Advertisements

Saturday, August 15, 2015

Waziri atembeza mkong’oto, wengine wawili waanguka

Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk Titus Kamani

Dar/Makete. Mawaziri wawili wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete wameanguka kwenye marudio ya kura za maoni zilizofanyika juzi, huku matokeo ya Jimbo la Busega yakikwama baada ya Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk Titus Kamani kumshambulia msimamizi wa uchaguzi.
Walioanguka ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid (Rufiji) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mazingira), Dk. Binilith Mahenge (Makete), huku Dk Raphael Chegeni akiongoza kwenye Jimbo la Busega.
Vurugu kubwa Busega
Hali ilikuwa mbaya jimboni Busega ambako baada ya Dk Kamani na wafuasi walizuia matokeo kutangazwa na kuibuka kwa vurugu zilizosababisha polisi kuingilia kati na kukamata watu wanne walioonekana kumuunga mkono.
“Napigania haki yangu,” alisema Dk Kamani baada ya kutulia kwa vurugu ambazo zilihusisha kupigwa kwa msimamizi wa kura hizo za maoni, Jonathan Mabiya.
“Huu ni ushindani. Uchaguzi uliopita tulikubaliana na matokeo na tulisaini, lakini uongozi umesema turudie, leo hatujasaini wanataka kutangaza kwa nguvu, hatujakubaliana.”
Mkuu wa Wilaya ya Busega, Paul Mzindakaya, licha ya matokeo kutotatangazwa alisema watu hawana budi kukubaliana na matokeo na kusema kitendo cha Dk Kamani kwa kuhusika kwenye vurugu hizo ni cha kibinadamu.
“Aliyeshinda ameshinda tu hakuna namna. Kilichofanywa na Waziri Kamani kumpiga msimamizi huyo ni mambo ya binadamu tu… lakini walioshindwa lazima wakubali matokeo na lazima yatangazwe,” alisema Mzindakaya.
Halmashauri Kuu ya CCM iliagiza kurudiwa kwa kura za maoni za ubunge kwenye jimbo hilo baada ya kubaini kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa kanuni. Katika kura za Awali, Dk Kamani na Dk Chegeni, kila mmoja kwa wakati wake alijitangaza kuwa mshindi, lakini baada ya matokeo rasmi kutangaza Dk Chegeni aliibuka mshindi kwa kupata kura 13,048 dhidi ya 11,829 za Dk Kamani.
Jana, vurugu zilianza saa 4:00 asubuhi baada ya Dk Kamani, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Simiyu, kuingilia kati wakati Mabiya, ambaye ni katibu wa Wilaya ya Meatu, akianza kutangaza matokeo.
Vurugu hizo zilisababisha wafuasi wanne wa Dk Kamani kukamatwa na polisi. Walikuwa wakigomea ujumlishaji matokeo, lakini baada ya kushindwa kuzuia, walianza kupiga huku wakitukana, hali iliyosababisha ofisa wa polisi Wilaya ya Busega aliyefahamika kwa jina moja la Nyaoga, kutoa onyo.
Hali iliyosababisha wananchi waliokuwa kwenye uwanja wa ofisi za CCM wilayani Busega, kushangilia huku wakiimba: “Tuna imani na Chegeni, Chegeni jembe, Kamani siyo chaguo letu.”
Baada ya Polisi waliokuwa na silaha kuimarisha ulinzi, Mabiya alisimama kutangaza matokeo lakini akakatishwa baada ya kurukiwa na watu walioonekana kumuunga mkono Waziri Kamani na kupigwa makonde mbele ya polisi na Mzindakaya.
Kipigo hicho kilimfanya Mabiya akimbilie ndani ya ofisi za chama hicho na kuacha askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakitumia nguvu kudhibiti watu hao.
Wakati wote wa vurugu hizo, Dk. Chegeni alikuwa amesimama pembezoni mwa ofisi za chama hicho akishuhudia matukio hayo, lakini baadaye akaondoka akiwa amepanda gari lake huku akishangiliwa.
Baada ya polisi kufanikiwa kutuliza ghasia, Mabiya alisimama tena kutangaza matokeo hayo, lakini Dk Kamani alimfuata na kumshambulia kwa makonde, hali iliyozua tafrani kubwa zaidi.
Wafuasi wanne wa waziri huyo walikamatwa.
Lakini mtu wa karibu na Dk Kamani alikanusha waziri huyo kumshambulia msimamizi wala kuhusika kwenye vurugu.
“Hivi unamfahamu mheshimiwa Kamani? Ni mtu muadilifu na wala asingeweza kupigana,” alisema mtu huyo baada ya Waziri Kamani kutopatikana kuzungumzia suala hilo.
