WIZARA YA KAZI NA AJIRA
1.
Serikali imepata taarifa za kuwepo kwa mpango
wa mafunzo kwa madereva nchini kote, ulioandaliwa na Chama cha Wafanyakazi
Madereva Tanzania-Tanzania Drivers Workers Union (TADWU) kuanzia wiki ijayo.
Mpango huo umeelezwa kuwa njia mbadala ya tishio la mgomo lililotolewa na
viongozi wa Chama hicho hapo awali, ili kuweza kupata suluhisho la malalamiko
yao.
Malalamiko hayo yalihusu Mkataba ya Ajira inayokidhi matakwa ya kisheria,
nyongeza ya posho na viwango vya mishahara juu ya kima cha chini cha mshahara
kwa sekta ya usafirishaji na kero nyinginezo za barabarani.
2.
Taratibu za Chama kuendesha mafunzo na
shughuli nyinginezo za kichama katika sehemu za kazi kwa mujibu wa Sheria ni kama
ifuatavyo:-
(i)
Wawakilishi wa Vyama vya wafanyakazi wanayo
haki ya kuwaarifu Waajiri na kuingia katika eneo la kazi ili kuandikisha
wanachama, kuwasiliana na wanachama wao, kukutana na wanachama kujadili masuala
yanayohusu mahusiano na Waajiri wao au kwa ajili ya kufanya chaguzi au upigaji
kura kwa mujibu Katiba za Vyama vyao.
(ii)
Katika kutekeleza haki hiyo, ni lazima
Wawakilishi hao wa Vyama wapate ridhaa ya Waajiri kwa kuzingatia vigezo na
masharti (utaratibu) yanayolenga kulinda maisha ya watu na mali au kuzuia
uvurugaji wa taratibu za kazi au utendaji kazi,
(iii)
Vyama vya Wafanyakazi vina haki ya kutoa
mafunzo katika sehemu za kazi ambazo kuna matawi yake au kuna wanachama wake
wanaotambulika kisheria.
3.
Baada ya kutafakari taarifa hiyo ya viongozi
wa TADWU na kuzingatia matakwa ya Sheria za Kazi nchini, Serikali imejiridhisha
kwamba, taarifa iliyotolewa na uongozi wa TADWU imekiuka matakwa ya Sheria za
Kazi. Taarifa hiyo haikuwasilishwa kwa Waajiri husika sehemu ya kazi, ambao
TADWU ina wanachama wake inaokusudia kuwahusisha kwenye mafunzo hayo.
Taarifa
hiyo haikubainisha ni wafanyakazi gani, wala idadi ya wafanyakazi hao
watakaohusika na mafunzo hayo. Hakuna ratiba iliyoidhinishwa na Waajiri,
inayohakikisha kuwa hakuna chombo cha usafiri kitakachosimama kufanya kazi na
kuepusha usumbufu kwa watumia huduma.
4.
Hivyo, Serikali inasisitiza na kuwakumbusha
viongozi wa Chama hicho cha TADWU na madereva kwa ujumla, kutekeleza majukumu
yao kwa kuzingatia matakwa ya Sheria za Nchi na kujiepusha na vitendo
vinavyohatarisha usalama wa mali na maisha ya watumia huduma. Aidha, watambue
kuwa umakini wao ni muhimu katika kuepusha hatua ambazo zina uelekeo wa
kudumaza shughuli za kijamii na kiuchumi nchini.
5. Kushiriki katika mafunzo yaliyoelezwa na viongozi wa
TADWU kwa utaratibu walioueleza ni sawa na kuitisha au kufanya mgomo usio
halali.
6.
Serikali imefanya
jitihada mbali mbali za kuwaelimisha na kuwaelekeza, ikiwemo semina, mafunzo,
ushauri na kugawa vijarida/vipeperushi. Elimu hiyo ilihusu taratibu za
majadiliano ya pamoja ya kuboresha maslahi na utendaji kazi na utatuzi wa
migogoro ya kikazi kisheria ili kuepusha madhara na usumbufu usio wa lazima kwa
wanachi wasio husika na utatuzi wa malalamiko yao.
7.
Hitimisho: Serikali inapenda
kutoa wito kwa Wamiliki wa vyombo vya usafirishaji, viongozi wa vyama vya
wafanyakazi vya madereva pamoja na madereva wote nchini kutekeleza makubaliano
yaliyokwishafikiwa hadi sasa katika vikao vya Kamati ya Waziri Mkuu. Aidha,
Serikali pamoja na Taasisi zake itaendelea kutoa elimu pamoja na kufuatilia
makubaliano yaliyofikiwa na hatua za kisheria zitachulikwa dhidi ya wale
watakaokiuka utekelezaji wa makubaliano hayo.
Eric
F. Shitindi
KATIBU MKUU
20/08/2015
No comments:
Post a Comment