uliofanywa na timu nyingine, tofauti na Simba, Yanga, Azam na Mwadui, umezigharimu kiasi cha zaidi ya Sh140 mil za Kitanzania.
Gharama hizo za usajili zimeonekana kuwashtua wadau wa soka nchini ambao wamezitaka timu pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuangalia ni kwa namna gani wanaweza kutengeneza mfumo bora utakaofanya timu zisitumie gharama kidogo kwenye usajili wao.
Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, Angetile Osiah aliliambia gazeti hili kuwa matumizi ya gharama kubwa kiasi hicho kwenye dirisha hili la usajili, yanatakiwa yatoe funzo kwenye soka la Tanzania.
“Timu zetu zinafanya usajili wa gharama huku zikiwa hazina njia ya kuwaingizia kipato. Wanaangalia zaidi kutumia leo pasipo kufikiria kesho itakuwaje. Sasa hivi umeanzishwa mfumo wa usajili wa klabu ambao unazilazimisha timu kuwa timu ya vijana pamoja na uwanja wake wa mazoezi.
“Matokeo yake shirikisho ambalo lilipaswa kuzihimiza timu, lenyewe ndio linazikaribisha kufanya mazoezi. Tunaendelea kulea wenyewe uozo ambao unazidi kuzifanya klabu zetu zisipate mendeleo,” alisema.
Alizishauri timu na TFF kukaa chini na kutafakari kuona wanawezaje kuondoa mfumo uliopo sasa ambao unakandamiza maendeleo ya soka letu.
Ofisa Habari wa Kimondo FC ya Mbeya inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, Christopher Kashililika alisema kuwa kuna usanii mkubwa unaofanywa na timu kwa sasa hadhani kama fedha zote wanazopata wachezaji zinawafia na badala yakekuna viongozi ambao hupata cha juu kupitia fedha hizo za usajili.
“Gharama hizo zilizotumika ni kubwa, lakini naamini hukuzwa na baadhi ya viongozi wa timu ili nao wapate fungu. Unakuta kiongozi anatangaza kuwa wamemsajili mchezaji kwa Sh20 mil, lakini ukweli ni kuwa mchezaji amepewa Sh10 au 15M, sasa hizo nyingine zinapelekwa wapi?” alihoji Kashililika.
Alisema kuwa hali hiyo inafanya wachezaji wajione wenye thamani kubwa kuliko uwezo wao. Kuwapo na kanuni zitakazoleta uwiano kipindi cha usajili sanjari na kuwakata kodi wachezaji kwa kila fedha ya usajili pamoja na mshahara.
No comments:
Post a Comment