“Tunachokipinga sisi ni Chegeni kushinda usiku mzima na viongozi wa wilaya wakihesabu kura wakati watu wetu sisi hawakuwapo. Tunauliza ameshindaje, hawasemi.”
Alilaumu kitendo cha polisi kukamata watu watatu waliokuwa wanamuunga mkono Dk Kamani wakati kwenye vurugu hizo kulikuwa na watu wa pande zote.
Dk Kamani aliondoka eneo hilo saa 5:12 na gari aina Toyota Land Cruiser huku kukiwa na ulinzi mkali wa polisi. Matokeo ya awali ya kura hizo yalionyesha kuwa Dk Chegeni alikuwa anaongoza kwa tofauti ya takriban kura 2,300.
Chegeni anena
Akizungumzia sakata hilo, Dk Chegeni alisema:“Sikutarajia kama mwenyekiti wa CCM wa mkoa, mbunge na waziri aliyekuwa mgombea urais na mzee wa familia kumpiga msimamizi wa uchaguzi.
“Kitendo cha kumshambulia msimamizi wa uchaguzi ni aibu na kinadhalilisha nafasi na utu wake. Akiwa kiongozi. alipaswa kusoma alama za nyakati siyo kupiga watu. Kama nisingekomaa mimi lolote lingeweza kutokea maana uchaguzi uliopita alichakachua.”
Rufiji
Kwenye jimbo la Rufiji, katibu wa CCM wa wilaya, Musa Liliyo alisema Waziri Seif alishindwa baada ya kupata kura 5,010 dhidi ya Mohamed Mchengerwa aliyeshinda kwa kupata kura 6,002.
Katibu huyo aliwataja wagombea wengine walioshiriki uchaguzi huo na kura zao kwenye mabano kuwa ni Hassan Sule (325), Shaaban Matwebe (126), Mohamed Salehe Afif (121), Jamal Rwambo (78) Juma Kiolobele (51) na Tano Seif Mwera (17). Hata hivyo, Dk Seif alikubali matokeo hayo akisema hayatasababisha ahame CCM.
“Haiwezekani katika baadhi ya vituo, inaonyesha idadi ya watu waliojiandikisha ni 300, lakini waliopiga kura ni 800, huu ni uhuni mkubwa unaokivuruga chama chetu cha CCM,” alisema Dk Seif.
Dk Seif anabainisha kuwa hatishwi na matokeo hayo kwa kuwa kwa taratibu za CCM, wingi wa kura si kigezo cha mwisho mtu kupitishwa na chama kugombea nafasi aliyoshinda.
Kwa mujibu wa Dk Seif, mwanasiasa yeyote aliyebobea hawezi kuhama chama kwa sababu ya kushindwa kwenye uchaguzi, hivyo hafikiri kabisa kuondoka CCM ila ametoa wito kwa viongozi kuzitazama upya taratibu za namna ya kupata haki pale mtu anapokuwa ameonewa.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Wilaya ya Rufiji, Musa Nyelesa amekiri kuwepo kasoro katika uchaguzi huo na kubainisha kuwa hata hivyo idadi ya wapigakura ilikuwa ndogo ikilinganishwa na uchaguzi uliopita.
Nyelesa alikitahadharisha chama hicho kuwa makini ili CCM iendelee kuwa chama cha wananchi, vinginevyo kitakuwa chama cha matajiri na wafanyabiashara wakubwa ambao hutumia fedha nyingi kupata madaraka.
“Tumeshuhudia genge kubwa la wahuni waliotoka Dar es Salaam kuja kusimamia kura hapa Rufiji. Hawa watu wametumia kila aina ya mbinu kuhakikisha kuwa mtu wao anapita katika mchakato huu, hii si sawa, ila kwa kuwa nina imani na chama changu najua kitarekebisha hizi kasoro,”alisema Nyelesa.
Kuhusu ushindi huo, Mchengerwa alisema: “Matokeo hayo ni faraja kwa Wanarufiji na yamenipa somo kwamba natakiwa kuwatumikia Wanarufiji na si kuwa kiongozi wao.”
Makete
Waziri mwingine, Dk.Binilith Mahenge ameanguka baada ya kupata kura kura 7,885 huku Dk Norman Sigala King akipata kura 8,838.
Katibu wa CCM wa Mkoa wa Njombe, Hosea Mpagike aliwataja wagombea wengine kuwa ni Bonic Mhami, aliyepata kura 124, Fabian Nkinga (74) na Lufunyo Nkinda (42).
Matokeo hayo yanasubiri kupitishwa na Kamati Kuu ya CCM.
Ukonga
Jimboni Ukonga, matokeo ya marudio ya kura za maoni yameendelea kumpa ushindi Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa baada ya kupata kura 10,965 dhidi ya mpinzani wake Ramesh Patel aliyepata kura 6,960.
“Huwezi kutofautisha Ukonga na Silaa, wananchi wananikubali. Ndiyo maana niliamua kukaa kimya wakati haya yote yakitokea kwa sababu mimi ni kiongozi wa CCM ninajua nini ninachokifanya,” alisema Silaa.
Habari hii imeandaliwa na Shaban Lupimo na Bakari Kiango wa Mwananchi

No comments: